22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

SIASA ZILIVYOZALISHA GENGE KUBWA LA ‘UNGA’ JAMAICA

 

 

Na Luqman Maloto,

SHOWER Posse ndilo genge kubwa la unga Jamaica. Shower Posse haliishii kuwa genge la biashara ya dawa za kulevya, bali pia mtandao mkubwa zaidi wa uhalifu wa mipango (organized crime) kuwahi kutokea Jamaica kisha kusambaa duniani.

Mwasisi wa genge hilo ni nani? Ujasiri na wazo la kuanzisha mtandao mpana wa biashara ya dawa za kulevya aliupata wapi? Ni hapo unaweza kuona chuki za kisiasa zilivyo kirusi hatari kwenye jamii.

Christopher Coke (Dudus) ambaye nchini Jamaica hufahamika kama President (Rais), aliyefungwa miaka 23 jela, nchini Marekani mwaka 2012, ndiye kiongozi wa Shower Posse.

President Dudus alichukua mamlaka ya uongozi wa Shower Posse kutoka kwa baba yake, Lester Lloyd Coke ambaye alifariki dunia mwaka 1992. Enzi za uhai wake, Lester Coke, alifahamika zaidi kwa majina ya Jim Brown na Ba-Bye.

Lester alilitwaa jina la Jim Brown kutoka kwa nyota wa zamani wa mchezo wa American Football ambaye alikuwa pia mwigizaji wa sinema, Hollywood, Marekani.

Kimsingi, Lester alikuwa akipenda kwenda kwenye kumbi za kuonesha filamu, akawa anavutiwa zaidi na sinema za Jim Brown, ni hapo akaamua kujitangaza kuwa yeye ni Jim Brown wa Jamaica.

Alipoanza kujiita Jim Brown, ilikuwa kama mchezo. Alikuwa kijana mdogo ambaye hakudhaniwa kuwa angepata umaarufu wa kuitikisa mpaka Serikali ya Marekani. Hata hivyo, baadaye Lester alipaa kwa umaarufu kupitia jina la Jim Brown kuliko mwenye jina lake.

Mwanzo wa ubaya

Jim Brown (Lester) anatambulishwa kama mmoja wa watu wabaya zaidi kuwahi kuishi duniani. Hata hivyo, hakuzaliwa mbaya isipokuwa alibadilishwa na tukio lililompata kutokana na chuki za kisiasa.

Jim Brown alikuwa kijana mpole kama ambavyo anasimuliwa kwenye documentary ya Lords of the Mafia ambayo msimuliaji wake ni Mmarekani Robert Stack, huku ndani yake kukiwa na maelezo ya watu mbalimbali ambao walimfahamu Jim Brown enzi zake tangu akiwa mtoto.

Vile vile ipo makala iliyochapishwa na gazeti la The Cleaner la Jamaica, yenye kichwa The Rise And Fall Of The Coke Empire (Kupanda na Kuporomoka kwa Utawala wa Coke), nayo pia inathibitisha kuwa Jim Brown nyakati za mwanzo za ujana wake, alikuwa mtu mzuri lakini aliharibiwa.

Makala hiyo ya Juni 25, 2010, mwandishi Gary Spaulding, anarejea kile kilichosimuliwa kwenye documentary ya Lords of the Mafia kuwa Jim Brown alikuwa kijana bora na mtulivu kabla hajakumbwa na mtikisiko wa machafuko ya kisiasa.

Spaulding ili kupata taarifa za kutosha kuhusu Jim Brown, alizungumza na rafiki wa zamani wa bilionea huyo wa dawa za kulevya, anayeitwa Byer Mitchell (Carl), anayesema kuwa tukio la Jim Brown kujeruhiwa kwa risasi tano mwaka 1966 ndilo lililombadilisha kabisa.

Carl anasema kuwa kila aliyemwona Jim Brown alipokuwa mdogo tangu akisoma, alimpenda kwa jinsi alivyoheshimu watu. Alikuwa kati ya vijana wachache wa Kijamaica walioonesha juhudi kubwa ya utafutaji wa maisha. Baada ya shule alianza kufanya shughuli halali mpaka alipopigwa risasi tano.

Tukio la kupigwa risasi

Mwaka 1966, wakati Jamaica ikijielekeza kwenye Uchaguzi wa Rais uliofanyika mwanzoni mwa mwaka 1967, nchi hiyo ilikumbwa na machafuko. Wafuasi wa vyama vya Jamaica Labour Party (JLP) na Peoples National Party (PNP), walirushiana risasi.

Ni machafuko hayo yaliyomsababishia majeraha ya risasi kijana asiye na hatia, Jim Brown ambaye alipigwa risasi tano. Kila mmoja aliamini Jim Brown amefariki dunia kutokana na mashambulizi hayo.

Hakuna mtu ambaye alikuwa tayari kujitokeza kwenda kumkagua Jim Brown. Ukimya ulitawala. Hofu ilikuwa kubwa mno kwenye Jiji la Kingston. Wanasiasa waliwatumia vibaya vijana wa ghetto kwa ajili ya kufanya mashambulizi ya risasi mitaani. Watu wasio na hatia waliuawa, wanasiasa walibaki salama.

Alitokea mtu mwenye baiskeli ambaye alimsogelea Jim Brown alipokuwa amelala na kubaini kwamba hakuwa amekufa. Alimwinua na kumbeba mpaka hospitali ambako alilalazwa kwa muda mrefu akitibiwa majeraha ya risasi.

Waliomfahamu Jim Brown walisikitika sana, maana alikuwa kijana asiye na makuu lakini alijeruhiwa bila kosa lolote. Hata uchaguzi ulipofanyika Februari 1967, Jim Brown alikuwa bado amelazwa hospitali.

Mbaya zaidi, vijana wa ghetto waliosababisha mitikisiko mitaani kwa mashambulizi ya risasi, walikuwa hawachukuliwi hatua stahiki. Hata waliokamatwa, walishikiliwa kwa muda kisha waliachiwa.

Hali ilikuwa hivyo kutokana na ukweli kwamba siasa za Jamaica, vijana wa ghetto walikuwa ndiyo mitaji ya wanasiasa. Sera na kushindanisha ubora wa ilani za uchaguzi, hakikuwa kitu ambacho wanasiasa waliegemea Jamaica, badala yake walitumia vijana kutekeleza vitendo viovu na mchafuko, hasa kupigana risasi.     

Vijana hao hawakukaa jela kwa sababu wanasiasa waliowatumia ndiyo ambao waliwawezesha kutoka nje mapema. Hiyo ndiyo sababu mazingira kisiasa miaka ya 1990 nchini Jamaica yalikuwa mabaya kupita kiasi.

Kitendo cha kujeruhiwa kwa risasi, vile vile hali hiyo ya wanaofanya vitendo vya uharamia na kuua watu kutochukuliwa hatua inayotakiwa, kilikuwa sababu ya Jim Brown kubadili tabia na kugeuka mtu mbaya kwenye jamii.

Jim Brown, aliona kuwa ili aheshimike kwenye jamii lazima na yeye awe mtu mbaya, amiliki bunduki na ikiwezekana kumiliki kikundi cha wahalifu ambacho angekuwa anakiongoza kufanya matukio.

Carl aliliambia The Cleaner: “Alipopona majeraha ya risasi aligeuka mtu katili kuwahi kutokea duniani. Hakuwa tena Ba-Bye tuliyemzoea, mtu mpole, mstaarabu mwenye kufanya mambo yake kwa mpangilio. Mimi simjui kama Jim Brown, namfahamu kama Ba-Bye, alipotoka hospitali, haikuwa rahisi kumfananisha na yule wa siku zote.”

Mwanzo wa Shower Posse

Jim Brown alipopona alianza kujiingiza kwenye vikundi vya kiharamia. Naye aligeuka mtu wa magenge ya ghetto, akiwa mmoja wa vijana waliokuwa tishio kwa matumizi ya bunduki na kuua au kujeruhi watu wasio na hatia.

Hadi kufikia mwaka 1970, tayari Jim Brown alikuwa anamiliki mtandao wa vijana wa ghetto ambao aliwatumia kufanya vitendo vya uharamia na kuwalinda watu ambao alikuwa na maslahi nao.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Jamaica mwaka 1980, Jim Brown aliongoza genge lake la vijana wa ghetto kukipigania Chama cha Jamaica Labour Party (JLP), kilichokuwa kinaongozwa na Edward Seaga.

Mchuano ulikuwa mkali kuelekea uchaguzi kama ilivyo kawaida ya vyama viwili vikuu vya siasa nchini Jamaica, ambavyo ni JLP na Peoples National Party (PNP). Kila chama kilikuwa na genge lake.

Kiongozi wa PNP, Michael Manley ambaye alikuwa Waziri Mkuu, alikuwa na kauli mbiu ya chama chake ya Power, JLP wao walikuwa na kauli mbiu ya Shower ambayo ilikuwa jawabu kwa Power ya PNP na Manley.

Kutokana na kuongoza genge lake la vijana wa ghetto kumlinda Seaga na viongozi wengine wa JLP, Jim Brown alipita na kutambulika kuwa mtu nyeti katika chama hicho, akionekana nguzo muhimu katika eneo la ulinzi wa chama.

Harakati za Jim Brown zilizaa matunda kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 1980, baada ya kufanikiwa kuiwezesha JLP kushinda uchaguzi dhidi ya PNP, hivyo Seaga alifanikiwa kuwa Waziri Mkuu na kumwondoa Manley.

Kitendo cha JLP kushinda mamlaka ya nchi, ndiyo ulikuwa mwanzo mpya wa Shower Posse katika ulimwengu wa biashara ya dawa za kulevya. Jim Brown aliamua kutumia genge lake la vijana wa ghetto na kuingia rasmi kwenye usafirishaji wa bangi kutoka Jamaica kwenda Marekani.

Jina Shower lilitokana na kauli mbiu ya JLP ya Shower na Posse kwa maana ya genge, hivyo Shower Posse lilianza kazi rasmi ya kusafirisha bangi kutoka Jamaica kwenda Marekani mwaka 1980.

Kadiri biashara ilivyokuwa inachanganya ndivyo Shower Posse ilivyotanuka, hivyo kujikita pia katika biashara ya silaha (bunduki) na dawa za kulevya aina ya cocaine. Ni hapo Jim Brown alibadilika ghafla na kuwa tajiri wa kuogopwa duniani.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,215FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles