25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

NAMHESHIMU ASKOFU GWAJIMA – MDEE

Na ELIZABETH HOMBO-DODOMA


SIKU moja baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kumtaka Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kumwomba radhi Spika wa Bunge,Job Ndugai kwa tuhuma za kumtukana, mbunge huyo amesema kauli hiyo ya kuudhi hakumtolea Spika.

Juzi, wakati akihubiri katika kanisa lake lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam juzi, Askofu Gwajima, alimtaka Mdee amwombe radhi Spika Ndugai kwa kumtukana, kwani si vyema kumtukana mkuu wa mhimili huo.

“Ukiongoza wananchi unatakiwa uwe mfano kwa maneno na matendo yako na uwe na moyo wa kuzuia hasira zako.
“Mimi huwa siangalii unatoka wapi, ukifanya lisilo sawa tunakusaga. Halima Mdee ni mbunge wangu na ni rafiki yangu lakini jambo alilolifanya halikubaliki na hatuwezi kukemea wengine halafu wewe (Mdee) tukakuacha.

“Nenda kaombe msamaha yaishe, ni afadhali ungeanguka chini ukalia ukapiga kelele…wewe ni mbunge mzuri lakini koma kumwambia maneno mabaya spika,” alisema Gwajima.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mdee alisema anamheshimu Askofu Gwajima na ni mtu wake wa karibu, kwa hiyo hawezi kujibishana naye.

Alisema huenda alichokitafsiri Askofu Gwajima, si kile kilichotokea hivyo hawezi kumbishia zaidi kwakuwa yeye ni binadamu anaweza kuwa ameteleza.

 “Unajua mimi ninamheshimu sana Askofu Gwajima kwa hiyo si mtu ambaye nitajibishana naye ni mtu wangu wa karibu, lakini kama alikuwa anaona ana ushauri best option angenipigia na kunipa ushauri kama ambavyo nimekuwa nikipokea ushauri mbalimbali kutoka kwake kwa sababu mimi ni binadamu nahitaji kushauriwa pale ninapokosea”alisema Mdee.

Aidha mbunge huyo wa Kawe alisema siku ya Uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki (EALA), wakati wa mabishano hakulenga kumtukana Spika bali kauli yake aliielekeza kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla ambaye alidai alitaka kupotosha.

Alisema amekwishaomba radhi kwa muhusika kupitia mahali panapohusika.

Alhamisi iliyopita, Spika Ndugai alimtaka Mdee kufika bungeni ndani ya saa 24 vinginevyo akamatwe na polisi kutokana na kumtukana kiongozi huyo wa Bunge.

Hata hivyo, Jumamosi iliyopita mbunge huyo alihojiwa na Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa takribani saa moja.

“Mtu akisikiliza ile clip ya mabishano utajua kwamba nilikuwa nimemlenga Kigwangalla kwa sababu alitaka kuvuruga utaratibu. Wakati haya matukio yanatokea Spika alikuwa amekaa alikuwa hazungumzi.

“Kwa hiyo sikumlenga Spika kabisa ni kwa bahati mbaya imelazimika ionekane hivyo all in all either nilimlenga Kigwangalla kwa mtu yeyote ile lugha inaudhi na nimeshaomba radhi katika mamlaka husika ambayo imeniita. Lakini katika mazingira yale ya siku ile ingekuwa ni mtu dhaifu zaidi yangu angefanya kitu kibaya zaidi,” alisema.

Alihamisi iliyopita baada ya maswali na majibu, Spika Ndugai baada ya kuombwa miongozo na wabunge juu ya kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyoitoa baada ya Uchaguzi wa EALA, alisema.

“Naendelea kusema tena kwa mara nyingine, safari hii tuko hapa kwa muda mrefu, tuko hapa karibu miezi mitatu na kila mnachokifanya hapa tunamwona mmoja mmoja wenu kwa tabia zenu na mwenendo na nimeshasema sana na tuko tayari kuleta nidhamu ndani ya Bunge,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles