Nafasi ya vyama vidogo uchaguzi wa urais Marekani

Wagombea urais wa vyama vikuu Hilarry Clinton na Donald Trump
Wagombea urais wa vyama vikuu Hilarry Clinton na Donald Trump
Wagombea urais wa vyama vikuu Hilarry Clinton na Donald Trump

NA JOSEPH HIZA,

KWA wasiofuatilia vyema siasa za Marekani wanaweza wakadhani kuna vyama viwili tu vya siasa nchini humo; Democratic kinachotawala sasa na hasimu wake Republican, kumbe sivyo.

Taifa hilo lina vyama vingi ukiondoa hivyo viwili vinavyotawala kwa kupokeza, huku vyama maarufu zaidi vikiwa Libertarian, Kijani (Green Party) na Kikatiba (Constitutional Party).

Libertarian ni chama kinachopigania uhuru wa mawazo, dini, kufikiri na kutenda, ukombozi wa kiraia na kupinga vita.

Chama cha Kijani huendekeza siasa za mazingira, ukombozi wa kiraia na kupinga vita huku Chama cha Kikatiba kikiwa cha sera za uhafidhina wa kijamii na haki za kidini.

Lakini pia kuna vyama vingine vya siasa ambavyo vimeishia katika ngazi za majimbo, au ambavyo havina lengo la urais. Vyama vya aina hii si makusudio ya makala haya!

Hivyo basi, vyama hivyo katika umoja wao vinajulikana kama ‘Chama cha Tatu’ yaani baada ya Democratic na Republican na wagombea wake hujulikana kama wagombea wa ‘Chama cha Tatu’ bila kujali kama wanatokea vyama tofauti.

Kwa sababu hiyo wagombea kutoka vyama hivyo vidogo kwa kawaida huwa hawana athari kubwa katika chaguzi za urais nchini humo. sihusishi zile za majimbo!.

Hata hivyo, ukifuatilia mwenendo wa uchaguzi wa mwaka huu, kuna sababu nzuri ya kuamini 2016 unaweza kuwa tofauti kidogo.

Wagombea wa chama cha tatu wana mwaka mzuri usio wa kawaida hasa katika jimbo la Colorado na mengine yenye ushindani (swing states).

Ralph Nader alijipatia zaidi ya asilimia tano Colorado mwaka 2000, kulinganisha na chini ya asilimia tatu kitaifa na Ross Perot alipata asilimia zaidi ya 23 mwaka 1992 huku akichukua asilimia 19 kitaifa.

Na bila kumsahau Tom Tancredo alipata asilimia 36 mwaka  2010, akiwakilisha chama cha Kikatiba, wakati mteule wa Republican alipata asilimia 11 tu jimboni humo.

Naam, ni ndoto kwa mgombea urais wa chama cha tatu kupata ushindi kitaifa. Mgombea wa Libertarian, Gary Johnson na wa Green, Jill Stein pia waliwania urais mwaka 2012 na baina yao walijipatia chini ya asilimia 1.4 ya kura.

2000 ilikuwa mara ya mwisho kwa chama cha tatu kupata zaidi ya asilimia moja. Na hakuna mgombea wa chama cha tatu aliyeshinda hata jimbo moja kitaifa tangu mwaka 1968.

Hilo linaweza kushangaza kutokana na ari inayoonekana kwa wagombea wa chama cha tatu miezi kadhaa kabla ya chaguzi.

Kwa kawaida, msimu wa kiangazi huonekana mzuri kwa wagombea wa vyama vidogo.

Ilikuwa Juni 1992 wakati Perot akiwaongoza Bill Clinton na Rais George H.W. Bush katika kura za maoni pamoja na kuwa alijikuta akishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa Novemba mwaka huo.

John Anderson alikuwa akitamba na asilimia 20 ya kura za maoni Juni ya 1980 lakini akaishia kupata asilimia saba tu ya kura ulipofanyika uchaguzi Novemba ya mwaka huo.

Lakini pia 2016 unaonekana si mwaka wa kawaida wa uchaguzi, kwa kitu kimoja, wagombea wa vyama vidogo wanaendelea kupata uungwaji mkono fulani hata baada ya mikutano mikuu ya vyama.

Johnson bado ana asilimia nane ya uungwaji mkono, ambao ni mzuri kuliko mgombea yoyote wa vyama vidogo aliyepata katika kura za maoni Agosti tangu mwaka 1996.

Stein ana asilimia nne. Kuna uwezekano kwa kiwango hicho kushuka kwa kadiri kampeni zinavyoendelea, lakini inaonekana wanajitutumua.

kwanini? Naam, wagombea wa vyama vikuu katika hali isiyo ya kawaida wana viwango vibaya vya uungwaji mkono. Hillary Clinton na Donald Trump ni wagombea wanaochukiwa zaidi katika historia ya siasa za taifa hilo kwa nyakati hizi za kisasa.

Kiwango cha uungwaji mkono kwa Clinton hata hivyo, hakionekani kuwa kibaya kwa harakati zake za urais kulinganisha na cha mpinzani wake.

Amefanikiwa kuteuliwa na Democrats, hata wale ambao walimuunga mkono mpinzani wake Bernie Sanders wakati wa mchakato wa kura za uteuzi ndani ya chama wanamuunga mkono.

Na hiyo ni moja ya sababu inayomfanya afanye vyema katika kura za maoni tangu kumalizika kwa mikutano mikuu ya vyama hivyo.

Kura ya hivi karibuni ya maoni iliyoendeshwa na Chuo Kikuu cha Monmouth kwa wakazi wa Coloradan ilionesha asilimia 93 ya wafuasi wa Democrats wanamuunga mkono Clinton.

Simulizi ni tofauti kwa Trump, viwango vyake ni vibaya kulinganisha na Clinton na ni wazi vinaathiri fursa yake ya kujipatia kura kutoka kwa wanachama wenzake wa Republicans.

Katika kura hiyo hiyo ya Monmouthl, ni asilimia 78 tu ya wana Republicans wanamuunga mkono Trump. Tofauti na Clinton, wanachama waandamizi wa Trump wamefikia hatua ya kuendesha kampeni ya kutompigia kura.

Moja ya hotuba za kukumbukwa wakati wa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Republican, ilikuwa ya tamko la Ted Cruz kuwa wana Republican wanapaswa kupiga kura kwa ufahamu wao, akimaanisha kutomuunga mkono Trump.

Ishara mbaya kutoka vigogo wa Republican kwamba hawafurahishwi na Trump kuwa mgombea wao ni pigo kubwa kwake.

Inawaambia wapiga kura wa Republican kwamba wao bado wanaweza kubakia kuwa wana-Republican watiifu hata kama hawatamuunga mkono mgombea wao huyo.

Kwa wale, wana-Republican wasiomtaka Trump, lakini pia wasio tayari kuisaliti dhamira yao dhidi ya chama chao kumpigia Clinton, wengi  wataelekea kwa mbadala- Johnson.

Kama m-Libertarian, Johnson ana vitu vya msingi vinavyoshahibiana na Republican kama vile wazo la serikali ndogo, kodi kidogo na kupunguza kanuni na kadhalika.

Wapiga kura wa Republican wasiopendezwa na Trump na ambao hawako radhi kumpa kura Clinton wana mbadala- Johnson.

Uungwaji mkono wa Stein si wa kutia moyo kama wa Johnson, lakini akiwa na asilimia nne, anafanya vyema kuliko mwaka 2012, na hivyo ana uwezekano wa kuvuta kura za wana-Democraric waliberali zaidi wasiompenda Clinton.

Mwaka 2016 hautatoa rais kutoka chama cha tatu, bali unaoweza kukifanya kiamue chama kikuu kitakachoingia Jumba Jeupe!.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here