29.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Profesa Lipumba inawezekana ‘anatumika’ kuivuruga CUF

Profesa Lipumba
Profesa Lipumba

NA JUSTIN DAMIAN,

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Chama cha Wananchi (CUF) kilifanya Mkutano Mkuu  Maalumu jijini Dar es Salaam uliokuwa na lengo la kujaza nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Mkutano huo haukuweza kumalizika baada ya wafuasi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kupinga uamuzi waliouita wa kura za kutengenezwa za kuridhia kuondoka kwa Mwenyekiti wao aliyejiuzulu katika nafasi yake Agosti mwaka jana.

Itakumbukwa kuwa, Julai mwaka huu, Profesa Lipumba aliutangazia umma kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu na kutaka kurudi katika nafasi yake ya uenyekiti hali iliyolazimu askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuingilia kati na kuwatawanya wafuasi hao.

Mkutano huo ulitawaliwa na jazba pamoja na mvutano mkali kati ya wafuasi wa mwenyekiti huyo wa zamani na kundi linalomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Wakati vugu vugu la Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana likipamba moto na hasa wakati Edward Lowassa akihamia Ukawa baada ya jina lake kuenguliwa kugombea urais kupitia CCM, Profesa Lipumba alipinga wazo la Lowassa kugombea urais kupitia umoja huo wa Ukawa.

Hata hivyo, baadaye alibadilika na kukubali wazo hilo huku akimmwagia sifa kede kede Lowassa kama Rais anayefaa kuiongoza Tanzania.

Baadaye akabadilika akisema kuwa hawezi kukubali Lowassa kugombea nafasi ya urais kupitia Ukawa na kuonya kuwa endapo atapitishwa atajiuzulu nafasi yake ya uenyekiti wa CUF jambo ambalo alilifanya.

Kwa kuunganisha matukio hayo mawili na hili la sasa la kutaka kurudi kwenye nafasi yake ya uenyekiti, utagundua kuwa Profesa Lipumba ambaye ni msomi na mchumi nguli, ni mwanasiasa asiyekuwa na msimamo.

Binafsi nilitegemea kuona msomi kama Profesa Lipumba akiwa mfano wa kuigwa kwa wanasiasa wengine kwa kufanya maamuzi ambayo yatakwenda sambamba na elimu, heshima pamoja na uzoefu wake.

Sina wasiwasi juu ya uwezo wake wa kufikiri pamoja na kupima mambo ila nina wasiwasi kama anayoyafanya anayafanya kwa matakwa yake au pengine kwa ushawishi kutoka sehemu fulani fulani.

Haiingii akilini msomi na mwanasiasa mkongwe kama yeye akazungumza hili kesho yake akazungumza lingine na kesho kutwa akazungumza lingine tena. Kwa mtizamo wangu naona kama kuna ajenda ya siri ndani ya hii ‘double standard’ au kubadilika badilika anakokufanya msomi huyu.

Profesa Lipumba bado hajaweza kuuambia umma na hususani wanachama wa CUF kwanini ameamua kurudi katika chama hicho wakati yale ambayo yalimfanya aondoke pengine bado yapo.

Wakati akijiuzulu uenyekiti wa CUF Agosti mwaka jana, Lipumba aliutangazia umma kuwa hatajihusisha na siasa tena na badala yake atajikita katika kuishauri Serikali namna ya kujenga uchumi imara na kutengeneza ajira lakini cha kushangaza leo tena anaibukia kwenye siasa.

Kwa wale wanaofuatilia siasa watakubaliana na mimi kuwa Lipumba anapwaya kwenye siasa. Pamoja na watu kusema siasa ni mchezo mchafu, lakini ukweli unabaki pale pale kuwa mwanasiasa mzuri ni yule ambaye anasimamia kile anachokiamini bila kutetereka.

Kitendo cha Lipumba kubadilika mara kwa mara kinaonyesha kutokuwa na msimamo imara na hivyo kumfanya akose sifa ya uongozi.

Kwa upande wangu nadhani ni muda  mwafaka kwa Profesa Lipumba kujiuzulu siasa ili kutunza heshima yake na kufanya kazi nyingine katika fani yake ya uchumi kama kuishauri Serikali jambo ambalo nadhani linaweza kuwa na tija kuliko siasa ‘maji taka’ anazozifanya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles