NA ELIZABETH HOMBO,
UMAARUFU wa jina la Dk. Tulia Ackson, uliibuka wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana baada ya kuteuliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alikuwa miongoni mwa mawakili wa Serikali waliopambana na kushinda kesi ya mita 200 iliyofunguliwa Mahakama Kuu na kada wa Chadema ambaye alitaka Mahakama itoe tafsiri kuhusu Sheria ya Uchaguzi 104 (1) sura ya 343 iliyorejewa mwaka 2010.
Miezi miwili baadaye akateuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge na baadaye akachaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge.
Wiki iliyopita MTANZANIA lilikutana na kufanya naye mahojiano maalumu ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia mwenendo wa Bunge na tuhuma ambazo amekuwa akielekezewa na wabunge wa Kambi ya Upinzani bungeni.
MTANZANIA: Ni changamoto zipi ulizokumbana nazo wakati wa Bunge la Bajeti?
TULIA: Unajua Bunge la Bajeti ni tofauti na vikao vingine kwa sababu Katiba inaainisha wazi majukumu ya Bunge linaposhughulika na suala la bajeti. Kwa hiyo Serikali kazi yake inatayarisha bajeti na inaleta bungeni ili Bunge lifanye kazi yake ya kuishauri na kuisimamia Serikali.
Kwa hiyo wakati wa Bunge la Bajeti ni wakati ambao Serikali inapata fursa kueleza utekelezaji wa bajeti iliyopita na walikofikia, pia matazamio ya mwaka mwingine na wanaomba fedha kiasi gani ili Bunge liweze kuidhinisha.
Sasa changamoto ni kubwa kwa sababu Katiba inaonyesha kwamba Bajeti ya Serikali isipopita yaani Bunge likikataa bajeti maana yake ni kwamba Rais atavunja Bunge na hatua hiyo maana yake ni kuwa uchaguzi unarudiwa.
Kwa hiyo ndio maana Bunge la Bajeti huwa ni zito kidogo na changamoto kubwa huwa ni kuhakikisha kwamba Serikali inapoleta bajeti inalishirikisha Bunge kwa maana ya kwamba linafanya utaratibu wa kuisimamia Serikali kupitia kamati halafu baadaye ndio tunaenda wote kwenye Bunge zima.
Changamoto nyingine kubwa huwa ni kunasibisha mahusiano baina ya wabunge hawa wanaofanya kazi kwenye kamati lakini pia Serikali.
Kwa sababu hivi vyombo viwili visipokutana vikawa na mawazo sawa wakati wa bajeti maana yake bajeti ya Serikali itapata wakati mgumu kupitishwa.
Kwa hiyo changamoto inayomkabili mtu yeyote anayesimamia Bunge la Bajeti ni hiyo, kuhakikisha kwamba bajeti ya Serikali inakuja kwa namna ambayo Bunge linaikubali si lazima likubali kila kitu lakini kwa maana kwamba tunakubali baadhi ya mambo na mengine hupaswa kurekebishwa, ndivyo inavyokuwa.
Lakini pia kuna wabunge ambao hawako serikalini kwa hiyo lazima wawe na muda wa kusoma ili wanapokosoa na kushauri Serikali nayo inatoa majibu yanayoshadadia sababu ya kufanya hivyo.
Na bajeti ya mwaka huu ilikuwa tofauti na ya vipindi vilivyopita kwa sababu asilimia 40 ya bajeti imepelekwa kwenye maendeleo kwa hiyo mambo mengine yaliyozoeleka huko nyuma kuwa kwenye vifungu tofauti sasa hivi yamehama kwenda kwenye maendeleo.
MTANZANIA: Katika Bunge lile tumeshuhudia namna wabunge wa upinzani walivyotoka na kususia vikao, unadhani pengine msingi wa haya yote ni nini?
TULIA: Hapo labda niseme vyanzo vinaweza kuwa vingi lakini mengi nimeyasoma kwenye vyombo vya habari, isipokuwa nadhani kama wangeulizwa wao, mathalan kwanini wanasusia wangetoa maelezo mazuri zaidi.
Lakini yale ambayo waliyaeleza kwanini wanasusia vikao utakumbuka hilo jambo halikuanza kama la bajeti, lilianza kama Serikali ilianza na uamuzi fulani ambao wabunge walitaka kuhoji ambalo ni jambo zuri kwa sababu ndiyo kazi yao, lakini sasa mjadala huo ufanyike wakati gani inategemea mtu anayeendesha vikao ndio maana anayeendesha kikao anaweza akampa nafasi A na asimpe B kulingana na utashi wake anavyoona.
Kwa hiyo yale ambayo waliyaeleza wao ambayo hawana imani na mimi yako mengi zaidi. Kwa yale waliyokuwa wameyaeleza ni mengi lakini mojawapo wao walichukua hatua zaidi, labda hilo naweza kulizungumzia kwa sababu liko kiofisi.
Walieleza pia kuhusu kurudisha fedha serikalini, nadhani unajua kuna zile Sh bilioni sita zilirudishwa serikalini sasa wameniunganisha kwenye hoja hiyo wakati sheria na taratibu ziko wazi kwa sababu Spika au Naibu Spika si ofisa masuhuli wa bunge, hilo ni jukumu la katibu.
Kwa hiyo kwamba Naibu Spika karudisha fedha mimi si Katibu wa Bunge ambaye ndiye anayehusika na masuala hayo, unajua Bunge halitengenezi fedha, bali kasma yote inatoka serikalini pamoja na ambazo tunatumia sisi Bunge.
Kwa hiyo kwamba Naibu Spika karudisha fedha serikalini, mimi si mshika mafungu kwa kuwa kimsingi hakuna fedha ambayo naweza kuirudisha serikalini.
Kwa kawaida fedha zinazoanishwa na Bunge, lazima matumizi yake yaende yalikoelekezwa na kama haikufanyika na ukapeleka sehemu nyingine utakuwa umefanya makosa kwa sababu itakuwa hakuna maana ya bajeti, hivyo ukiona zimebaki unazirudisha.
MTANZANIA: Sababu nyingine waliyoitoa wabunge wa Ukawa ni madai ya kuendesha vikao kwa upendeleo, hili nalo unalizungumziaje?
TULIA: Kuhusu hilo niseme kuwa katika uendeshaji wa mabunge sioni kama suala hilo ni geni kwa sababu sisi huwa tuna vikao vyetu vya watu wanaosimamia Bunge, ambako utasikia changamoto zinazoshabihiana katika mabunge mengi yanayoendeshwa na nchi za Jumuiya ya Madola.
Kwa maana ya kwamba tukikaa bungeni pale kwa sasa tuna jumla ya wabunge 389, sasa hawa ni wengi sana na hawawezi kupata wote nafasi ya kuongea.
Kwa hiyo kiutaratibu wakisema kuwa napendelea; leo hii wewe ukiniomba nafasi ya kuongea nitakupa na utaniona niko sawa, lakini vikao vinaendelea, kesho utasimama sikupi nafasi nikampa mwingine sasa wewe unasahau kuwa jana nilikupa nafasi halafu unalalamika, sijui nilisimama mara kumi yaani naibu spika hata hanioni!
Mtu ambaye anayeweza kusema naibu anapendelea au hapendelei lazima afuatilie maamuzi niliyoyafanya bungeni kwamba ni mangapi ambayo kwa upande wa upinzani na CCM hayakwenda sawa.
Kwa hiyo kutoridhika kutokana na hilo ni katika hali ya kawaida. Nami nikiwa kiongozi naona sehemu mojawapo ya kusimamia jamii ina changamoto zake ambazo zitaendelea kwa miaka mitano Mungu akitupa uhai.
MTANZANIA: Kumekuwa na malalamiko kuwa ni kwanini wanaopewa adhabu mara nyingi ni wabunge wa upinzani, je, ina maana wale wa kutoka chama tawala huwa hawakosei?
TULIA: Unajua kuna namna ambayo adhabu zinavyotolewa bungeni huwa hutumia muda mrefu, ziko chache ambazo yeyote aliyeko kwenye kiti anaweza akatoa lakini nyingi zina utaratibu fulani ambao lazima ufuatwe, kwa mfano ukisema wanaopewa adhabu wengi ni wa upande wa upinzani mfano mmoja mzuri kulikuwa na malalamiko kuhusu Bunge kutorushwa ‘live’ na wakati huo mambo hayo yalikuwa yakitokea, ilikuwa Januari.
Sasa siku waliposimama kudai na kufanya vurugu wale wa CCM hawakufanya hivyo, adhabu zikaja kutolewa hapo baadaye.
Kwa hiyo hilo liwe wazi tu kuwa aliyekuwepo kwenye kiti aliwaona na kuwataja majina wakapelekwa kwenye kamati ya maadili.
MTANZANIA: Pia kuna madai kwamba hukutenda haki siku Mbunge wa Ulanga, Gudluck Mlinga, alipowatukana wabunge wanawake wa Ukawa, hebu tupe ufafanuzi juu ya hili.
TULIA: Jambo lilitokea kama leo habari ya vurugu ikatokea kesho sasa na wewe jiulize kwanini walisubiri kesho yake!?
Kama kiti kingekuwa kimekosea mtu angenyanyuka pale pale kwa sababu ni jambo la kawaida katika kikao kama kile.
Wakati vikao vinaendelea siku ile kuna mbunge wa Chadema alimtukana wa CCM, baada ya kumtukana kama ilivyo ujue wakati mwingine unavyoendesha kikao kila mmoja anaposimama na kusema neno ukisema uwe unasimama, inakuwa ngumu kwa sababu kuna kipindi vijembe huwa vinatawala.
Sasa maana yake hakutakuwa na vikao zaidi ya wewe kushughulikia vijembe, kwa hiyo inawezekana mmoja au wawili wakawa wanarusha vijembe lakini nane wakaendelea kujikita kwenye hoja iliyoko mezani kwa sababu kwenye mkutano mkubwa kama ule watu hawalingani akili.
Kwa hiyo siku hiyo alianza wa Chadema kutukana wa CCM huyu wa Chadema hakuambiwa chochote na aliyekuwa amekaa pale nilikuwa mimi.
Nikasema hicho alichosema huenda atajibiwa au something kwa hiyo hakuna aliyesimama lakini aliposimama Mlinga akaamua kutukana wakasimama afute kauli, nikasimama kwamba watulie wakaomba mwongozo kwamba afute nikamwambia Mlinga afute na alifanya hivyo na akaendelea kuchangia.
Baada ya hilo tukio nilisimama na kuagiza kwamba lugha hizo zote zifutwe kwenye hansard. Kesho tukarudi wakaona kufuta haitoshi…wakaja na hiyo habari sijui wajitoe kwenye chama sijui aombe radhi…
Mimi mwenyewe ni mwanamke, lakini pengine ni namna tofauti ya kuchukulia hayo mambo wao wanaosema wanawake walidhalilishwa laiti ungeona hansard walichonituna kuhusu mimi.
Maana walitukana ndani ya Bunge na actually Mlinga hajatukana lakini ulisikia nililalamika mahali kwamba nimetukanwa na Ukawa, wao hata waongee vibaya wanitukane mimi bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza kuwakasirikia kwa sababu itakuwa nashindwa kuwaongoza na mimi walinichagua kuwa kiongozi wao pia ni kama mzazi tu.
MTANZANIA: Unadhani ni kwanini migogoro ilizidi wakati ukiendesha vikao, pengine unadhani wanakudharau kwa sababu wewe ni mwanamke au kwa vile huna uzoefu na mabunge yaliyopita?
TULIA: Kwa kweli (kicheko) nadhani mtu mwingine angewasemea vizuri, lakini mimi huwa sipendi kuwawazia labda wanaleta dharau kwa sababu sijui mimi ni mwanamke au umri wangu, ni kweli hayo yote yanawezekana lakini sipendi kuwawazia.
Lakini kimsingi kuhusu uzoefu unajua zile kanuni hata wewe ungepewa uendeshe kikao ukishazielewa hazihitaji uzoefu wowote. Watalalamika si wao peke yao, ni jambo la kawaida nisingependa kufikiri japokuwa wengi wanafikiri hivyo.
Kwa sababu Mwenyekiti aliyewapeleka kwenye kamati ya maadili ni mzoefu wa siku nyingi yeye ndio alikuwa amekalia kiti. Uzoefu wake mbona ulimtuma hawa niwatoe nje na baadhi niwapeleke kwenye kamati, sidhani kama ni hoja sana.
Uzoefu unakuja tu pale unapotaka kufanya maamuzi fulani hapo ndio unaweza kuangalia wenzako waliamua nini huko nyuma, lakini zaidi kuendesha kikao inahitaji kuzielewa zile kanuni.
MTANZANIA: Tangu wabunge wa upinzani waliposema hawana imani na wewe, uliendesha vikao mpaka dakika za mwisho pengine ilikuwa ni kuwakomoa au?
TULIA: Nilishapata kuulizwa hilo swali huko nyuma, kanuni ziko wazi kwamba Spika ataongoza vikao asipokuwepo Naibu Spika ataongoza na asipokuwepo ni mbunge yeyote ambaye amechaguliwa anaweza akaongoza.
MTANZANIA: Spika wa Bunge alipata kusema kuwa Bunge hili lina wabunge wapya asilimia 70, hivyo kuwaongoza kunahitaji viongozi kuwa na uvumilivu wa hali ya juu, hili unalizungumziaje?
TULIA: Nisingependa kuongelea kauli ya Spika…wewe nimeshakupa mfano uvumilivu wa mtu kutakiwa akae chini zaidi ya mara 11 ni uvumilivu gani?
MTANZANIA: Pengine unadhani nini kinakosekana katika Bunge hili la 11 ambacho kinatakiwa kurekebishwa?
DK. TULIA: Sidhani kama kukosekana hasa kwa sababu hili ni Bunge jipya, kuna umuhimu wa wabunge kuambiwa ni mambo gani wanapaswa kuyafanya maana kuna mambo mengi hata mavazi kwa sababu wapo ambao wamekuwa wakirudishwa getini na walinzi kwa sababu mavazi yao si ya staha hivyo kuna mambo mengi. Lakini nikuhakikishie kuwa tunakoelekea kutakuwa kuzuri zaidi kuliko tulikotoka.