27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Nafasi nyingine kwa Yanga kujiuliza

YANGA (2)

NA ADAM MKWEPU,DAR ES SALAAM

NI nafasi nyingine ya kipekee kwa timu ya Yanga kujiuliza na kurekebisha makosa yao waliyofanya katika michezo iliyopita ya Kombe la Shirikisho Afrika wakati itakapocheza dhidi ya Medeama ya Ghana Julai 16 mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa Dar es salaam.

Yanga ambayo ipo kundi A  itaingia dimbani huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo miwili katika hatua ya makundi, ukiwemo wa ugenini dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria iliyopoteza kwa kufungwa bao 1-0 na mchezo wa nyumbani dhidi ya  TP Mazembe ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)  bao 1-0.

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara,Yanga ndio timu inayoshika mkia ikifuatiwa na Medeama ya Ghana yenye  pointi moja  katika kundi hilo  ambalo linaongozwa na TP Mazembe yenye point sita na kufuatiwa na Mo Bejaia yenye  pointi nne.

Yanga inakabiliwa na michezo minne  muhimu ambayo inatakiwa ishinde ili ifikishe pointi  12  na kufanikiwa kusonga hatua inayofuata.

Hata hivyo ili kufanikiwa kuzipata pointi hizo Yanga inatakiwa kujiuliza ilipokosea  kwenye michezo miwili iliyopoteza awali kabla ya kukutana na Medeama ya Ghana mwishoni mwa wiki hii.

Mchezaji wa zamani wa timu ya Yanga na mchambuzi wa soka wa masuala ya soka, Ally Mayai (Tembele) anasema kwamba kama Yanga ikipoteza  dhidi ya Medeama itakuwa imejikaanga yenyewe katika kundi hilo kwa sababu haitakuwa na nafasi ya kusonga mbele.

“Hawana cha kupoteza wanachotakiwa kukifanya ni kucheza soka la kushambulia  kwa kuwatumia zaidi ya washambuliaji watatu huku nafasi ya kiungo mkabaji ikifanya kazi yake ipasavyo.

“Matokeo ya sare  hayatosaidia kutokana na nafasi ya Yanga ilivyo, lazima wawe na mpango  wa kupata ushindi  ikilinganishwa na mchezo uliopita  dhidi ya TP Mazembe ambao haukuwa na malengo yeyote hivyo ni wakati mwalimu kukifanyika maboresho kikosi chake ili kipate matokeo mazuri,”anasema Mayai.

Anaongeza kwamba katika michezo miwili iliyopita Yanga ilikuwa na mapungufu makubwa eneo la kiungo na safu ya ushambuliaji.

“Thaban Kamusoko hana tatizo katika eneo hilo lakini amekosekana kiungo halisia wa kukaba anayeweza kuwalinda viungo wa katikati.

“Kosa hilo ndio chanzo cha washambuliaji kukosa mipira mbele na kufa kwa kiungo cha kati, kutokana na kushindwa kumiliki mpira hauwezi kuona  mbio za winga wala usanifu wa washambuliaji, ndio maana tulikuwa tuki mwona Donald Ngoma kama vile anacheza mbele ya mabeki wa TP Mazembe,”anasema Mayai.

Pia anaongezea kwamba makosa hayo  hayawezi kuonekana katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara bali  kwenye michezo mikubwa ya Kimataifa ambayo huwa na changamoto kubwa.

“Hii ndio michezo ambayo unaweza ukaona kikosi chako kina mapungufu sehemu gani na si kwenye michezo ya ligi  kwa kuwa si mikubwa kama hii,”anasema Mayai.

Kwa uapnde wake kocha wa timu ya vijana wa Yanga Shadrak Msajigwa, anasema katika mchezo huo ni jukumu la kila mchezaji kutambua  kazi yake ili kuisaidia timu kusonga mbele.

“Tunayo nafasi  labda Mo Bejaia na Medeama  wawafunge TP Mazembe lakini kama hilo halitawezekani bado tuna haki ya kujiuliza na kupata ushindi katika kila mchezo uliopo mbele yetu.

“Nafikiri mwalimu atakuwa amefanyia kazi makosa yaliyojitokeza kwani tunahitaji kucheza kwa kushambulia bila kuchoka ili tuweze kuwa na uhai katika kundi letu vingine hali itakuwa mbaya,”anasema Nsajigwa.

Naye Kocha Mkuu wa Stand United, Jamhuli Kiwelo, ‘Julio’ anasema kwamba kikubwa kinachoiangusha Yanga ni eneo la kati, kwa mchezaji anayecheza namba sita.

“Yanga inamtumia Kamusoko kucheza kama kiungo mkabaji lakini kiuhalisia si mchezaji wa aina hiyo bali ni kiungo mshambuliaji wa kweli.

“ Kutokana na makosa hayo licha ya kucheza kwa ustadi mzuri Yanga wanajikuta hawawezi  kukaba na kupokonya mipira na kama wangefanikiwa kuboresha eneo hilo  wasingefungwa katika mchezo wowote  wa kundi lao kwani ndio timu inayocheza vizuri hadi sasa,”anasema Julio.

Julio anaongeza kwamba  kwa sasa kama kusingekuwa na utani wa jadi mbele, Yanga ndio timu inayofanya vizuri katika Ligi Kuu Tanzania Bara  na Kombe la Shirikisho.

“Tukiachana na masuala ya utani wa Usimba na Uyanga, tukubali tukatae Yanga ipo vizuri, kinachowasumbua ni makosa madogomado ambayo kama mwalimu wao ameyaona ninaimani watashinda katika mchezo wao ujao hakuna tatizo,”anasema Julio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles