24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mzindakaya: Wizara ya Kilimo inaua nchi

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Chrisant Mzindakaya amesema tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, Wizara ya Kilimo imekuwa ikiliangusha Taifa.

Dk. Mzindakaya ambaye alipata kuwa mbunge wa muda mrefu aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 1965 akiwakilisha Jimbo la Kwela wakati huo, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mkutano kati ya Rais Magufuli na wafanyabiashara Ikulu jijini Dar es Salaam.

Alisema kilimo ni sayansi na si hotuba na kwamba taasisi zote za kilimo katika wizara hiyo zinakufa.

 “Kilimo ni sayansi sio hotuba tena kitaalamu, taasisi zote za kilimo katika wizara hii zinakufa na ushahidi ni Uyole-Mbeya ilikuwa inawika leo ni taabani sasa kilimo kitaendeleaje?.

“Huyu waziri wako wa  Kilimo aamke nipo tayari kumshauri na hawa vijana wako wakubali  wazee tuwape ushauri naweza kusaidia bado, wala siombi kazi kwa mtu mimi, nitasaidia maana ninapenda unavyoendesha nchi,”alisema Dk. Mzindakaya.

Kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimshauri Rais Magufuli kutoa nafasi kwa kila waziri kuchagua jambo moja litakaloliletea sifa Tanzania kwa sababu hawawezi kufanya kila kitu.

“Naamini kila mtu ana sehemu anayoiweza kwa asilimia 100 kuliko nyingine na akipewa ataifanya vizuri…kama tungetakiwa kuchagua mtu mmoja asiyefanya vitu nusunusu wewe Rais Magufuli ungepata kura nyingi za ujenzi na miundombinu kwa sababu ni kitu kilicho ndani ya damu yako hakuna anayebisha.

“Sasa tunataka na mawaziri hawa uliowapa wizara angalau kila mmoja achague kitu kimoja kwa sababu hawezi kufanya yote saba,”alisema Dk. Mzindakaya.

Dk. Mzindakaya aliyepata kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), alisema mkoa wa Rukwa unazalisha mahindi kwa wingi lakini ununuzi wa mazao hayo umekuwa na siasa huku akiiomba Serikali kuwa mstari wa mbele kununua badala ya kuwaachia wafanyabiashara peke yao.

“Serikali inapaswa kuchagua ni kazi gani inapaswa kufanywa na wageni pamoja na wenyeji kwa kuangalia ni nani mmiliki.

“Mabilionea hawawezi kupatikana bila mpango wa Serikali wenyewe, rasimu bado ni tatizo na hakuna maamuzi ya wakati yanayotolewa kwa wafanyabishara wanapotuma maombi yao au wanapojaribu kuwasiliana na ofisi za Serikali.”

“Wakati mwingine wamekuwa hawajibu barua wanazoandikiwa na wafanyabiashara na hata wanapopigiwa simu wanatuambia mzee leta nakala sasa ni mgeni gani kutoka nje atataka huo usumbufu,”alihoji Dk. Mzindakaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles