23.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 8, 2024

Contact us: [email protected]

MZEE MWINYI AZUNGUMZIA UTAWALA WA JPM

JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


 

mwinyiRAIS  Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi jana amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Dk John Magufuli, ikiwa ni mara ya kwanza tangu aingie madarakani.

Katika mazungumzo hayo, Mzee Mwinyi alisifu juhudi zinazofanywa na Rais Dk Magufuli hususani mapambano dhidi ya rushwa ambayo amesema yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Dar es Salaam jana, Gerson Msigwa, ilisema mbali na mazungumzo hayo,  Mzee Mwinyi alimpongeza  Rais Dk Magufuli kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Msigwa alisema Mzee Mwinyi aliyataja baadhi ya maeneo ambayo Rais  amepata mafanikio makubwa kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa na kwamba hatua zilizochukuliwa kwa mwaka huo mmoja zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo.

“Rushwa ilikuwepo tangu enzi ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere, hakuimaliza na sote tuliosalia hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta sunami, nafurahi sana, alisema Dk Mwinyi.

Aidha rais huyo mstaafu alizungumzia suala la kuimalisha utendaji kazi serikalini ambapo alisema hatua zilizochukuliwa zimeongeza  kasi zaidi huku akitoa wito kwa viongozi na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.

“Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumwombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambapo wanapotosha, tuseme sio hivyo, ilivyo ni kadhaa kadhaa kadhaa, tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri ya ajabu,” alisema Dk Mwinyi.

Wakati huo huo, Rais Dk Magufuli alifanya mazungumzo na  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Mendeleo ya Makazi, William Lukuvi. Hata hivyo Ikulu haikuweka wazi mazungumzo hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles