27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

DOSARI SIMU 2000 ZINAVYOHATARISHA USALAMA WA ABIRIA

kituo-cha-daladala-cha-simu-2000Na JONAS MUSHI-DAR ES SALAAM

IKIWA ni mwaka mmoja na miezi kadhaa tangu Kituo kipya cha daladala cha Simu 2000 maarufu Mawasiliano kianzishwe, kimejizolea sifa lukuki na pengine kupewa sifa ya kuwa kituo cha mfano nchini.

Sifa hizo zinatokana na ukweli kwamba wasimamizi wake wamekuwa wabunifu na wafuatiliaji wa karibu wa shughuli za kila siku katika kituo hicho kilichopo Sinza C Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya mambo ambayo yanakifanya kituo hicho kuwa cha mfano ni usafi wa mazingira yanayokizunguka ambapo kuna maua yaliyopandwa na kuchanua vizuri lakini pia kufagiliwa kila siku huku kukiwa na mapipa makubwa ya kuweka taka.

Kimekuwa pia kituo cha kwanza kuwa na huduma ya intaneti ya bure kwa njia ya Wifi, pamoja na spika za redio vyote hivyo ni kuhakikisha abiria hawi mpweke wakati wa kusubiri daladala.

Pia pembeni ya kituo hicho lipo soko zuri lenye bidhaa za aina mbalimbali ambapo abiria huweza kujipatia mahitaji yake kabla ya kupanda daladala.

Vipo pia vyoo vizuri na vikubwa ambavyo ni vya kulipia pamoja na kituo cha polisi kuhakikisha ulinzi na usalama wa abiria na mali zao wakati wowote kituoni hapo.

Pamoja na sifa hizo nzuri kumekuwa na malalamiko yanayotolewa na abiria wanaosubiri daladala kituoni hapo kuhusu changamoto ambazo zimeanza kujitokeza huku uongozi wa kituo ukionekana kutochukua hatua yeyote.

MTANZANIA lilifanya uchunguzi kituoni hapo na kubaini ukweli wa malalamiko yanayotolewa na abiria.

Kwanza ulinzi na usalama wa abiria na mali zao umekuwa mdogo kutokana na kuwa na giza nyakati wa usiku licha ya kuwapo kwa taa ambazo nyingi haziwaki tena kwa muda mrefu sasa.

Abiria wamelalamika kuwa hali hiyo imesababisha vibaka kuingia kituoni hapo na kuwaibia simu na fedha wakati wa kugombania magari.

“Kama unavyoona sasa ni usiku na taa haziwaki, kutokana na hili giza huwezi kumwona mtu vizuri hivyo kuna vibaka huwa wanavizia wakati wa kugombania magari waibe simu au pochi za abiria,” anasema abiria aliyekuwa akisubiri magari ya kwenda Mbagala aliyejitambulisha kama Omary Abdallah.

Anasema mwanzoni taa zote zilikuwa zinawaka na hakukuwa na matukio mengi ya wizi kama ilivyo sasa ambapo kwa kituo kizima taa zinazowaka hazizidi nne.

“Juzi wakati tukiwa kwenye gari tulipofika Ubungo mataa (makutano ya taa za barabarani) kuna mama mmoja alikuwa analalamika baada ya kugundua ameibiwa pochi yake iliyokuwa simu na fedha na wapo wengi waliofikwa na mikasa kama hiyo,” anasema Abdallah.

Mkazi wa Gongo la Mboto, Juliana Kisaka, anasema kutokana na kuwapo kwa giza kuna mateja (watu wanaotumia dawa za kulevya) ambao huingia kituoni hapo wengine wakijifanya wanaokota chupa za maji na wengine wanapiga debe lakini lengo lao ni kuibia watu.

“Tunaomba uongozi wa kituo hiki ulifanyie kazi suala la taa, wanafanya vizuri kwenye usafi wa mazingira pamoja na huduma kama kuweka redio na intaneti lakini taa zimekuwa changamoto kubwa,” anasema Juliana.

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu hali hiyo Meneja wa kituo hicho, Elichilia Khamis, anakiri taa kutowaka na kueleza kuwa imekuwa changamoto kutokana na kutumia umeme wa jua.

Hata hivyo anasema wameshalifanyia kazi suala hilo kwa kuwasiliana na Manispaa ya Ubungo pamoja na Kampuni ya MCL ambayo inahusika na uwekaji wa taa hizo ili kuja kuangalia tatizo lililopo.

“Hizi taa zinatumia umeme wa jua, kwahiyo inaonekana kuna hitilafu kwenye betri za kutunza umeme na tumeshaanza kulishughulikia suala hilo kwa kupeleka taarifa Halmashauri ya Manispaa Ubungo pamoja na kumfahamisha mhandisi ambaye ni kampuni MCL kuja kuangalia tatizo hilo,” anasema Khamis.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles