23.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

MAZOEZI KWA MATATIZO YA KIAFYA YATOKANAYO NA UMRI MKUBWA

Na Dk. Fredirick Mashili


akiendesha-baiskeliMAGONJWA na matatizo mengi kiafya hujitokeza zaidi pale umri unaposogea. Kuumwa mgongo, viungo na hata kushindwa kufanya au kufurahia tendo la ndoa ni miongoni mwa matatizo machache ambayo hujitokeza sana kadiri umri unavyoongezeka.

 

Mambo ya kuzingatia

 Unaweza kupunguza au kuzuia kabisa matatizo haya kwa mambo matano yafuatayo ambayo katika hali ya kawaida umuhimu wake husahaulika.

 

1. Kufanya mazoezi ya kunyanyua au kusukuma uzito

 Wengi wetu hupuuzia mazoezi ya aina hii kwa kusema ni kwa ajili ya watunisha misuli na wenye kutaka kuwa na misuli mikubwa. La hasha, mazoezi haya ni muhimu katika kuzuia kupotea kwa nguvu na kiasi cha misuli–vitu ambavyo hutokea kadiri umri unapokuwa ukiongezeka. Mazoezi haya pia husaidia kuzuia upungufu wa homoni ya kiume inayoitwa testosterone.

Kiwango cha homoni hii mwilini hupungua kadiri umri unavyoongezeka. Kupungua kwa kiwango cha homoni hii mwilini huchangia katika kusababisha tatizo la kupungukiwa kwa nguvu za kiume na kushindwa kufanya au kufurahia tendo la ndoa.

Hivyo ni muhimu kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ya kunyanyua au kusukuma uzito angalau mara mbili au tatu kwa wiki. Kumbuka kunyanyua au kusukuma uzito, haimaanishi kutumia uzito mkubwa utakaouzidi uwezo wako.

 

2. Kuendesha baiskeli

Kuendesha baiskeli hukupa fursa ya kufanya mazoezi ya aina tofauti kwa wakati mmoja. Tafiti zimeonyesha kwamba watu wanaondesha baiskeli mara kwa mara huishi miaka mingi zaidi ya wale wanaotumia magari na pikipiki, na pia viungo na miili yao huwa na nguvu na uwezo wa kufanya kazi zaidi

Hakikisha unaendesha baiskeli kila unapopata fursa. Kama unaishi karibu na barabara yenye sehemu maalumu iliyotengwa ya waendesha baiskeli, tumia fursa hiyo kuendesha baiskeli.

 

3. Fanya mazoezi ya kunyoosha na kulainisha viungo

 Kadiri umri unavyoongezeka misuli na viungo huzidi kukakamaa. Hii inaweza kusababisha matatizo ya kushindwa kutembea vizuri, kuanguka na hata kuumia mara kwa mara. Mazoezi ya kujinyoosha hupunguza au kuzuia kukakamaa kwa misuli na viungo–hivyo kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na tatizo hilo.

Hakikisha unafanya mazoezi ya kujinyoosha kabla au kila baada ya kufanya mazoezi. Kumbuka pia kujinyoosha mara kwa mara kama kazi yako inakufanya kuketi kwa muda mrefu.

 

4. Pata mapumziko ya kutosha

 Kama ufahamu kupumzika ni sehemu ya mazoezi pia. Kazi na mambo mengi kama sehemu ya maisha, hutufanya tukose muda wa kupumzika ipasavyo. Kukosa mapumziko ya kutosha huifanya miili yetu kuchoka na hivyo kupoteza nguvu haraka pale umri unaposogea. Kutokupata mapumziko ya kutosha pia husababisha kuongezeka kwa vichocheo vya magonjwa mwilini na hata kupunguza kinga za miili yetu. Mapumziko ya kutosha husaidia kuzuia kupanda kwa kiwango cha homoni ya stress mwilini, hivyo kukufanya mwenye nguvu na furaha.

Pumzika kwa kupata usingizi wa kutosha (kulala kusikopungua saa nane kwa siku), kushiriki katika michezo na kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki mara kwa mara.

 

5. Kutumia virutubisho – lishe

 Hili huyasaidia mazoezi kufanya kazi ipasavyo. Umri unapokwenda uwezo wa miili yetu kutumia chakula tunachokula ipasavyo hupungua. Lakini pia uhitaji wa kula lishe bora huongezeka. Virutubisho lishe husaidia kuupa mwili uwezo wa kutumia chakula tunachokula na hata kuupa mwili virutubisho muhimu.

Ongea na daktari wako au mtaalamu wa lishe kuhusu uhitaji wa virutubisho-lishe. Daktari ataangalia hali yako na kukushauri kama unahitaji na hata kukushauri aina ya virutubisho-lishe unavyohitaji.

 

Dk. Mashili ni Mtaalamu wa Fisiolojia ya Mazoezi na Homoni. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS).  0752255949,  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles