Mwitikio mdogo uandikishwaji daftari la wapiga kura unatoa taswira gani?

0
449

LEAH MUSHI

NOVEMBA 24, mwaka huu Watanzania nchi nzima watapiga kura kuwachagua viongozi wao katika ngazi ya Serikali za Mitaa.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo unaotoa taswira ya Uchaguzi Mkuu kwa maana kwamba wananchi wakijitokeza wachache basi uwezekano wa Uchaguzi Mkuu kuwa wa kusuasua ni mkubwa.

Lakini kwanini mwaka huu wananchi wamejitokeza wachache kujiandikisha katika daftari la wapigakura? Hii inatoa taswira gani?

Lakini kwanini pia kumekuwa na kampeni kubwa na imetumika nguvu kubwa zaidi kuhamasisha watu kujiandikisha kuliko wakati wowote?

Je, kwanini watu watu hawataki kujiandikisha? Wamechoka? Wameamua kususa? Kuna nini nyuma ya pazia?

Hayo na mengine mengi niliyoshuhudia wakati huu yamenifanya nikikumbuke kipindi change kilichokuwa kinaitwa ‘Kura Yangu’.

Mwaka 2014 hadi 2015, nilikuwa muandaaji na mtangazaji wa kipindi hicho cha Kura Yangu kilichokuwa kikiruka mara moja kwa wiki kupitia Televisheni ya Taifa (TBC1).

Lengo kuu la kipindi hicho, lilikuwa ni kutoa elimu ya uraia hususani umuhimu wa kupiga kura kwa wananchi, na nilipata fursa ya kuzunguka maeneo mbalimbali ya nchi kuzungumza na wananchi wa chini kabisa.

Ilinilazimu kuzunguka karibu nchi nzima kupata maoni ya wananchi na kutoa elimu kwao kuhusu uchaguzi na elimu ya kupiga kura.

Maeneo mengine kulikuwa hata hakuingiliki na gari na baadhi ya wilaya tulikuwa tunakosa hata sehemu ya kulala kwa kuwa kulikuwa na wageni wengi katika kila wilaya kwa ajili ya kuandikisha wananchi kwenye Daftari la Kielekroniki (BVR)

Muitikio wa wananchi ulikuwa mkubwa na kwenye maeneo mengine vijana walikuwa wanawachukua wazee kwenda kujiandikisha na tulipowahoji hao wazee wala hawakuwa wanaelewa BVR ni nini lakini walijiandikisha na foleni zilikuwa kubwa sana kila sehemu tuliyoenda.

Pamoja na majukumu yangu mengine kwa sasa lakini bado mimi ni mwanahabari na hili suala la muitikio mdogo wa wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari la kupiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa linanitafakarisha sana.

“Hivi nini kimetokea kiazi cha kuwafanya wananchi wale waliokuwa wanakaa msururu mrefu kujiandikisha wasijiandikishe tena sasa hivi?

Mimi ni mkazi wa jijini Dar es Salaam, na nilipokwenda kujiandikisha katika mtaa wangu watu nilimkuta mwandikishaji ‘anapiga story’ tu, kwa sababu watu hakuna, niliumia sana. Hivi kweli watu wamekata tamaa au wanaudharau huu uchaguzi?

Wazungu wanasema No research no right to speak (kama hujafanya utafiti basi huna mamlaka ya kulizungumzia hilo suala), lakini ebu tuzungumzeni kiuhalisia, nini kimetokea wananzengo wenzangu? Au mambo ni mengi muda mchache ndiyo maana hatujaenda kujiandikisha ama nini?

Watanganyika wenzangu ebu tulonge hili maana nionavyo mimi dalili ya mvua mawingu sasa kwa wingu hili lililotanda ikifika uchaguzi mkuu utakuwaje?

Tukifanya mchezo uchaguzi mkuu wananchi watakaoenda kujiandikisha na kupiga kura inaweza kuwa asilimia 20 ya wote wenye vigezo vya kupiga kura, sijui kama tunaelewana vizuri hapo.

Kama tulivyojaaliwa methali na misemo kutoka kwa wazee wetu basi jamani tuzibeni ufe tusije hangaika kujenga ukuta huko baada ya uchaguzi mkuu.

Ndiyo. Maana haya mambo ya mchelea mwana kulia mwisho wa siku tutalia wenyewe maana hadi sasa hatujui nani atamfunga paka kengele kila mtu anamlaumu mwingine kuhusu mwitikio mdogo wa wananchi kujiandikisha.

Leah Mushi ni mwanahabari na mkufunzi wa masuala ya dijitali.

Facebook: Leah Mushi

Instagram: leahmushi

Twitter: @leahbtz

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here