24.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

Mwenge watilia shaka ujenzi wa maabara ya Sekondari Anthony Mtaka

Na Derick Milton, Simiyu

Kiongozi wa mbio za Mwenge maalumu wa Uhuru 2021, Luten Josephine Mwambashi, ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya Busega mkoani Simiyu kufanya uchunguzi mara moja wa ujenzi wa jengo la maabara katika shule ya Sekondari Anthony Mtaka iliyoko katika Kijiji cha Lukungu wilayani humo.

Luten Mwambashi, ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Juni 28, 2021 mara baada ya mwenge huo kufika shuleni hapo kwa ajili ya uzinduzi wa maabara hiyo, ambapo kabla uzinduzi Kiongozi huyo aliomba kupatiwa nyaraka zilizotumika katika ujenzi wa mradi huo kwa ajili ya kuangalia matumizi ya fedha.

Hata hivyo nyaraka hizo zilikosekana baada ya uongozi wa shule hiyo kuzisaka bila mafanik licha ya kupewa muda wa masaa mawili huku mwenge ukiwa umesubilia shuleni hapo.

Mara baada ya kutumia muda huo wakisaka nyaraka hizo, kiongozi huyo alisema mwenge hautazindua jengo hilo kutokana kuomba wapatiwe nyaraka zilizotumika katika ujenzi licha ya kutumia masaa mawili lakini wahusika wameshindwa kuziwasilisha.

Luten Mwambashi amesema kuwa moja ya Nyaraka ambayo wameomba kupitiwa ni mchanganuo wa ununuzi wa vifaa vilivyotumika katika ujenzi huo, nyaraka nyingine ni mchanganuo wa gharama za wa ujenzi (BOQ) pamoja na nyaraka zinazoonyesha mapokezi ya vifaa vya kutumia kwenye maabara hiyo.

“Mradi huu umetumia gharama kidogo lakini tumeomba nyaraka hizo zimekosa, tumeomba ili tujiridhishe kama kuna matumizi sahihi pesa za umma, lakini zimekosekana, kwa msingi huo mwenge wa uhuru maalumu mwaka huu hautazindua jengo la maabara hii,” amesema Luten Mwambashi.

Kiongozi huyo ameitaka Takukuru kufanya uchunguzi wa haraka kwani wametilia shaka ujenzi huo, huku akitaka wahusika wote ambao watabainika wachukuliwe hatua kali za kisheria sambamba na kuagiza kuwa Mwenge huo upatiwe taarifa za awali za hatua zilizochukuliwa kabla ya kuondoka Mkoani humo.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo, Mkuu wa shule hiyo, Joseph Kazimoto amesema kuwa ujenzi wa maabara hiyo umekamilika kwa asilimia 100 ikiwemo ununuzi wa vifaa vyake ambapo ujenzi umegharimu kiasi cha Sh milioni 50 na vifaa vikigharimu Sh milioni 8.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Gabriel Zakaria amemwahidi Kiongozi huyo wa mwenge kutekelezwa kwa maagizo yake yote katika mradi huo, ikiwemo uchunguzi pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote ambao watabainika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,268FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles