Mwandishi wa habari Kabendera aeleza afya yake inavyozorota

0
2422

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imempa nafasi Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), kuelezea hali ya afya yake ambaye amedai tatizo la kushindwa kupumua usiku linaendelea, ana maumivu makali mguu wa kulia na mfupa wa paja la mguu huo unauma sana hadi anakosa usingizi.

Kabendera ambaye anaburuza mguu wa kulia wakati akitembea, alipanda kizimbani jana wakati kesi yake ilipokuwa inatajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile.

Akiiwakilisha Jamhuri, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai upelelezi haujakamilika baadhi ya maeneo, hivyo aliomba kuahirisha kesi hiyo.

Wakili wa utetezi, Jebra Kambole alidai mteja wake bado anaumwa, mguu wa kulia umepooza, usiku anashindwa kupumua, hivyo aliomba mahakama itoe maelekezo kwa Jeshi la Magereza wampeleke hospitali ya Serikali ili afanyiwe vipimo.

Akijibu, Wankyo alidai kuwa amefanya mawasiliano na Mkuu wa Gereza la Segerea na amemuhakikishia kwamba Kabendera anapata matibabu, hivyo kama kuna haja ya kumpeleka hospitali ya rufaa, watafanya hivyo kwa utaratibu wao na si mahakama kujieleza.

Alidai maombi ya wakili wa utetezi kutaka maeneo ambayo upelelezi haujakamilika yawekwe wazi, hilo haliwezekani kwani haitakuwa busara wakati wapelelezi wakiendelea na upelelezi wao wanaweka wazi hatua hizo mahakamani.

Akirudia kujibu, Kambole alidai kuna kupatiwa matibabu na matibabu sahihi na kwamba wiki ya pili hali ya mteja wake inazidi kutetereka.

“Mheshimiwa Hakimu, tunaomba mteja wetu apimwe ili sisi mawakili na ndugu tujue anaumwa kitu gani,” alidai Wakili Kambole.

Alidai mahakama ndiyo chombo cha utoaji haki, hakuna mahali kwingine ambako wanaweza kuomba hivyo.

Hakimu Rwizile alimwita Ofisa wa Magereza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Muhogo kuelezea Kabendera anapatiwa huduma gani gerezani.

Muhogo alidai gerezani kila siku madaktari wanawapitia wagonjwa kujua hali zao na kuwapa tiba, endapo hali ikizidi wanampeleka hospitali za rufaa.

KABENDERA AZUNGUMZIA AFYA YAKE

Hakimu alipompa nafasi Kabendera kuzungumzia afya yake, aliinuka alipokuwa amekaa kwa ruhusa ya mahakama na kujieleza.

“Gerezani hawana vifaa vizuri vya kupimia, walinipima damu kisha wakanichoma sindano tatu za kutuliza maumivu, nilikuwa nafanya mazoezi nikapata nafuu kidogo, lakini siku nane zilizopita nilianza kupata maumivu makali mguu wa kulia.

“Nina maumivu makali katika mfupa wa paja la kulia, maumivu yananifanya nikose usingizi, bado nashindwa kupumua ikifika usiku, jana (juzi) nilionana na daktari, mara ya mwisho nilimuona Alhamisi iliyopita, lakini akasema kulikuwa na ugeni.

“Daktari amesema atakuja kuniona anisikilize kesho (leo) Ijumaa,” alimaliza Kabendera.

Hakimu Rwizile baada ya kumsikiliza, aliamuru mshtakiwa huyo kurudishwa mahakamani Septemba 18 ambayo ni siku saba kuanzia jana ili atakapokuja aeleze kitu gani kinaendelea baada ya kukutana na daktari na kisha atatoa uamuzi.

Kesi iliahirishwa hadi Septemba 18 kwa kutajwa, Kabendera huku akiburuza mguu wa kulia alishuka taratibu kuelekea mahabusu.

HALI ILIVYOANZA KUTETEREKA

Awali Agosti 30, Wakili Kambole alianza kuifahamisha mahakama hali ya Kabendera ilivyoanza kutetereka.

“Agosti 21 mwaka huu mteja wetu aliumwa ghafla akiwa gerezani, mpaka leo anapata shida ya kupumua ukifika muda wa usiku.

“Agosti 21 hiyo hiyo mteja wetu alipooza miguu yote miwili akashindwa kutembea kwa siku mbili, akaishiwa nguvu, kama mawakili na ndugu zake hatujui anachoumwa.

“Tunaomba mahakama ilielekeze Jeshi la Magereza ili akapimwe sababu hajapata matibabu, tunaomba apelekwe Muhimbili sababu atapimwa, kuna vifaa vyote,” alidai.

MASHTAKA YANAYOMKABILI

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, shtaka la kwanza la Kabendera ni kwamba kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yeye na wengine ambao hawapo mahakamani, wanadaiwa walitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.

Inadaiwa shtaka la pili, kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, bila sababu za msingi Kabendera alikwepa kulipa kodi Sh 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la tatu la kutakatisha fedha, inadaiwa katika tarehe hizo mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here