29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 30, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanasiasa kuhojiwa mauaji ya mfanyabiashara Kenya

NAIROBI, KENYA

MWANASIASA, mtangazaji wa zamani wa redio, ambao majina yao yamehifadhiwa ni miongoni mwa watu, ambao polisi wanatarajia kuwahoji kuhusu mauaji ya mfanyabiashara Monica Nyawira Kimani.

Kimani (28) aliuawa katika nyumba yake usiku wa Septemba 19 na 20, na mwili wake ulikutwa ukiwa umekatwa shingoni, mdomo kuzibwa na miguu na mikono kufungwa ukiwa umeachwa sakafuni katika bafu linalotiririka maji.

Watu hao, kwa mujibu wa polisi, mshukiwa mkuu wa mauaji hayo, Joseph Irungu, aliwasiliana nao siku hiyo ya mauaji katika kile kilichoonekana kutafuta ushauri wa suala lililokuwa likimsumbua.

Uchunguzi wa kipolisi unaonesha Irungu alikuwa mtu wa mwisho kuondoka katika makazi, ambayo mwili wa Monica ulikutwa.

Irungu, rafiki yake wa kike, ambaye ni mtangazaji maarufu wa televisheni Jacque Maribe, na rafiki yao, Brian Kasaine, wanashikiliwa na polisi.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyo karibu na uchunguzi huo, mawasiliano ya simu ya mkononi yanaonesha saa chache baada ya Irungu kuondoka katika nyumba hiyo iliyopo Lamuria Gardens alipiga simu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa watu wanne.

Polisi walisema pia uchunguzi wao utawafikisha hadi Sudan Kusini, ambako Monica aliishi na kufanya kazi ili kunasa nyendo na shughuli zake.

Timu ya upelelezi ilisema inataka kufahamu nini alichobeba Monica wakati alipoondoka Juba kwenda Nairobi Septemba 19.

Pia wanataka kufahamu shughuli alizofanya kujiingizia kipato na nyingine zozote zile.

Hiyo ni sehemu ya juhudi zao kutafuta nadharia ya fedha kama sababu ya uwezekano uliosababisha kuuawa kwake.

Polisi wanaamini Monica aliuawa na kuporwa kiasi kisichojulikana cha fedha.

Kadhalika wanachunguza uwezekano wa Kimani kuhusiana na mwanasiasa mkubwa serikalini na jeshini nchini Sudan pamoja na uwezekano Kasaine alikuwa Juba.

Hilo linakuja huku matokeo ya sampuli ya vinasaba (DNA) iliyokusanywa kutoka nyumba ya Kimani yametoka.

Matokeo ya vipimo yamewasilishwa kwa maofisa wanaoshughulikia kesi hiyo katika Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) juzi.

Maelezo ya matokeo hayo ni siri kwa sababu ni sehemu ya ushahidi utakaowasilishwa mahakamani.

Hata hivyo, polisi walisema jana kwamba wamethibitisha pasipo shaka utambulisho wa muuaji.

Awali juzi wapelelezi pia waliwahoji mashuhuda zaidi ambao walikutana na mshukiwa mkuu katika nyumba ya Kimani kabla ya mauaji.

Watu hao mmoja ni raia wa Lebanon na mwingine Mkenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles