29.3 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

MWANAMKE WA KWANZA SUDAN KUFUNDISHA SOKA LA WANAUME

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO


SALMA al-Majidi ni moja kati ya majina makubwa nchini Sudan kwa sasa tangu mwaka 2015 baada ya mrembo huyo kutajwa na Shirika la Utangazaji nchini Uingereza BBC, kuwa mmoja kati ya wanawake 100 ambao wanaweza kushawishi.

Alizaliwa mwaka 1990, huku Omdurman mjini Sudan, akitokea kwenye moja ya familia ambayo inajali mila na tamaduni za nchini hiyo.

Kwa sasa msichana huyo ametajwa kuwa wa kwanza kutambulika na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), kwamba ni mwanamke wa kwanza nchini Sudan mwenye asili ya Kiarabu kufundisha soka kwa upande wa wanaume.

Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 28, anafundisha klabu ya Al-Ahly Al-Gadaref ya nchini humo ambayo inashiriki Ligi daraja la pili tangu mwaka jana baada ya kufanikiwa kutunukiwa leseni B ambayo inaweza kumfanya kocha huyo akafundisha timu yoyote ya Ligi Kuu barani Afrika.

Mbali na kufundisha soka, Salma alifanikiwa kuhitimu Shahada ya usimamizi wa fedha, lakini tangu amalize masomo yake hajaitumia elimu hiyo kwa kupata ajira.

Salma amesema alianza kupenda soka tangu akiwa na umri wa miaka 16, huku akiwa shule, alikuwa karibu na mwalimu wa michezo shuleni kwao, hivyo alitumia muda kumuuliza maswali mara kwa mara jinsi ya kufundisha soka.

Mwalimu hiyo aliweza kuyajibu kwa furaha na alimpa nafasi ya kuwa karibu hasa katika benchi lake la ufundi ili aweze kushirikiana.

Alisema baada ya kuona anaweza kutoa maelekezo ya soka kwa vijana aliamua kwenda shule kwa ajili ya kusomea jinsi ya kufundisha soka.

Hata hivyo inadaiwa kwamba haikuwa kazi rahisi kwa familia ya mrembo huyo kumpa ruhusa ya kwenda kusomea ukocha, lakini walikubali kwa shingo upande huku baadhi yao wakikataa kabisa kutokana na mila na tamaduni zao.

Mila zao zinasema mwanamke hawezi kumuongoza mwanaume, hivyo hawakuwa tayari kuona mtoto wao anakuja kuwaongoza wanaume.

“Kwa nini nimependa soka? Kwa sababu ni mchezo wangu wa kwanza kuupenda na utakuwa wa mwisho katika maisha yangu.

“Nimeamua kuwa kocha wa soka la wanaume kutokana na hakuna ushindani katika soka la wanawake nchini Sudan,” alisema Salma.

Inadaiwa kwamba nchini humo hakuna Ligi ya soka la wanawake kutokana na wanawake wengi kubanwa na sheria za dini ya Kiislamu, sio kama hakuna wanawake wanakatazwa, ila wamekuwa wakiingia sana kwenye dini na kuwafanya wasikubaliane na wanawake kucheza soka.

Wapo wanawake ambao wanacheza nchini humo lakini wengi wao hawataki kucheza soka mbele za watu.

Kocha huyo ambaye ni mmoja kati ya watoto wa polisi mstaafu nchini humo, aliongeza kwa kusema alianza kufundisha timu za vijana chini ya miaka 13 na 16 na baadae kuzifundisha timu kubwa za Ligi daraja la pili Al-Nasr, Al-Nahda, Nile Halfa na Al-Mourada kabla ya timu ya sasa.

Nile Halfa na Al-Nahda zilizidi kupata jina kubwa misimu miwili tofauti kutokana na uwepo wa kocha huyo ambapo ziliweza kumaliza nafasi ya kwanza kwenye msimao wa Ligi.

“Ilikuwa kazi kubwa kukubalika kwa klabu husika, hivyo kulikuwa na changamoto mbalimbali hasa kwa wachezaji wenyewe kuamini kama nitaweza kuwafundisha na wakafanya vizuri, lakini hadi sasa nashukuru kila kitu kipo sawa na wanafuata yale ninayowapa na timu zinafanya vizuri,” alisema.

Hata hivyo kocha huyo ameweka wazi kuwa ndoto yake ni kuhakikisha anafundisha soka timu kubwa ambazo zinajulikana duniani.

“Ushauri wangu kwa wanaume wote ni kwamba, wawape uhuru wanawake wa kufanya kile wanachotaka kukifanya,” aliongeza.

Mshambuliaji wa timu ya Al-Ahly Al-Gadaref, Majid Ahmed, amesema ilimchukua mwezi mmoja kumkubali kocha wake huyo baada ya kutajwa kuwa kocha wao mkuu, lakini sasa anajiona kuwa mshambuliaji bora tangu ujio wa kocha huyo.

“Kwa sasa naweza kusema nina uwezo mkubwa wa kushambulia tangu tuwe na kocha Salma, awali ilinichukua mwenzi mmoja kukubali mipango ya kocha huyo, lakini sasa sina la kusema.

“Siwezi kushangaa Salma kuwa kocha wetu kwa kuwa hata shule nyingi zina waalimu ambao ni wanawake na wanafundisha watoto wetu na wanafaulu,” alisema Ahmed.

@@@@@@@@@@@@

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles