24.8 C
Dar es Salaam
Friday, June 2, 2023

Contact us: [email protected]

NANI KUINGIA NUSU FAINALI UEFA WIKI HII?

Na BADI MCHOMOLO


MICHEZO ya marudiano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali inatarajiwa kupigwa wiki hii huku timu nne zikitarajia kuyaaga mashindano hayo na nne kuingia hatua ya nusu fainali.

Mtoto hatumwi duniani! Ndio tunaweza kusema hivyo kutokana na ushindani ambao utaonekana unaweza kuwa tofauti na ule wa wiki iliyopita.

SPOTIKIKI leo hii imekufanyia uchambuzi kuelekea michezo hiyo minne ya wiki hii ambayo itaanza kutimua vumbi kesho Jumanne.

Man City vs Liverpool

Hakuna ambaye alikuwa anadhani kama Liverpool wataweza kutumia vizuri uwanja wa nyumbani Anfield dhidi ya vinara hao wa Ligi Kuu nchini England, Man City.

Wapo mashabiki wa Liverpool ambao waliamini wanaweza kushinda au kutoka sare, lakini sio kwa ushindi mnono kiasi kile wa mabao 3-0, hasa kutokana na ubora wa wapinzani.

Hatimaye furaha ilikesha jiji la Liverpool, lakini kesho watakuwa kwenye uwanja wa Etihad kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

Bado Liverpool wana safari ndefu kuhakikisha wanaingia nusu fainali japokuwa wana idadi kubwa ya mabao ambayo yanawapa nafasi ya kusonga mbele.

Inawezekana Man City wakawa na mlima mrefu wa kupanda kuhakikisha inawaondoa wapinzani hao huku ikihitaji ushindi wa mabao 4-0 ili kuweza kusonga mbele au 3-0 ili kwenda kwenye matuta.

Hata hivyo katika historia ya kawaida Liverpool wamekuwa wababe kwa Man City katika kipindi chote walichokutana tangu 1901.

Timu hizo zimekutana mara 160, huku Liverpool wakifanikiwa kushinda mara 75, wakati huo Man City wakishinda mara 42 na kutoka sare mara 42.

Kocha wa Man City, Pep Guardiola anaogopeka na makocha mbalimbali nchini England, tayari ameweka wazi kuwa atahakikisha anaishangaza dunia kwa kuwaondoa wapinzani wake japokuwa wana idadi kubwa ya mabao.

Hakuna kinachoshindikana katika soka, hivyo kauli ya Guardiola inaweza kutimia au Liverpool wakaingia nusu fainali na kuweka historia ya muda mrefu.

AS Roma vs Barcelona  

Mchezo wa wiki iliyopita Barcelona waliweza kutumia vizuri uwanja wao wa nyumbani Camp Nou na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 4-1. Huo ni ushindi muhimu kwa timu hiyo.

AS Roma watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanawaondoka wapinzani hao, wanaweza kufanikiwa kushinda kwenye mchezo wa kesho lakini sio kufuzu hatua ya nusu fainali, lakini Barcelona wanapewa nafasi kubwa ya kushinda na kusonga mbele.

Hakuna dalili ya Barcelona kupoteza nafasi hiyo ya kuingia nusu fainali bila ya kujali mabao mawili waliyoshinda kati ya manne yalikuwa ya kujifunga kwa wachezaji wa timu pinzani.

AS Roma wanahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kuweza kusonga mbele, jambo ambalo ni wazi litakuwa ngumu japokua soka ni mchezo wa makosa.

Bayern vs Sevilla

Huu ni moja kati ya michezo miwili itakayopigwa kesho kutwa, tayari Bayern Munich waliweza kuutumia vizuri uwanja wa ugenini na kushinda mabao 2-1.

Wana faida kubwa ya bao la ugenini, hata hivyo kutokana na ubora wa wachezaji wa Bayern bado wana nafasi ya kushinda kwenye uwanja wa nyumbani.

Sevilla wanahitaji kushinda mabao 2-0 ili kuweza kusonga mbele jambo ambalo linaonekana kuwa ngumu kwa Sevilla.

Real Madrid vs Juventus

Tayari Real Madrid wanaamini wamemaliza kazi baada ya ushindi wa awali wa mabao 3-0 dhidi ya Juventus huku Madrid wakiwa ugenini.

Safari hii Juventus watashuka dimbani bila ya mshambuliaji wao hatari Paulo Dybala kutokana na kuwa na kadi nyekundu, wakati huo kwa upande wa Real Madrid watashindwa kumtumia nahodha wake Sergio Ramos kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.

Ni pengo kwa upande wa Juventus ambao wanahitaji ushindi wa mabao 4-0 ili kuweza kusonga mbele au ushindi wa mabao 3-0 ambao utawapeleka kwenye matuta.

Juventus watakuwa na wakati mgumu kuliko Madrid ambao kazi yao kubwa watahakikisha wanalinda lango lao na sio lazima washinde japokuwa mabao ni muhimu kwenye mchezo.

Kutokana na hali hiyo tunatarajia kuziona timu nne zikiyaaga mashindano hayo, wakati huo vidume wanne wakiendelea hatua ya nusu fainali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,264FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles