25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mwambe aitaka CRDB kuanzisha dirisha la viwanda kuchochea uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, ameishauri Benki ya CRDB kuanzisha dirisha maalumu la viwanda ili kuchochea kuimarika viwanda vidogo na vikubwa kwa kuwawezesha wawekezaji kupata mitaji ya uhakika.

Akizungumza wakati wa Semina ya Uwekezaji na Fedha iliyoandaliwa na Benki ya CRDB amesema benki hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia ajenda za maendeleo ya nchi.

Semina hiyo imefanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 3,000 wengi wao wakihudhuria kupitia mtandao.

“Kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hii, Abdulmajid Nsekela ndio Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) nimuombe ashawishi na mabenki mengine kutekeleza hili. Nitaandaa mkutano na umoja huu ili tuweze kulijadili kwa upana,” amesema Mwambe.

Amesema ili sekta binafsi iweze kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kunatakiwa kutengenezwa mazingira mazuri ya kuwawezesha watu na makampuni kupata fedha za kuwekeza.

Amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa urasimu na kupunguza utitiri wa kodi na tozo ili kupunguza gharama za uwekezaji nchini ikiwa.

“Mkurugenzi naomba nikuhakikishie mkiweza kuwawezesha wawekezaji kuwekeza katika viwanda faida ni kubwa mno katika uchumi wa taifa letu. Tutaweza kuimarisha uchumi kwa kiasi kikubwa, ajira zitakuwa za kutosha, mzunguuko wa fedha utaongezeka, na hata faida mtakayopata itakuwa zaidi ya hii shilingi bilioni 165 ambayo mmeipata mwaka jana,” amesema Mwambe.

Waziri huyo amesema mpango wa Serikali ni kuachana na kusafirisha malighafi nje ya nchi kwa kutengeneza bidhaa hapa nchini kupitia viwanda vya ndani na kuzitafutia soko nje ya nchi.

Aidha ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa semina hiyo na kuwataka Watanzania kuiunga mkono kwa kwa kupata huduma katika benki hiyo ili kuendelea kuiimarisha.

“Benki ya CRDB ukiwekeza huna wasiwasi nayo kwamba itakufa kesho kwa sababu maeneo yote iko vizuri, mikopo chechefu kushuka tafsiri yake ni kwamba watu wana imani kubwa na benki hii,” amesema Mwambe.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema malengo ya semina hiyo ni kuona Watanzania wengi zaidi wanashiriki katika fursa za uwekezaji hapa nchini pamoja na kupata uelewa wa huduma za benki hiyo zitakazowasaidia kuwa wawekezaji wazuri.

“Watanzania wengi wamekuwa nje ya mfumo rasmi wa kifedha kwa sababu hawana elimu ya kutosha hivyo kusababisha wengi kuogopa, lakini kupitia elimu hii tunaamini wengi sasa wataweza kujiunga na taasisi za kifedha lakini pia kichangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta hii pamoja na masoko ya mitaji,” amesema Nsekela.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dk. Ally Laay, amemuhakikishia Waziri Mwambe kuwa wataandaa sera itakayoelekeza na kusimamia uwezeshaji katika sekta ya viwanda na kwamba pendekezo la kuanzisha dirisha la viwanda wamelipokea kwa ajili ya utekelezaji.

Mada mbalimbali ziliwasilishwa katika semina zikiwemo Biashara ya Hisa Kidijitali, Uwekezaji wa Pamoja, Gawio kwa Wanahisa, Uwekezaji Endelevu wa Mali, Uwekezaji kupitia Huduma na Bidhaa za Benki na Bidhaa na Huduma za Benki ya CRDB Kufanikisha Uwekezaji.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki, Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye pia ni Mwanahisa wa Benki ya CRDB ameishukuru Bodi na Menejimenti kwa kuendelea kutekeleza programu za elimu ya uwekezaji na fedha na kuwakaribisha Watanzania wengine kuwekeza katika benki hiyo.

“Faida ya kuwekeza huku ni kubwa mno, niwakaribishe mjionee wenyewe,” amesema Sumaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles