Mwakyembe aagiza maafisa michezo kulinda viwanja

0
594
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na Maafisa Michezo wa Mikoa na Halmashauri za Tanzania Bara wakati akifungua kikao kazi cha maafisa hao cha siku mbili

Anitha Jonas – WHUSM, Dodoma

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amewataka Maafisa michezo kote nchini  kulinda viwanja vya michezo na kutoa taarifa ya viwanja vinavyobadilishwa matumizi kwa siri.

Waziri Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Desemba 12 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha maafisa michezo kinachofanyika kwa siku mbili chenye lengo la kutathimini, kujadili na kuelekezana namna bora ya kuimarisha michezo na kutumia sekta hiyo kutangaza vivutio vya utalii nchini.

“Wapo baadhi ya wakuu wa shule na walimu wanaozuia michezo shuleni na mnawajua, mnakaa kimya sasa wajibu wenu ni nini? tambueni michezo sasa ni ajira ambayo ni mgodi na taifa lina vijana wengi simamieni vyema michezo,” amesema Mwakyembe.

Akiendelea kuzungumza katika ufunguzi wa kikao kazi hicho Dkt. Mwakyembe amekiagiza Chuo cha Michezo cha Malya kufanya utafiti wa kodi inayotokana na michezo mbalimbali inayofanyika nchini.

Naye Kaimu Katibu Mkuu, Dk. Ally Possi amemwagiza Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo kuhakikisha kikao kazi hicho kinakuwa endelevu na kufanyika kila mwaka. Aidha amemtaka aandae utaratibu wa kuwa na vikao hivyo kikanda vikiwa na lengo la kuwaandaa vijana waweze kushiriki michezo mbalimbali kitaifa na kimataifa.

“Kikao Kazi hiki kitatoa tathimini ya wapi tulipo, nini kifanyike pamoja na kutoa mwongozo wa kusimamia michezo mbalimbali na kutoa maelekezo kwa kuweka maazimio yatakayosaidia kupeleka michezo kuwanufaisha vijana maana michezo ni ajira,” amesema Dk. Possi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here