Mambo yameiva bandari za Bukoba na Kemondo Bay sasa kuhudumia meli kubwa

0
1246
Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria, Morris Mchindiuza akikagua miundombinu katika daraja la kuunganisha reli na meli katika Bandari ya Kemondo Bay

MWANDISH WETU-BUKOBA

UFUFUAJI wa bandari katika Ziwa Victoria sasa umeshika kasi ambapo sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imekamilisha maboresho ya bandari za Kemondo Bay na Bukoba ambazo kwa sasa zipo tayari kuanza kuhudumia meli kubwa za shehena za mizigo na abiria.

Kutokana na hali hiyo TPA imesema kuwa hatua ya kusuasua kwa bandari hizo kwa miaka 15 iliyopita ikiwamo kusimama kwa huduma kulichangia kwa kasi kubwa kuibuka kwa bandari bubu katika eneo hilo.

Akizungumza leo mjini Bukoba, Meneja wa Bandari za wa Ziwa Victoria, Morris Mchindiuza, amesema kuwa kwa sasa wamejipanga kuanza kuhudumia shehena za mizigo na abiria katika maeneo hayo jambo ambalo litachochea kukua kwa uchumi na ukusanyaji mapato ya Serikali.

“Tupo katika Bandari ya Kemondo Bay na Bukoba, mkoani Kagera, kwa hii bandari ya Kemondo ilijengwa kuanzia mwaka 1971 na kukamilika mwaka 1974.

“Lengo kuu la bandari hii kwa wakati huo lilikuwa zaidi kusafirisha shehena za mizigo mbalimbali na hasa zao kuu lilikuwa kahawa lakini pia ilikuwa inahudumia abiria kilikuwa kituo kikubwa cha kuibeba mizigo ikiwamo mihogo na ndizi na maparachichi ambayo yalikuwa yakisafirishwa kwa wingi kutoka katika eneo hili.

“Lakini pia mizigo yote iliyokuwa ikitolewa mkoani Mwanza kama vifaa vya ujenzi ikiwamo saruji pamoja na nondo ilikuwa ikifikishwa hapa na baadaye kutawanywa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Kagera pamoja na vitongoji vyake.

“Kwa takribani miaka 15 iliyopita hapa katika Bandari ya Kemondo Bay ilikuwa inakwenda kwa kusimama na kusuasua na baadaye kabisa tukajikuta hatuna oparesheni zozote zinazofanyika kwenye hili eneo kubwa la Bandari Kuu ya Kemondo Bay,” alisema Mchindiuza

Amesema baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kuona kwamba hali hiyo inaendelea wakaanza kuwekeza na kuhuisha miundombinu iliyopo hivyo kwa kuanza kufanya ukarabati kwenye jengo la abiria lakini pia tukaja kwenye hili eneo la daraja la reli ambalo huunganisha mabehewa ya mizigo na meli.

“Reli zilizopo hapa kama mnazoziona zilikuwa zimefukiwa kabisa kwa hiyo kulikuwa hakuna uwezekano wa kuingiza behewa zikawesha kufanya kazi.

“Tukasema tuwekeze fedha hapa kiasi cha cha zaidi ya milioni 815 kwa ajili ya kufanya kazi hiyo na kazi hii tumeianza wiki tatu zilizopita na sasa tupo mwisho kabisa kuikamilisha ili kazi zianze za kuingiza mizigo katika bandari hii,” alisema

Meneja huyo wa Bandari za Ziwa Victoria, alisema TPA ina imani kwamba bandari hiyo itakuwa ni kichocheo cha ajira katika eneo letu hili lakini pia kumuwezesha mwananchi wa kipato cha chini mkulima Mtanzania ambaye yeye analima ndizi na maparachichi.

Bandari ya Bukoba

Akizungumza Bandari ya Bukoba amesema ni kati ya bandari sita kubwa ambazo zipo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania, katika eneo hili la Ziwa Victoria.

Amesema bandari hiyo ilijengwa toka wakati wa ulokoni mnamo mwaka 1945, baada ya Uhuru bandari hii ikawa chini ya Shirika la Reli pamoja na lile ya Bandari la Afrika Mashariki mpaka kufikia mwaka 1977 baada ya juiya hiyo kuvunjika na kurudishwa tena chini ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

“Na ilipo fika mwaka 1997 ikawa chini ya Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania kwa maana MSCL ambao wao nao wakaendelea kuhudumia bandari hii mpaka kufikia mwaka 2004 baada ya kuundwa kwa sheria ya TPA kwa Sheria namba 17 ndipo bandari hii chini ya Usimamizi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania.

“Na katika maboresho haya tumetumia gharama ya Shilingi milioni 565 kwa kazi hii ya kuhuisha jengo zima la abiria pamoja na jengo la utawala kwa hiyo kwa sasa hivi kila kitu kimekamilika kwa upande wa huu na tunaendelea pia na ukarabati wa majengo ya kuhifadhia mizigo ambao nao huu upo katika mradi mwingine wa uboreshaji a miundombinu ya Bandari kwa eneo la Bukoba, Kemondo, Mwanza Kaskazini na Kusini,” alisema

Amesema bandari hiyo ni chachu ya wafanyabiashara wa mkoa wa Kagera hususan Bukoba mjini ambapo wafanyabishara wadogo wadogo na wakulima wamekuwa wakisafirisha mazao ya kilimo ama ndizi, maparachichi na kuyapeleka kwenye soko mkoani Mwanza.

“Lakini tulikuwa na meli miaka ya nyuma za MSCL ambazo zilifanyakazi ikiwamo meli ya Mv Bukoba ilianza hapa hadi Mwanza, Meli ya Mv Victoria nayo ilikuwa ikija hapa na Mv Serengeti na kuanzia Machi mwakani safari zitaanza tena kwa kasi,” alisema

Amesema kwa sasa bandari ya Bukoba imekuwa ikiendelea kutoa huduma hususan kwa wateja wakubwa wawili ambao ni Kiwanda cha Sukari Kagera ambaye amekuwa akitumiia usafiri wa meli na kupeleka sukari jijini Mwanza pamoja na Kampuni ya Omukwano ya Uganda ambayo huleta bidhaa za mafuta, sabuni na kuziingiza nchini kupitia Bandari ya Bukoba na kasha kusambazwa katika maeneo mengine ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here