24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Muhimbili kuweka masharti magumu

kigwangwallaNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

SERIKALI itaanza kuweka masharti magumu ya rufaa za wagonjwa kabla ya kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kupatiwa matibabu zaidi dhidi ya magonjwa yanayowasumbua.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangwala, alisema hayo Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya pili ya tathmini ya utoaji wa huduma za afya nchini.

Dk. Kigwangwala alisema hatua hiyo imelenga kupunguza msongamano wa wagonjwa wanaohamishiwa katika hospitali hiyo kubwa kutoka hospitali na vituo vingine vya afya.

“Hospitali ya Muhimbili inapaswa kuwa na vitanda vya kulaza wagonjwa kati ya 800 na 1,000, sasa vipo zaidi 1,500. Tumebaini kwamba wagonjwa wengi wanaohamishiwa Muhimbili matibabu yao yangeweza kumalizika katika hospitali zetu za ngazi ya chini.

“Lakini madaktari wamekuwa wakiwapa rufaa za kwenda Muhimbili bila sababu za msingi na wakati mwingine kwa sababu mgonjwa mwenyewe anaamini kuna madaktari wazuri watakaomtibu kwa kuwa anaona hata viongozi wamekuwa wakitibiwa Muhimbili,” alisema Dk. Kigwangwala.

Alisema madaktari wamekuwa wakiwaandikia rufaa hizo wagonjwa bila kuelekeza wanakwenda kuonana na daktari wa aina gani na kutibiwa ugonjwa gani.

“Mgonjwa akifika Muhimbili anaanza upya mchakato wa kupimwa ili kujua tatizo linalomsumbua, mwisho wa siku idadi imekuwa kubwa wakisubiri vipimo wodini,” alisema Dk. Kigwangwala.

Alisema pamoja na masharti hayo, Serikali itaboresha huduma za afya katika hospitali za ngazi ya wilaya na kuzipandisha hadhi kuwa za rufaa.

“Kwa mfano Dar es Salaam tutaboresha Mwananyamala, Temeke na Amana kwa kuziongezea nafasi za kulaza wagonjwa na kuwapatia madaktari bingwa ili kuipunguzia mzigo Muhimbili,” alisema Dk. Kigwangwala.

Akizungumzia tathmini hiyo, Dk. Kigwangwala alisema matokeo yake yataisaidia Serikali katika kufikia lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

“Utafiti wa awali wa mwaka 2006 unaonyesha tulikuwa na vituo vya afya 5,669, vimeongezeka hadi 7,021 ingawa kuna changamoto mbalimbali, huku asilimia 87 vinatoa huduma ya kujifungua, hali ambayo inatupa picha halisi nini tufanye ili kuboresha huduma,” alisema Dk. Kigwangwala.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk. Albina Chuwa, alisema matokeo ya utafiti huo yatasambazwa kwa wadau wote nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles