23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, June 16, 2024

Contact us: [email protected]

CAG Assad awavutia pumzi maofisa wake

cag-mussaNa Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam

WAKAGUZI 10 wanaotuhumiwa kuchukua rushwa katika halmashauri nne nchini, bado wanaendelea na majukumu kwenye vituo vyao vya kazi.

Halmashauri hizo ni Mbogwe (Geita), Nanyumhu (Mtwara), Kilolo (Iringa) na Misenyi (Kagera).

Wakaguzi hao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa katika halmashauri hizo ili kuziandikia hati safi baada ya ukaguzi wakati kuna madudu.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad, alisema kuwa ofisi yake imeshindwa kuwachukulia hatua za kisheria wakaguzi hao kutokana na kutopewa barua rasmi zinazohusu tuhuma zinazowakabili.

Alisema hadi sasa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, hajampa taarifa zozote kuhusu tuhuma hizo, jambo ambalo limemfanya kushindwa kutoa uamuzi wowote kwa watuhumiwa hao.

“Nimeshindwa kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi kutokana na tuhuma zinazowakabili kwa kuwa Tamisemi hadi sasa hawajaniandikia barua kunitaarifu juu ya tuhuma zinazowakabili,” alisema Profesa Assad.

Alisema hadi sasa wakaguzi hao bado wanaendelea na majukumu yao kwenye vituo vyao vya kazi, huku wakidaiwa kuchukua rushwa.

Profesa Assad alisema kama Tamisemi itawaandikia barua ya kuwataarifu kuhusu suala hilo, wakaguzi hao watasimamishwa kazi mara moja ili kupisha uchunguzi.

“Hatuwezi kuwavumilia wakaguzi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, tutachukua hatua zinazostahili,” alisema.

Aliongeza kuwa ikiwa watabainika kufanya hivyo, watafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Alisema hawezi kuwaacha wakaguzi wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali waendelee na kazi huku wakijua kuwa wanachokifanya hivyo ni kosa kisheria.

Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, mkaguzi yeyote atakayebainika anakwenda kinyume na maadili ya kazi yake, atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.

“Hatuwezi kuwavumilia wakaguzi wanaoshindwa kutimiza majukumu yao na kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa, tutawachukulia hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Profesa Assad.

Aliwataka wakaguzi wote nchini kufanya kazi zao kwa weledi na uadilifu na kuacha tabia ya kujiingiza kwenye masuala ya rushwa ambayo yanachangia kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Wiki iliyopita, Simbachawene aliwataja wakaguzi 10 kuhusika katika kashfa ya uchukuaji wa rushwa katika halmashauri hizo, jambo ambalo lilisababisha wakurugenzi wake kusimamishwa kazi kwa ajili ya uchunguzi.

Wakurugenzi waliosimamishwa kazi ni pamoja na Elizabeth Kitundu (Misenyi), Ally Kasenge (Nanyumbu), Abdallah Mfaume (Mbogwe) na Halima Mtupa (Tunduma).

Wakaguzi wanaodaiwa kuchukua rushwa kwenye halmashauri hizo ni pamoja na Stephen Uwawa, John Elias, Kilembi Nkole ambao wanadaiwa kuchukua rushwa ya Sh milioni 3 katika Halmashauri ya Misenyi ili kuwaandikia hati safi wakati kuna madudu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles