24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 4, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto wa mwandishi wa habari atoweka mazingira ya kutatanisha

Na MWANDISHI WETU – Dar es Salaam


MTOTO wa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Global Publishers Ltd, Elvan Stambuli aitwae Christopher Stambuli (24) anadaiwa kutoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kwenda kazini na kushindwa kurejea nyumbani.

Taarifa za kutoweka/kupotea kwa kijana Christopher ambaye anadaiwa kuwahi kufanya kazi katika Kampuni ya CZI inayomiliki magazeti likiwamo Tanzanite na Tanzanite Online Televisheni, zilianza kusambaa juzi mitandaoni.

Tangazo la kutoweka kwake lililoambatanishwa na picha yake lilieleza kuwa anatafutwa na wazazi wake kwani hakuwa ameonekana nyumbani tangu Septemba 23, mwaka huu.

Tukio hilo limekuja katika wiki ambayo kumekuwa na taarifa nyingi za watoto wadogo kupotea.

Hata hivyo tukio la Christopher kutoweka kulingana na umri wake linaonekana kutofautiana na matukio ya kutoweka au kupotea watoto ambayo yameonekana kuibuka kwa kasi katika kipindi hiki.

Taarifa ya tangazo hilo iliyochapwa gazetini, iliambatanishwa na mawasiliano ya baba mzazi wa Christopher pamoja na RB na. KJN/RB/26112/2018.

MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo, alithibitisha kuwapo kwa taarifa za kutoweka kwa kijana huyo ambazo alisema jeshi lake linazichunguza.

Kamanda Muliro alisema hawezi kuzungumza zaidi juu ya tukio hilo kwani atavuruga upelelezi.

“Tumezisikia hizo taarifa, tunachunguza kuona kama ni kweli,” alisema Kamanda Murilo kwa kifupi.

Baba mzazi wa Christopher, Stambuli ambaye pia ni Mhariri wa Gazeti la Uwazi, alipotafutwa na gazeti hili alikiri kutoweka kwa kijana wake huyo huku akikataa kulizungumzia kwa upana kwa kile alichosema ameshauriwa na viongozi wa juu wa polisi kutolizungumzia kwani liko kwenye vyombo vya kipelelezi.

“Lakini hilo suala liko kwenye upelelezi wa polisi hivyo linafanyiwa kazi,” alisema Stambuli.

Akimwelezea kijana wake, Stambuli alisema alikuwa bado akiishi naye nyumbani kwake Mwenge Mlalakuwa, hivyo alibaini mapema kupotea kwake.

Wakati Stambuli akikataa kuzungumza kwa kirefu kwa sababu ya ushauri aliopewa na vyombo vya dola, MTANZANIA Jumapili limedokezwa na wanafamilia hiyo kuwa Christopher kabla ya kutoweka alikuwa akifanya kazi Kampuni ya CZI kama mtaalamu wa teknolojia ya mawasiliano (IT).

MTANZANIA Jumapili lilielezwa kazi hiyo aliipata miezi mitatu iliyopita baada ya baba yake kumwombea kwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Cyprian Musiba.

Siku moja au mbili baada ya Christopher kutoweka, inaelezwa Stambuli aliwasiliana na Musiba ambaye alimwambia kuwa kijana huyo aliyehitimu IT katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam miaka miwili iliyopita, aliacha kazi kwake siku nyingi.

Taarifa za Christopher kuacha kazi katika kampuni hiyo zinadaiwa kumshtua baba yake ambaye inaelezwa hakuwa akifahamu lolote kwani mwanawe huyo alikuwa akimwaga kila siku kwenda katika kibarua chake hicho.

Wakati familia ikitoa maelezo hayo, taarifa ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii na ambazo Jeshi la Polisi limekataa kuzizungumzia kwa kile ilichoeleza kukwepa kuharibu uchunguzi, zinaeleza kijana huyo alitoweka baada tu ya kuwasiliana na mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo ambaye hata hivyo hakutajwa jina katika eneo la Africasana, Sinza, Dar es Saalam.

MTANZANIA Jumapili liliwasiliana na Mkurugenzi wa Kampuni ya CZI, Musiba ambaye alikiri kusikia taarifa za kutoweka kwa kijana huyo.

Pia alikiri kijana huyo kuwahi kufanya kazi kwenye kampuni hiyo, lakini aliacha kazi siku na muda ambao hakumbuki.

Musiba ambaye alisema huwa hafuatilii maisha ya wafanyakazi wake zaidi ya kujua kulipa mshahara kwa wakati, alisisitiza taarifa za kijana huyo kuacha kazi alizipata akiwa jijini Dodoma ambako anaishi kwa sasa.

“Aliacha kazi nikiwa Dodoma ninakoishi, hata sasa nipo huku, nilipokuja huko nikakuta ameacha kazi. Nikamwomba kwa kumtumia ujumbe mfupi arudi kazini, lakini ikashindikana. Sikumbuki ni lini aliacha,” alisisitiza Musiba.

Alisema kitendo cha kijana huyo ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni yake upande wa televisheni kuacha kazi kilimshangaza baba yake ambaye ndiye alimwombea kazi katika kampuni hiyo.

“Alivyoacha kazi baba yake alishangaa kwani alimwombea kwangu. Nilipigiwa simu pia na Shigongo (Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers Ltd, Eric Shigongo) nikamweleza kama nilivyokueleza. Mimi huwa siwafuatilii wafanyakazi,” alisema Musiba.

Musiba alisema kitendo cha kijana huyo kuacha kazi kilimsikitisha kwani alifanya uamuzi pasipo kumtaarifu.

“Nilisikitika aliacha kazi bila kunitaarifu labda alipata sehemu ya fedha nyingi akaona 400,000 ni ndogo. Hata barua ya kuacha hakumkabidhi mtu, alitupa chini, walikuja kuokota wafanyakazi wenzake na kukuta kumbe ni yake,” alisema Musiba.

Alisema kabla ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, Christopher alikuwa akifanya kazi katika Kampuni ya Global Publishers Ltd.

Alipoulizwa kijana huyo ni wa umri upi, Musiba alisema ni mtu mzima kwa kuwa tayari alikuwa na mwanamke na mtoto.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Musiba inapingana na ile aliyoitoa baba yake ambaye alisema kuwa Christopher alikuwa akiishi naye nyumbani kwake, hajaoa wala hana mtoto.

Pia Musiba anapingana na taarifa zinazomkariri baba wa Christopher kwamba alipata habari za mwanawe kuacha kazi siku moja au mbili baada ya kupotea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles