23.4 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mtoto wa Mkuu wa Majeshi afariki dunia kwa ajali ya ndege

ANDREW MSECHU –dar es salaam

MTOTO wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, amefariki dunia baada ya ndege aliyokuwa akirusha kupata ajali Uwanja wa Soronera jana asubuhi.

Nelson Mabeyo ambaye alikuwa rubani wa ndege za Kampuni ya Euric Air, alifikwa na mauti baada ya ndege kupata itilafu na kuanguka muda mfupi baada ya kuruka kwenye uwanja huo ambao uko ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Kamishna Msaidizi wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete, alithibitisha kutokea ajali hiyo na kusema watu wawili walipoteza maisha.

Shelutete alisema japokuwa sababu za kiufundi zilizosababisha ndege kupata ajali hazijajulikana, wanasubiri mamlaka husika kufanya uchunguzi.

Alisema ndege hiyo ilianguka baada ya kushindwa kushika kasi wakati ilipokuwa ikijaribu kuruka.

“Ni kweli ndege ya Kampuni ya Auric Air imeanguka alfajiri ya leo (jana) na kusababisha vifo vya watu wawili, akiwemo Nelson ambaye ni mtoto wa Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo.

“Ndege hii iliangukia baadhi ya majengo yaliyopo uwanjani, sasa mamlaka zinazohusika ndizo zinazosubiriwa kutoa taarifa kuhusu chanzo cha ajali, Tanapa tunahusika kutoa taarifa kuhusu ajali tu,” alisema Shelutete.

Juhudi za kuupata uongozi wa Kampuni Auric Air ili  kuzungumzia ajali hiyo hazikuzaa matunda.

Lakini taarifa zilizo kwenye mtandao wa kampuni hiyo, zina ujumbe unaolezea masikitiko ya ajali hiyo.

Taarifa hiyo ilithibitisha ndege iliyopata ajali ni yenye namba 5H-AAM.

“Hadi sasa tunachojua ndege hii iliondoka asubuhi  Uwanja wa Soronera kwenda Grumeti ikiwa na rubani mmoja na msaidizi wake, lakini ilipata ajali muda mfupi baada ya kuanza kupaa, hakuna aliyenusurika.

“Mamlaka zote zinazohusika zimeshapewa taarifa na wanaohusika tayari wameshapelekwa eneo la tukio kwa ajili ya hatua zaidi, tutaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu ajali hiyo baadaye kwa kadiri tutakavyopata mrejesho,” ilieleza taarifa hiyo.

Ilieleza kuwa ndege hiyo ilikuwa ikielekea Hoteli ya Grumeti kuchukua watalii.

Mmoja wa maofisa wa kampuni hiyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema viongozi hawawezi kuzungumzia ajali hiyo kwa sasa hadi mamlaka zinazohusika zitakapokamilisha uchunguzi wake.

Gazeti hili lilifika nyumbani kwa Jenerali Mabeyo karibu na Msasani Beach Club, Kawe na kukuta taratibu za mazishi zikiendelea.

Mmoja wa maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aliyekuwapo nyumbani hapo ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema taratibu za msiba zinaendelea na wanafamilia wanaendelea kukusanyika kwa taratibu za mazishi.

“Ni kweli kijana wetu Nelson amefariki, kama unavyoona, hapa ndiyo kwanza taarifa zimefika na maandalizi ndiyo yanaanza, kwa hiyo hata familia nzima bado iko kwenye mshtuko,” alisema.

Alisema tararibu za maziko zitatangazwa baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles