23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Mtoto wa Masaburi ashinda unaibu meya Ilala

Nora Damian -Dar es salaam

DIWANI wa Kata ya Chanika, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Ojambi Masaburi (CCM), amechaguliwa kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Ilala baada ya kupata kura 33 dhidi ya mpinzani wake Diwani wa Viti Maalumu Chadema, Hellen Lyatura aliyepata kura 21.

Nafasi hiyo ilikuwa wazi baada aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Omar Kumbilamoto kuchaguliwa kuwa meya wa manispaa hiyo mwezi uliopita.

Kumbilamoto alichukua nafasi ya Charles Kuyeko aliyekuwa Diwani wa Kata ya Bonyokwa (Chadema) ambaye alijiuzulu Machi 23, mwaka huu na kujiunga na CCM.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi, Ofisa Tawala Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Jabir Makame, alisema kura zilizopigwa ni 54 na Masaburi alipata 33 wakati Lyatura alipata 21.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Masaburi aliwashukuru viongozi wa CCM na madiwani kwa kuona kuwa anafaa kuwa msaidizi wa meya na kuahidi kushirikiana nao.

“Mmenipa imani kubwa na mimi sitawaangusha, nawaahidi ushirikiano na tutahakikisha ilani ya chama inaendelea kutekelezwa kwa vitendo,” alisema Masaburi.

Naye Lyatura alisema ameridhika na matokeo hayo kwani uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na kwamba walijipanga vizuri kulinda kura.

“Kwenye uchaguzi kushinda na kushindwa ni jambo la kawaida, mimi nimeridhika na matokeo kwa sababu tulizilinda kura zetu mwanzo hadi mwisho.

“Matokeo haya hayatuvunji moyo, tunaendelea na mapambano kuhakikisha tunajipanga vizuri na kupata ushindi katika chaguzi zingine ukiwemo wa Serikali za Mitaa,” alisema Lyatura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles