28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, October 2, 2022

MTOTO HAPASWI KUCHAPWA, ANASIKILIZWA NA KUELEKEZWA – DORCAS

Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro


WAPO wazazi ambao hawazifahamu tabia za watoto wao, hii inatokana na aidha kutokuwa nao karibu na kushindwa kufuatia mienendo yao.

Hali hii pia uhusiano baina ya mama na mzazi kuwa mbaya na hivyo mtoto kufanya kila jambo bila kumshirikisha, matokeo yake kuwa na tabia zisizofaa. Ili mtoto awe na tabia njema, ni muhimu awe na uhusiano wa karibu na mzazi, pia ajenge tabia ya kumsikiliza hata kama anazungumza mambo ya kitoto.

Dorcas Aid Tanzania, kwa kutambua udhaifu wa baadhi ya wazazi, imeamua kuwapa mafunzo wazazi na walezi wa watoto wanaofadhiliwa na shirika hilo ili kuwakumbusha wajibu wao.

Jane Jackson ni miongoni mwa wazazi walioshiriki katika mafunzo hayo yaliyohusu mbinu za kulea na mabadiliko ya ukuaji wa mtoto, anasema mafunzo waliyopatiwa yatawajengea uwezo wa kulea.

“Baada ya mafunzo nimejifunza kuwa tabia ya mtoto inategemea na umri wake, mwonekano na maumbile.

“Awali sikuwa nafahamu kwamba kuna tabia za watoto ambazo tunapaswa kuzivumilia, tusiwe wakali kila wakati pindi wanapokosea. Sisi pia huwa tunawakosea na tunapaswa kuwaomba msamaha,” anasema.

Mwezeshaji kutoka Smart Community on Legal Protection Organization, anasema wazazi hawapaswi kukariri namna ya kuwalea watoto, wanapaswa kujenga tabia ya kuwasikiliza, kuwapa nafasi ya kuzungumza pindi wanapohitaji kufanya hivyo, hii itawawezesha kujua kila linalowasibu wanapokuwa mbali na nyumbani.

Naye Katibu wa mradi wa watoto  unaofadhiliwa na Doricas Aid International Tanzania, Vicent Steven, anasema mafunzo waliyopatiwa yamewafungua akili na kubaini kuwa walikuwa wanafanya makosa katika kuwalea watoto.

“Nimegundua kuwa nimewakosea watoto wangu mara nyingi, sikuwapa nafasi ya kuwasikiliza hata baada ya kufanya kosa, badala yake niliwachapa bila ya kuwasikiliza.

“Najisikia vibaya, nitakwenda kuwa balozi mzuri katika jamii ili waepuka kuwaadhibu watoto bila mpangilio,” anasema Steven.

Anasema mtoto anatakiwa kuwa na muda maalumu wa wa kucheza na kufanya kazi za shule. Hii itamsaidia kujali muda hata atakapokuwa mtu mzima.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Dorcas, Lilian Michael, anasema watoto wanapaswa kulelewa vema ili waweze kujisimamia wenyewe.

Anasema shirika hilo lina mradi wa kusaidia watoto mahitaji ya msingi na kwamba kwamba wanawakumbusha wazazi na walezi wajibu wao kwa watoto.

Anasema ni jukumu la wazazi kuwafundisha watoto kwa upole bila kutumia fimbo, kwani tabia zao hazijengwi kwa kiboko.

Mratibu wa mradi wa watoto unaohusisha vijiji 10 vya Kata ya Masama Rundugai, Hans Harold, anasema wanatarajia baada ya mafunzo hayo walengwa watabadilika na kuwalea watoto wao vema.

Harold anasema tangu mwaka 2004  wanahudumia watoto na sasa wana watoto 155 waliopo shule za awali, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu.

Anataja vijiji 10 wanakotoka watoto hao kuwa ni Mtakuja, Chemka, Rundugai, Chekereni, Ngusero, Mbatakero, Mkalama, Longoi na Kawaya.

Anasema wanatamani kuona watoto hao wakiishi maisha bora yasiyokuwa na msongo wa mawazo, ndiyo maana wanatoa mafunzo ya mbinu za wazazi kuwalea watoto na mabadiliko yao ili kujenga uhusiano bora baina yao.

Anasema wanautamaduni wa kukutana na watoto hao, kucheza na kupata mlo kwa pamoja, kuwapatia mahitaji ya msingi ya shule ikiwamo madaftari, nguo za shule, viatu na mahitaji ya nyumbani.

“Pia tunawalipia ada na michango ya shule, lengo letu ni kuhakikisha wanaishi maisha mazuri,” anasema na kuongeza:

“Huwa tunawapeleka kutembelea mbuga za wanyama na kuhakikisha wanapata mafunzo ya kiroho.”

Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka Smart Community on Legal Protection Organization. Mary Mwita, anawasisitiza wazazi na walezi kutenga muda maalumu wa kukaa na watoto wao ili kubaini yanayowasibu pindi wanapokuwa mbali nao.

Mwita anasema fimbo haibadili tabia ya mtoto bali humwongezea hofu. Ni vema kumsema na kumsikiliza pindi anapohitaji kujieleza, hii itambadilisha haraka zaidi kuliko kumpiga.

Anawashauri wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kuwapongeza watoto wao  pindi wanapofanya jambo la kufurahisha.

Anatoa mfano endapo mtoto atafanya kazi za nyumbani vizuri au kufanya vema darasani  anastahili kupungezwa hata kwa zawadi ili kumuhamasisha kuendelea na tabia hiyo.

“Wazazi mnatakiwa kuchora jedwali la kuonyesha makosa wanayotenda watoto na mambo mazuri wanayoyafanya na wanayopaswa kujifunza,” anashauri.

Mwita anawataka wazazi kukubaliana na tabia ya mtoto anayeongea sana akidai kuwa huwa wanabadilika baadaye.

Pia anawasihi wazazi kutowakaripia watoto mbele ya watu wengine na kumwambia kwamba ana tabia mbaya kwani nao hujisikia vibaya kama ilivyo kwa wakubwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,491FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles