Mtibwa Sugar yaipania Ndanda

0
730

Mwandishi wetu

KOCHA  wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, amesema watahakikisha  wanapambana ili waweze kupata ushindi dhidi ya Ndanda.

Mtibwa Sugar ambao  msimu huu hawajaonya utamu wa Ligi Kuu Tanzania Bara  wanatarajia kucheza na Ndanda Oktoba 19, mwaka huu, kwenye  Uwanja wa Nangwanda Sijaona, mkoani Mtwara.

Tayari Mtibwa Sugar imecheza michezo mitano na kufungwa mitatu huku ikitoka sare mbili.

Timu hiyo ilianza ligi hiyo kwa kufungwa na Lipuli mabao 3-1, kisha ilichapwa na  Simba 2-1, kabla ya kutoka suluhu na JKT Tanzania na baadaye kufungwa na Tanzania Prisons 3-1 na kutoka sare ya bao 1-1 na Mbeya City.  

Akizungumza na MTANZANIA jana, Katwila alisema  kutokana na timu yake kufanya vibaya wamejipanga kuhakikisha wanapata pointi tatu dhidi ya Ndanda.

Katwila alisema wamefanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita  na anaimani kikosi chake kipo vizuri kwa mchezo unaofuata.

 “Tupo kwenye maandalizi ya kukutana na Ndanda mchezo ambao tutakuwa ugenini, lazima tuzidishe umakini kutokana na rekodi ya matokeo ya nyuma tuliyopata kwani tumepania kwenda kuonyesha uwezo wa Mtibwa ya zamani,” alisema.

Alisema licha ya kupata matokeo yasiyoridhisha wapinzani wao Ndanda wasitarajie kupata matokeo kirahisi mbele yao kwa kuwa mipango yao ni kupata pointi tatu.

Katwila aliwataka mashabiki wa timu yao kuendelee kuwapa sapoti ili  waweze kutimiza malengo  waliyojiwekea. Mtibwa Sugar inashika nafasi ya 19 katika msimamo wa ligi hiyo kutokana na pointi mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here