31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Ninatimiza ndoto za Nyerere

Elizabeth Hombo -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli ameelezea namna Serikali ya awamu ya tano inavyomuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kufanya mambo mbalimbali ya maendeleo ambayo alitamani kuyafanya.

Alieleza hayo jana wakati akihutubia wananchi katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha mwasisi huyo wa taifa, yaliyofanyika kitaifa mkoani Lindi.

Rais Magufuli alisema Serikali yake itaendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuheshimu tunu za Mwenge pamoja na kuendelea kuthamini vijana, ikiwemo kuwateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi.

Katika hilo, aliwataka vijana watakaoteuliwa kushika nafasi mbalimbali wajitahidi kufanya kazi kwa bidii na uzalendo mkubwa.

Vilevile alisema Serikali yake imejitahidi kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kupambana na vitendo vya rushwa, wizi na ubadhirifu wa mali za umma.

“Mambo hayo Mwalimu Nyerere aliyachukia enzi za uhai wake na kutokana na hilo, tumeanzisha kitengo maalumu cha mahakama cha kushugulikia mafisadi, pia tumeondoa watumishi hewa takribani 20,000 na wafanyakazi wenye vyeti vya kughushi takribani 14,000,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ili kuendelea kuenzi mchango mkubwa uliotolewa na Mwalimu Nyerere, hawana budi kuwafundisha vijana kuhusu mambo muhimu ambayo yalisimamiwa na mwasisi huyo katika uhai wake.

Aliyataja mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyasimamia kuwa ni pamoja na uzalendo, uaminifu, nidhamu, uchapakazi na moyo wa kujitolea.

Alisema Mwalimu Nyerere aliyazingatia hayo kwa sababu bila hivyo, taifa litakuwa limeangamia kwa sababu vijana ni kundi kubwa na viongozi wa leo na kesho.

“Ninawaomba Watanzania tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kutimiza maoni yake aliyoyatamani kuyatimiza, kusimamia miiko ya Azimio la Arusha pamoja na kudumisha umoja bila kubaguana kwa dini wala kabila,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema Serikali yake inamuenzi Baba wa Taifa kwa kutekeleza ndoto yake ya kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma.

“Na tayari viongozi wa Serikali na watendaji wengine wameshahamia Dodoma na mimi pia nimehamia rasmi jijini Dodoma juzi,” alisema Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli alisema Tanzania ina kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa Mwalimu Nyerere kuzaliwa katika taifa hili.

“Hii ni bahati ya pekee sana kwa nchi yetu, ninawapongeza viongozi wa awamu zilizofuata kwa kuweka mazingira mazuri ya kumuenzi Baba wa Taifa,” alisema.

Alisema akishirikiana na Rais wa Zanzibar, Dk. Mohamed Ali Shein wamendelea kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kudumisha amani na kwamba Watanzania wamebaki kuwa wamoja na Muungano umeendelea kuimarika.

UMUHIMU WA MWENGE

Rais Magufuli pia amezungumzia umuhimu wa Mwenge wa Uhuru, akisema kuwashwa kwa Mwenge huo mwaka 1961 ilikuwa ni ishara ya ukomo wa dhuluma, dharau na uonevu vilivyokuwa katika utawala wa wakoloni.

Kutokana na hilo, alisema hiyo ilikuwa ishara ya mwangaza na matumaini mapya kwa taifa.

“Mwalimu Nyerere aliamini uhuru wa Tanzania usingekuwa na maana endapo mataifa mengine yangebaki chini ya utawala wa kikoloni,” alisema.

Aidha alisema dhamira hiyo ya Mwalimu Nyerere ndiyo ilisaidia harakati za ukombozi katika nchi nyingine zilizo kusini mwa Afrika.

“Ndiyo maana Oktoba mwaka 1959 Mwalimu Nyerere alitamka namnukuu; ‘Sisi Watanganyika tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau’,” alisema Rais Magufuli.

Pia alisema Mwenge huo uliwekwa juu ya Mlima Kilimanjaro ili mwanga wa matumaini usiishie Tanzania peke yake, bali usambae katika mataifa mengine Kusini mwa Afrika kufanikisha ukombozi.

“Mwalimu Nyerere aliamua taifa letu kuwa kitovu cha harakati za ukombozi na nchi yetu ilishiriki kikamilifu katika ukombozi wa Bara la Afrika,” alisema Rais Magufuli.

Kutokana na hilo, alisema akishirikiana na Dk. Shein, wataendeleza kuwepo Mwenge wa Uhuru na utakimbizwa katika maeneo yote nchini.

RIPOTI TAKUKURU

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimkabidhi Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo ripoti ya miradi 107 iliyobainika kuwa na dosari.

 “Mkuu wa Takukuru sogea hapa mbele nikukabidhi ripoti hii, naikabidhi hii ripoti ukafanye ukaguzi kila ukurasa, kila nukta na ukachambue wale wote wanaohusika kupelekwa mahakamani usisite kuwapeleka mahakamani.

“Wale ambao utaona ni wakubwa unafikiri ni ngumu niletee ripoti yao mimi nitafanya kazi yangu. Nataka Tanzania inyooke, hatuwezi tukawa tunapeleka fedha inachezewa tu na ndio maana nawapongeza sana vijana hawa kwa kukimbiza Mwenge.

“Ni matumaini yangu kwamba ofisi ya Waziri Mkuu pia itafuatilia miradi hii, maana najua na Waziri Mkuu huwa anafuatilia hadi nukta,” alisema.

Awali katika risala yake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Mkongea Ally, alisema katika maeneo walikopita mbali na wananchi kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo, wamemwomba kufuatilia kwa ukaribu miradi ya maji na kuwachukulia hatua stahiki wanaobainika kuhujumu miradi hiyo.

MIRADI 107 YENYE KASORO

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu, miradi 107 ya maendeleo ya Sh bilioni 90.2 kwenye halmashauri 82 nchini ina kasoro.

“Mheshimiwa Rais, Mwenge ulibaini kasoro katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ya maji, elimu, barabara na ujenzi wa majengo ya umma.

“Miradi hiyo haikufunguliwa au kuwekwa mawe ya msingi kutokana na kasoro hizo zisizoendana na matumizi ya fedha katika miradi husika.

“Kujengwa kinyume na mikataba na makadirio yaliyopitishwa na wataalamu, makandarasi kushindwa kufuata na kusimamia kanuni za ujenzi.

“Ilifanya ubora wa miradi hiyo kutia shaka, hususani katika suala la uimara, jambo jingine ni matumizi duni ya vifaa katika miradi ya umma.

“Mwenge pia umebaini wakandarasi kutosimamia majukumu wanayopewa kwa wakati na mamlaka husika na kutowachukulia hatua za kisheria,” alisema Mhagama.

Alisema baadhi imekuwa na ubora usioridhisha, hasa ujenzi wa visima vya juu vya kuhifadhia maji, ambavyo kuta zake zilikuwa na nyufa na kabla ya miradi hiyo kuanza kutumika.

“Lingine ni udanganyifu katika lugha za kitaalamu, hususani miradi ya maji na ujenzi na hivyo kuwa vigumu kwa viongozi ambao hawana utaalamu kubaini matumizi ya fedha za umma zilizotumika vibaya.

“Ufanyaji wa makadirio ya gharama za ujenzi zisizoendana na gharama zilizo sokoni, vitendo vinavyofanywa na wahandisi wetu katika miradi na kuhujumu fedha za Watanzania,” alisema waziri huyo.

MWENGE WAZIDUA MIRADI 28

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, alisema Mwenge huo umeambatana na kuzinduliwa miradi 28 ya Sh bilioni 12.8.

Alisema kwa kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inahusu maji ni uhai, mkoa huo unaendelea kusambaza maji kwa wananchi wake.

“Upatikanaji maji vijijini katika mkoa wetu ni asilimia 57 na mijini ni asilimia 68, tunaamini kwa kipindi kilichobaki tunaweza kufika kwa kiwango ambacho kinaelekezwa katika ilani ya uchaguzi ya CCM,” alisema Zambi.

Akizungumzia kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, alisema Takukuru Mkoa wa Lindi ilipokea taarifa 249 za rushwa kati ya Julai mwaka jana na Septemba mwaka huu.

Zambi alisema kati ya taarifa hizo, wamefungua majalada 32 na kuendelea na uchunguzi katika kesi 73 na kushinda 11.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles