Mtandao utoaji taarifa za matibabu wazinduliwa

0
971

NA PATRICIA KIMELEMETA- DAR ES SALAAM

Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wamezindua mtandao wa utoaji wa taarifa za matibabu (TanzMED).

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk. Amos Nungu, alisema mtandao huo ulianzishwa mwaka 2011 baada ya kundi la vijana wakiwamo madaktari wabobezi na wataalamu wa tehama kufanya utafiti wa utoaji wa taarifa za matibabu kwa njia ya mtandao.

Alisema ilipofika mwaka 2014, ulizinduliwa rasmi na mwitikio kwa wananchi kutaka kujua taarifa za afya na matibabu yake unaongezeka siku hadi siku.

Alisema kutokana na hali hiyo, taarifa za magonjwa yote yakiwamo Ukimwi, kisukari, magonjwa ya moyo, kliniki ya watoto, hospitali zilizo karibu na zinazotumia bima ya afya na mengineyo utazipata kupitia mtandao huo.

“TanzMED ilianzishwa baada ya kundi la vijana kuja na wazo la utoaji wa taarifa za matibabu kwa njia ya mtandao, jambo ambalo liliungwa mkono na Costech na kulifanyia kazi, hivyo basi wananchi wataweza kupata taarifa za matibabu, ushauri na maelekezo kupitia mtandao huo,” alisema Nungu.

Alisema wananchi wanaotumia lugha ya Kiswahili kutoka ndani na nje ya nchi wanaweza kujiunga na mtandao huo utakaowasaidia kuunganishwa na wataalamu wabobezi wa afya ili kupata taarifa hizo jambo linaloweza kuwasaidia katika huduma za matibabu.

Naye Mtaalamu wa Tehama wa mtandao huo, Mkata Nyoni, alisema kwa siku zaidi ya watu 700 kutoka ndani na nje ya nchi wanautembelea mtandao huo kwa ajili ya kuuliza mambo mbalimbali yanayohusu afya.

“Idadi kubwa ya vijana wenye umri kati ya miaka 24 hadi 44 wanaingia kwa siku kutoka ndani na nje ya nchi ili kupata taarifa mbalimbali za matibabu, lengo ni kuwasaidia wananchi waliokua mbali na vituo vya afya ili waweze kupata taarifa  sahihi,” alisema Nyoni.

Alisema mkakati wao ni kuwashawishi wananchi waweze kujiunga na mtandao huo utakaowasaidia kupata taarifa za matibabu na ushauri bila ya kulipia gharama yoyote.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here