27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wanafiki wanalichelewesha Taifa

Yapo maradhi wengine wanaweza kuyaona madogo, lakini ukiyatazama kwa kina unaweza kukubaliana nasi  pasipo na shaka kwamba ni miongoni mwa mambo yanayolitafuna Taifa letu kidogokidogo.

Miongoni mwa maradhi hayo ambayo hata Mitume wa madhehebu mbalimbali walishindwa kuyavumilia ni uongo na unafiki.

Pengine kabla hatujakwenda mbali, hebu tujikumbushe tafsiri sahihi ya neno ‘unafiki’, ambalo kwa jicho lingine linabeba tafsiri ya uongo.

Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno “Unafiki” ni; hali ya kujifanya kuwa ni rafiki na hali ni adui; hali ya kutokuwa mkweli.

Wengine wanasema ‘unafiki’ ni kujifanya mwema machoni pa watu ili kupata sifa.

Wenye imani zao wanasema Yesu Kristo aliuchambua unafiki kwenye eneo la kukosoana au kuhukumiana baada ya kuona mabigwa wa kukosoa wengine wao wenyewe ni wakosaji wakubwa.

Kwa ujumla binadamu wengi wa leo wanachokisema na kukitenda si kile wanachokimaanisha.

Ni watu wachache wenye ujasiri wa kusema kile wanachokimaanisha.

Tunasema hivyo kwa sababu kwa muda mrefu Watanzania tumeendelea kushuhudia maigizo hata katika mambo  yanayogusa Taifa na pengine kuathiri mustakabali wa nchi yetu.

Leo hii ukitaka kujua kwamba tumefika kiwango cha juu cha uongo au unafiki ni kwamba ili uwe kiongozi ama uteuliwe au uchaguliwe, ni lazima uwe mnafiki.

Ipo orodha ndefu inayothibitisha jinsi unafiki unavyolitafuna Taifa, mfano matukio ya madiwani au wabunge kuhama vyama vyao na kuisababishia nchi hasara ya kurudia uchaguzi, licha ya kutovunja sheria, lakini ukitazama msingi wake utagundua kuna unafiki.

Si hilo tu, matendo ya wanasiasa wakati wanatafuta kura huwa ni tofauti sana na wanayohubiri wakiwa madarakani.

Kwa sababu ya unafiki wa kiwango cha juu, baadhi ya viongozi wetu wapo tayari kufanya maigizo ya siku moja ili tu kumridhisha mkubwa mmoja wakati hali halisi haipo hivyo.

Zipo nyakati tulizoshuhudia maji yakitoka kwa siku moja kwa sababu tu kiongozi fulani wa juu amefanya ziara katika eneo hilo na akiondoka hayatoki tena.

Lakini pia tumeona usafi ukifanyika au rangi kupakwa kuta za mbele na wanafiki zinapotokea ziara za viongozi wakubwa wa kitaifa na kimataifa na hivyo kupotosha uhalisia wa jambo au shida ya eneo husika ilivyo.

Jambo ambalo tumekuwa tukilitazama kwa namna ya kuchukizwa ni hatua ya baadhi ya watu kufika mahali kufanya unafiki/uongo kama mtaji wa kufanikisha mambo yao hata kupitia mambo makubwa yanayogusa maslahi ya Taifa.

Kibaya zaidi viongozi mara nyingi ni kama na wao hutoa baraka kwa sababu ya kuwapa wanafiki nguvu na madaraka makubwa ambayo huyatumia kufanikisha mambo yao kwa njia za hila.

Rais Magufuli ni mtu asiyependa mchezo mchezo, zipo nyakati tunatamani asiamini wanafiki kwa sababu tunajua watamwangusha.

Wanafiki ambao Rais Magufuli anatakiwa kutowaamini na pengine kuwaogopa ni pamoja na wale ambao licha ya upeo wao mkubwa wa kuona mambo, lakini wapo tayari kumsifia hata katika mambo ambayo hayapo sawa sawa.

Wanafiki ambao Rais Magufuli anatakiwa kuwatambua ni wale ambao akichukua uamuzi wa jambo fulani hata kama lina ukakasi utawaona wapo mstari wa mbele kumuunga mkono.

Tunaamini tukiweka unafiki pembeni, suala linaloligharimu Taifa kwa sasa la chaguzi za marudio kwa sababu tu viongozi waliochaguliwa kuhama vyama, litatafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili kunusuru fedha za wavuja jasho wanazokwamuliwa kupitia kodi mbalimbali.

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles