25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Mtaalamu: Ujenzi Dodoma uzingatie viwango kupunguza madhara ya tetemeko

Nyumba zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi Kagera
Nyumba zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi Kagera

Na LEONARD MANG’OHA – DAR ES SALAAM

TETEMEKO la ardhi lililotokea Septemba 10 mwaka huu mkoani Kagera limeonekana kama jipya na la kwanza nchini, lakini ukweli ni kwamba si la kwanza.

Hadi linatokea tetemeko hilo ilikuwa ni kiasi cha takribani miezi miwili tu imepita tangu kutokea tetemeko lingine huko mkoani Dodoma lakini tofauti ya matetemeko hayo mawili ni kwamba lile la Kagera limesababisha maafa kwa binadamu.

Maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi huko Kagera ndilo jambo ambalo linafanya tukio hilo kuwa geni miongoni mwa Watanzania.

Wako baadhi ya watu walioweka sauti na picha katika mitandao ya kijamii wakiigiza lafudhi ya Kihaya kuwa wao ni watu wa tabaka la juu hivyo hupatwa na majanga makubwa ya kimataifa wakieleza tukio lililowapata limekuwa likitokea katika mataifa makubwa kama Japan na mengineyo, tofauti na Dar es salaam ambao hukumbwa na majanga kama kipindupindu.

Idara ya Jiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, ilieleza kuwa kitovu cha tetemeko la Kagera kilikuwa umbali wa kilomita 40 chini ya ardhi hivyo kusababisha miamba mikubwa kupasuka hali iliyosababisha misuguano mikubwa ya vipande vikubwa vya miamba vilivyogandamizwa kuliko kikomo chake cha mgandamizo.

Maeneo yaliyopitiwa na bonde la ufa yanatajwa kuwa moja ya maeneo yaliyo katika hatari ya kukumbwa na matetemeko ya mara kwa mara kwa sabbau ni maeneo ambayo tayari yalikwisha kumbwa na mtikisiko hivyo miamba yake si imara sana.

“Tetemeko la ardhi tunaloliongelea limetokea karibu na mkondo wa bonde la ufa la Afrika Mashariki, sehemu ambayo matetemeko ya ardhi yanatarajiwa kujitokeza kutokana na uhalisia wa kijiolojia na kijiografia wa sehemu hiyo,” ilieleza taarifa ya idara hiyo.

Pamoja na maeneo mengine yaliyopitiwa na bonde la ufa, mikoa ya Songwe na Dodoma ni moja ya maeneo yanayoelezwa kuwa si salama kutokana na kukumbwa na matetemeko ya ardhi ya mara kwa mara.

Akizungumza na MTANZANIA, Kaimu Mkuu wa Idara ya Jiolojia Chuo Kikuu cha Dar es saam, Elisante Mshiu, anasema kutokana na kutokea kwa matetemeko ya mara kwa mara katika mkoa huo kumefanya miamba yake kutokuwa imara.

Katika kipindi hiki ambacho serikali imeanza kuhamia Dodoma, Mshiu anasema ni vema ikaweka mikakati na kuzingatia vigezo vya ujenzi wa majengo na miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha inakuwa imara na hivyo kuzuia madhara kuwa makubwa pindi litakapotokea tetemeko.

“Tunahitaji maandalizi kukabiliana na matetemeko, kwa sasa kuna taarifa za kujengwa bwawa kubwa kwa ajili ya kuwezesha kupitakana kwa maji, miradi kama hii inapaswa kujengwa katika ubora wa hali ya juu,” anasema Mshiu.

Anasisitiza kuzingatiwa kwa vigezo vya ujenzi wa majengo marefu kulingana na jiografia ya eneo husika na ikiwa eneo limeshauriwa kujengwa majengo yenye ghorofa nne lizingatiwe.

“Kuwe na sera ya ujenzi hata kwa wananchi wa kawaida,” anasema.

Anasema madhara yaliyojitokeza Kagera yanapaswa kuchukuliwa kama fundisho kwa kujenga nyumba zilizo imara ili kupunguza hatari pale linapotokea tetemeko.

Mtaalamu huyo anasema wananchi wanapaswa kutambua kuwa nyumba juu ya ardhi ni kama karatasi kwa sababu linapotokea tetemeko kutokana na nguvu za mgandimizo huweza kutokea madhara.

Anasema pia iko miamba ya aina tofauti, kuna migumu na laini na hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine.

Miamba tabaka ni moja ya aina ya miamba laini ukilinganisha na aina nyingine za miamba na inaelezwa kuwa hulainika haraka na kuachana pale inapokumbana na mgandamizo mkubwa hivyo huachana na kuruhusu kutokaea kwa tetemeko la ardhi.

Mikoa ya Kagera na Dodoma inaelezwa kuwa ni moja ya maeneo yenye miamba hiyo ukilinganisha na kipenyo cha miamba migumu ndiyo maana kunakuwa na madhara makubwa pale linapotokea tetemeko.

“Kutokana na miamba hii kuwa laini mgandamizo unapotokea hulainika na kuwa kama mawimbi ya maji kutokana na mgamdamizo mkubwa na hivyo kushindwa kuhimili hupasuka na kusababisha tetemeko,” anasema.

Anasema kwa kuwa serikali imeamua kuhamia Dodoma inapaswa kuhakikisha miundombinu inayojegwa mkoani humo inakuwa na ubora wa hali ya juu na kusisitiza ujenzi wa nyumba imara kwa wakazi wote wa mji huo.

Japo kiuhalisia hakuna sehemu iliyo salama zaidi lakini linapokuja suala la tetemeko la ardhi ni vema kuhakikisha ushauri wa kitaalamu unazingatiwa ikiwa ni pamoja na kutojenga kandokando ya milima ili kuepuka kuporomokewa na mawe.

[email protected] 0763207431

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles