27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mbinu za kumfanya mtoto akuheshimu, kukusikiliza

pix-wazazi

Na CHRISTIAN BWAYA,

MSOMAJI mmoja wa safu hii aliniandikia ujumbe mfupi wa maneno akidai kuwa mwanawe hamsikilizi. Kwa mujibu wa mzazi huyu, pamoja na kufanya jitihada za kumwelekeza mwanae mambo muhimu ya kimaisha, bado kijana wake huyo haonekani kusikiliza. Anasema kadri anavyomwadhibu, ‘ndivyo anavyozidi kuwa mkaidi…’

Mzazi huyu, inavyoonekana, amepoteza mamlaka yake kama mzazi. Mamlaka kimsingi ni uwezo wa kusema kitu na kikasikika bila kulazimika kutoa adhabu. Unapokuwa na mamlaka maana yake unayo nguvu ya ushawishi inayomfanya mtoto awe tayari kukuiga, kukusikiliza, kukuelewa na kufanya kwa hiari yake yale unayomwelekeza.

Ni ukweli ulio wazi kuwa ushawishi wa mzazi kwa mtoto wake hauji hivi hivi. Ushawishi ni matokeo ya jitihada za muda mrefu zinazofanywa na mzazi ili kuwekeza katika uhusiano na mwanawe tangu mapema. Tutazame maeneo manne yanayoongeza ushawishi wa mzazi kwa mtoto.

Kuaminika

Mamlaka yako mzazi kwa mwanao yanategemea kiwango cha imani alichonacho kwako. Kukuamini maana yake, kwanza, hana shaka na nia yako njema kwake na pili, anaamni anayo nafasi ya pekee kwako kama mzazi wake.

Kwa kawaida, mambo madogo madogo mno ndiyo humfanya mtoto aongeze imani yake kwako. Kwa mfano; kutumia sehemu ya muda wako kwa ajili yake kwa kufanya mazungumzo na matembezi naye, kufurahia yale mema yanayomgusa zaidi, humfanya mtoto akuamini. Kuaminika kunakwenda sambamba na vile unavyoonesha kumthamini kama mtu anayestahili heshima.

Msimamo usioyumba

Hakuna kitu kibaya kama kutokueleweka unataka nini. Kutokueleweka kunakotokana na kubadilika badilika, kunatuma ujumbe mbaya kuwa huna uhakika na usahihi wa kile unachokidai kwake. Hali hii ya kutokutabirika kwako humfanya atake kuendelea kujaribu bahati yake kwa sababu tayari ana wasiwasi na mamlaka yako kama wazazi.

Ili kujihakikishia mamlaka ni muhimu kuwa na msimamo wa pamoja na mzazi mwenzako. Kupingana wazi wazi na msimamo na maamuzi ya mzazi mwenzako mbele ya mwanao huwapunguzia mamlaka yenu kama wazazi na ni kutengeneza mazingira ya kujaribiwa kwa mamlaka yenu mara kwa mara.

Kuishi unayoyasema

Mtoto hujifunza zaidi kwa yale unayoyafanya kama mzazi kuliko yale unayoyasema. Mamlaka yako kama mzazi yanategemea na namna maneno yako yanavyooana na yale unayoyafanya. Mtoto anapokuona ukifanya yale yale unayomzuia yeye anakupunguzia alama za ushawishi wako kwake.

Hakikisha unaishi maneno yako. Tenda unayoyasisitiza. Unapomwambia ashukuru anapopewa kitu, kuwa mfano kwa kuwa mtu wa shukrani. Unaposisitiza aombe msamaha, jitahidi kuonesha mfano kwa kuomba msamaha pale unapojikwaa.

Mstahi anapokosea

Unafanya nini pale unapogundua mwanao amekosea? Unamkemea kwa ghadhabu tu kwa sababu ni mtoto? Ni vizuri kuelewa kuwa watoto, kama sisi tulio watu wazima, wanatamani sana kutendewa kwa staha. Unapomtendea kwa staha unamfanya ajione analo deni la kukulipa heshima unayostahili.

Hakuna sababu ya kumkemea mtoto kupita kiasi hata kama unajua ni kweli amekosea. Hakuna sababu ya kumvunjia heshima kwa kumdhalilisha mbele ya rafiki zake. Unapofanya hivyo, ni rahisi kujenga kisasi cha utoto. Usipomstahi mwanao, unapoteza mamlaka yako kwake.

Kwa ujumla, mamlaka yako kama mzazi ni zao la maisha yako yanayohalalisha kusikilizwa. Ukijenga uhalali kama mzazi, hutalazimika tumia nguvu nyingi kutafuta ushiwishi kwa mwanao.

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles