23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, August 11, 2022

Kanuni za kuongeza ushawishi wa hoja zako

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa anayeweza kujenga ushawishi.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa anayeweza kujenga ushawishi.

Na CHRISTIAN BWAYA,

KWA nyakati tofauti kila mmoja wetu hutamani kuwa na ushawishi kwa wengine. Ni kawaida kutamani hoja tunazozitoa zipokelewe na wale tunaowatumia ujumbe husika. Ili ujumbe upokelewe, inahitajika nguvu inayoweza kuwasukuma wengine kuupenda, kuukubali na ikiwezekana kubadilika kwa sababu ya ujumbe husika. Nguvu hii inaitwa ushawishi.

Kwa hakika ushawishi ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Viongozi kwa mfano, wanatamani kuwa na ushawishi kwa wafuasi wao. Mzazi, kama kiongozi wa familia, angependa kuwa na ushawishi kwa mwanawe. Kwa ujumla, urafiki, siasa, uhusiano wa kijamii, kazi na maeneo mengine mengi yanadai ushawishi.

Ikiwa unatamani kuwa na ushawishi, makala haya yanaangazia kanuni kadhaa za kuwasilisha ujumbe wako ili kuoongeza uwezekano wa wengine kukubaliana nao.

Jenga uhalali wako

Wewe kama msemaji wa ujumbe unayo nafasi kubwa sana ya ushawishi pengine kuliko ujumbe wenyewe. Wasikilizaji wako hawawezi kuzingatia ujumbe kama hawajakuchukulia kwa uzito wewe uliye na ujumbe. Hivyo, kabla hujatumia nguvu nyingi kwenye ujumbe unalazimika kujenga uhalali wako.

Kujenga uhalali ni kuwaaminisha wale wanaokusikiliza kuwa unaelewa kile unachokisema. Watu wana kawaida ya kuheshimu weledi. Kama unazungumzia mambo ya uchumi, watu wangependa kujiridhisha kuwa unaufahamu uchumi vilivyo. Kwa hivyo, unalazimika kuwahakikishia wasikilizaji wako kuwa unao utaalamu wa kile unachokizungumza.

Kingine katika kujenga uhalali ni kuwaondolea wasikilizaji wako shaka ya mgongano wa maslahi na kile unachokisema. Ni vigumu mtu anayefahamika kuwa mpiga debe wa bidhaa fulani kuchukuliwa kwa uzito unaostahili ikiwa atabainisha ‘anawamba ngoma’.

Kadhalika, mwonekano unaokubalika na wasikilizaji huwa unabeba nafasi kubwa ya kiushawishi. Hakikisha unakuwa katika mwonekano unaotarajiwa. Kwa mfano; ikiwa wasikilizaji wako wanatarajia uonekane katika mavazi fulani, litakuwa ni kosa kubwa kuonekana tofauti. Mavazi, lugha unayotumia, namna unavyoongea, matumizi ya lugha ya ishara, vyote kwa pamoja vinabeba ujumbe mzito kuliko hata ujumbe wenyewe.

Unavyouweka ujumbe wako

Tafiti zinaonesha kuwa hata wasikilizaji wasioelewa kile unachokisema wanazo mbinu za kuamua ujumbe gani wanaweza kuuchukua na upi wakuachie wewe msemaji. Moja wapo ya mbinu hizo ni kujiridhisha kuwa ujumbe husika haulengi kuwadhalilisha na kuwabadilisha. Upo ukweli kuwa binadamu hatufurahii pale tunapogundua kuna mtu anafanya bidii ya kutaka kutubadilisha. Kwa kulitambua hilo, unahitaji kuwaheshimu wasikilizaji wako kwa kutokuonesha wazi wazi nia ya kuwabadilisha watu  vinginevyo, wataupuuza mapema kabisa.

Kadhalika, ujumbe ulio dhahiri unaojenga matarajio chanya huongeza hamasa ya kupokelewa na kufanyiwa kazi kuliko ujumbe hasi unajenga hofu. Ni kweli kuwa ujumbe hasi hugusa hisia za watu kirahisi mno.

Hata hivyo, tafiti zinaonesha hofu huwa haiambatani na utendaji kwa sababu watu huvutiwa na kuufanyia kazi ujumbe unaojenga taswira chanya ya kile kinachowezekana na kamwe si kile kisichowezekana.

Sambamba na hilo, ni muhimu kuelewa watu hawana tabia ya kupenda hoja zinazohitaji nguvu nyingi kuzielewa na zisizokidhi mahitaji yao halisi. Hoja ngumu inayoonesha tofauti kubwa ya kimtazamo na wasikilizaji, hujenga upinzani na juhudi za kutotaka kuielewa. Kwa hiyo, ikiwa unapenda kujenga ushawishi kwao, ni muhimu kufanya jitihada za kurahisisha hoja zako na kuzioanisha na mahitaji halisi ya wasikilizaji.

Itaendelea wiki ijayo…

Mwandishi ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com Simu: 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,411FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles