22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

MSUVA KUIKOSA BOTSWANA IKIIVAA STARS

Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Salum Mayanga, amemwita kwenye kikosi chake hicho kiungo wa Yanga, Emmanuel Martin, ili kuziba nafasi ya Simon Msuva.

Msuva anayekipiga katika klabu ya Difaa Hassan El-Jadida, inayoshiriki Ligi Kuu Morocco, ameshindwa kujiunga na kikosi cha Taifa Stars kinachojiandaa kuikabili Botswana katika pambano la kalenda la Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), litakalopigwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mbali ya Msuva, mchezaji mwingine aliyeitwa na Mayanga katika kikosi hicho ambaye ameshindwa kuripoti mpaka jana ni Orgenes Mollel.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas, alisema wachezaji hao watakosekana kwenye mchezo huo baada ya kushindwa kuwahi mazoezi ya pamoja na wachezaji wengine wa Taifa Stars.

Alisema kutowasili kwa wachezaji hao kumemlazimu Mayanga kumjumuisha Martin, ambapo sasa kikosi hicho kitakuwa na wachezaji 20 badala ya 21 aliowaita kwa mara ya kwanza.

“Ni wazi Msuva na Mollel hatutakuwa nao katika mchezo dhidi ya Botswana baada ya kushindwa kufika katika muda uliokusudiwa.

“Tiketi ya ndege ya Msuva inaonyesha atafika Alhamisi usiku maana yake ni kwamba atachelewa mazoezi kutokana na mzunguko wa safari yake kuonyesha atapita Cassablanca kisha Dubai,” alisema Lucas.

“Mollel naye atashindwa kujiunga na timu ya Taifa kutokana na kikwazo cha Shirikisho la Soka Ureno (FPF), kushindwa kumruhusu kwa wakati mwafaka,” alisema Lucas.

Nyota wengine wa Tanzania wanaokipiga soka la kulipwa mataifa mbalimbali ambao tayari wamejiunga na kikosi hicho ni mshambuliaji wa KR Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta, beki wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda na mpachika mabao, Elias Maguli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles