29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

KISA LIPULI LWANDAMINA, AWAKOMALIA AJIB, NGOMA

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, bado anahaha kuisuka safu yake ya ushambuliaji ili kuhakikisha inafunga mabao ya kutosha.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walianza msimu mpya kwa kusuasua baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na Lipuli katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Lipuli inayofundishwa na kiungo wa zamani wa Simba, Seleman Matola, ilionesha kiwango maridadi huku ikifanikiwa kufunga bao la kuongoza kabla ya Yanga kusawazisha.

Kabla ya sare na Lipuli, Yanga ilichapwa na Simba penalti 5-4 katika pambano la Ngao ya Jamii baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 kwa suluhu.

Katika mazoezi yaliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Lwandamina alionekana akitilia mkazo katika kuwapika washambuliaji wake pamoja na kuimarisha safu yake ya ulinzi.

Lwandamina alikigawa kikosi chake katika makundi matatu, kila moja likiwa na washambuliaji wanne na mabeki wanne.

Kwa upande wa washambuliaji walitakiwa kuchukua mpira katikati ya uwanja na kuingia nao eneo la hatari ambako walikutana na mabeki na kutakiwa kutafuta mbinu za kuwapita na kufunga mabao.

Hata zoezi hili halikuhusu kundi zima, badala yake lilifanyika kwa utaratibu wa mshambuliaji mmoja kutakiwa kumvaa  beki mmoja.

Kundi la kwanza la washambuliaji lilikuwa Donald Ngoma, Ibrahim Ajib, Yusuph Mhilu na Matheo Antony, wakati Abdallah Shaibu, Juma Abdul, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Haji Mwinyi, walikuwa mabeki.

Kundi la pili liliundwa na Emmanuel Martin, Juma Mahadhi, Said Juma na Pius Buswita, wakati mabeki wakiwa Andrew Vincent, Kessy Ramadhani na Pato Ngonyani.

Kundi la mwisho alikuwepo Kabamba Tshishimbi, Thaban Kamusoko, Said Juma na Maka Edward, huku Ninja, Abdul, Cannavaro na Mwinyi wakiunda timu ya mabeki.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema baada ya sare yao na Lipuli wamekuwa wakifanyia maboresho kikosi chao ili kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Njombe Mji.

Alisema licha ya baadhi ya wachezaji kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars hali hiyo haitawaathiri kwa kuwa bado wana hazina kubwa ya wachezaji.

“Nafahamu tunakabiliwa na michezo ya ugenini, ukizingatia awali tulicheza na timu ambayo imepanda daraja na mechi inayofuata na wao vile vile ni wageni na wameweza kuonyesha uwezo mzuri,  tunatakiwa tukapambane kwa ajili ya kuhakikisha tunapata pointi tatu.

“Kimsingi kila unapocheza mechi moja unajiuliza kuhusu inayofuata, ndivyo mpira ulivyo, jambo la msingi tunawaomba mashabiki wa Yanga waendelee kutuunga mkono kwa kuwa  hii ni vita na kila mmoja anataka kushinda,” alisema Nsajigwa.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles