24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

RC AAGIZA MKURUGENZI BODI YA KOROSHO AKAMATWE

NA FLORENCE SANAWA – MTWARA

MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya, kumkamata Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Hassan Jarufu na baadhi ya watumishi wenzake kutokana na kusambaza pembejeo zilizoisha muda wa matumizi kwa wakulima.

Hatua hiyo, imechukuliwa baada ya kubainika kuwapo dawa zilizoisha muda wa matumizi ambazo ziliandaliwa kupelekwa kwa wakulima. Hadi sasa dawa za maji lita 414.5 na za unga tani 20 zinashikiliwa.

Akizungumza baada ya kutoa agizo hilo jana, Dendego alisema kitendo cha watumishi wa bodi kuhusika na ugawaji wa pembejeo hizo, kinaonyesha wazi ni mbinu chafu za kufifisha uzalishaji wa zao hilo.

Alisema Jeshi la Polisi linatakiwa kumkamata Jarufu, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Shauri Mokiwa, Mkurugenzi wa Kilimo na Ubanguaji, Luseshelo Silomba na mkurugenzi wa kampuni inayolinda ghala lililokuwa na pembejeo hizo.

Alisema udanganyifu unaofanywa na bodi hiyo ni mkubwa na unaweza kugharimu uzalishaji wa korosho msimu wa 2017/18.

“Hizi ni hujuma ambazo tunafanyiwa, hatuwezi kukaa kimya tunapoona mtu akitaka kuharibu dhahabu yetu ya kijani, kitendo cha kusambaza pembejeo zilizoisha muda wake ni kuua zao la korosho na kufifisha jitihada za Serikali kukuza uchumi utokanao na kilimo nchini.

“Inawezekanaje mtaalamu anachukua dawa zilizotengenezwa mwaka 2012 ambazo zinatakiwa kutumika kwa muda wa miaka miwili, zinasambazwa kwa wakulima msimu huu? Tunashangaa msimu huu zinapelekwa kwa wakulima zaidi ya lita 414.5 kinyume cha sheria, jambo hili limetusikitisha.

“Nilipofika niliona maboksi mapya yakiwa yamepangwa ghalani, nilipoyafungua nilibaini jina lililoandikwa juu yake ni tofauti na dawa zilizopo ndani yake,” alisema Dendego.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mkondya, alisema hadi sasa jeshi hilo linawashikilia mtunza ghala ambaye pia ni Katibu Mahsusi wa Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Felista Onestina, Mtunza Ghala Emiliana Salia na mwenzake, Husna Rajabu.

“Sisi tumepokea maagizo, nitahakikisha  mtandao wote uliofanikisha pembejeo zilizoisha muda wake kuwafikia wakulima wanakamatwa,” alisema Mkondya.

Baada ya taarifa hizo, MTANZANIA ilifika ofisi za bodi hiyo na kukutana na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Shauri Mokiwa ambaye alipoombwa kuzungumzia suala hilo, alikata katakata.

Mei, mwaka huu katika mkutano wa wadau wa zao hilo, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba,  alisisitiza kuwa bodi hiyo inapaswa kuhakikisha inakuwa makini na viuatilifu vinavyoingizwa nchini kwa kuvipima kwa kutumia wataalamu wa Serikali ili kujiridhisha ubora wake kabla ya kuwafikishia wakulima hatua ambayo itawafanya wawe salama zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles