31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MKURUGENZI JKCI AMTOLEA MANJI USHAHIDI

NA KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohammed Janabi, amepanda kizimbani kumtetea mfanyabiashara Yusufali Manji, anayekabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin. 

Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa utetezi, alitoa ushahidi wake jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kwa kuongozwa na mmoja wa mawakili wa Manji, Hajra Mungula.

Profesa Janabi, alidai mshtakiwa Manji aliwahi kulazwa katika taasisi hiyo mara mbili tofauti, Februari na Julai, mwaka huu.

Alidai alipofika hospitalini hapo Februari, mwaka huu, alitokea polisi akiwa na matatizo ya moyo.

Alidai kuwa alikuwa akisikia maumivu upande wa kushoto wa moyo na alipofikishwa hapo, alifanyiwa uchunguzi kuangalia kama vyuma vilivyopo katika moyo wake vimeziba ama la.

“Tulifanya uchunguzi kuangalia kama vyuma vilivyopo katika moyo vimeziba ama la, tuliingiza mipira mpaka katika moyo, tukaona mirija haijaziba na vyuma vinafanya kazi vizuri.

“Alipofikishwa kwa matibabu, alipewa dawa aina tatu tofauti za moyo na kabla ya hapo, alikuwa na tatizo la mgongo na kukosa usingizi, kwa tatizo hilo alikuwa akipatiwa matibabu Hospitali ya Agha Khan,” alidai.

Alidai mgonjwa wa moyo mwenye chuma katika moyo wake, kabla hajawekewa chuma hicho huelezwa vitu ambavyo hatakiwi kutumia, ikiwamo kuvuta sigara na matumizi ya dawa za kulevya, ikiwamo heroin.

Alidai matumizi ya dawa za kulevya kama heroin kwa mgonjwa huyo, yana athari kubwa kwani hufanya mirija kuziba na kusababisha kufanyiwa upasuaji mkubwa.

Shahidi huyo aliendelea kufafanua kuwa ugonjwa wa moyo una visababishi vingi na si kwa kutumia dawa za kulevya pekee.

Mkurugenzi huyo alidai alimwona Manji alipofikishwa katika taasisi hiyo na kwa kumbukumbu zilizopo katika faili, aliwahi kufanyiwa matibabu ya moyo, Florida nchini Marekani. 

Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis alipomuhoji shahidi huyo kama anajua athari za mgonjwa wa moyo kutumia dawa za kulevya, alijibu akidai yeye ni daktari wa moyo na anazijua athari. 

Shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi na Wakili Hajra aliomba kesi iahirishwe hadi leo kwa Manji kujiteea. 

Manji alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 16, mwaka huu akidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9 katika eneo la Upanga Sea View, Ilala, alitumia dawa za kulevya aina ya heroin. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles