NA HARRIETH MANDARI-GEITA
MBUNGE wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM) na watuhumiwa wenzake wanane, jana walikwama polisi, baada ya kushindwa kufikishwa mahakamani kama ambavyo ilitarajiwa.
Musukuma ambaye alitakiwa kufikishwa mahakamni pamoja na madiwani, ameshindwa kufikishwa mahakamani kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayomkabili ya uhujumu uchumi wa miundombinu ya barabara na maji mkoani Geita kutokana na Mahakama ya Wilaya ya Geita kudai muda wa kazi umemalizika.
Akizungumza nje ya mahakama hiyo, baada ya kutaarifiwa juu ya suala hilo, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Adam Ngalawa alisema wadhamini wa mtuhumiwa Musukuma na wenzake wanane ambao ni madiwani kutoka kata mbalimbali za halmashauri ya mji na wilaya, walikuwa wamekamilisha taratibu za kuwadhamini.
“Tumekuwa tukisubiri Musukuma na madiwani waletwe ili tuwadhamini, taarifa tuliyopata ni kwamba muda wa kazi umemalizika… mahakama haiwezi kuendelea kuwasubiri kwa ajili ya kuwasomea mashtaka watuhumiwa hadi kesho (leo),” alisema Ngalawa.
Baada ya taarifa kusambaa mjini hapa, mamia ya wakazi wakiwamo wafanyabiashara wakubwa na wadogo na viongozi mbalimbali wa CCM walifika mahakamani hapo wakiwa na shauku ya kuwaona watuhumiwa.
Mmoja wa wananchi waliokuwa kwenye mkusanyiko huo Ikongolo Oto, ambaye ni Katibu wa Chama cha ACT Wazalendo Mkoa wa Geita, alilitaka Jeshi la Magereza kuondoa urasimu usio na tija wa kuchelewesha watuhumiwa kupelekwa mahakamani.
“Suala la dhamana ni haki ya kila mtu hivyo ni vyema wahusika wa magereza kuwaleta madiwani na mbunge ili wasomewe mashitaka waliyotuhumiwa na siyo kuwakalisha tu ndani kwani nao wana haki ya kupata dhamana.”alisema.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Ally Rajabu na madiwani sita walikamatwa na kuwekwa rumande, baada ya kudaiwa kuhusika na kuharibu miundombinu ya barabara na kukata bomba kubwa linalosambaza maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Geita mjini, ikiwa ni njia ya kushinikiza walipwe malimbikizo ya deni la kodi ya huduma Dola za Marekani milioni 12 kati ya mwaka 204 hadi 2013.