24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

MBUNGE CCM AHAMASISHA MICHANGO MATIBABU YA LISSU

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu (CCM), amejitokeza hadharani kuhamasisha wananchi wa Singida na Watanzania, kutoa michango ili kugharimia matibabu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).

Lissu ambaye alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka huu mjini Dodoma, yupo Nairobi nchini Kenya akipatiwa matibabu zaidi.

Katika andiko lake kwenye ukurasa wake wa Facebook, Nyalandu alisema. “Mazungumzo yanayoendelea na madaktari bingwa na hospitali mahiri kote duniani yafanikiwe upesi kumwezesha Mh. Lissu kuifikia huduma bora ya matibbu iliyopo kwa sasa ulimwenguni. Iwe heri kwake,” alisema.

Maelezo hayo yalionesha kuwa kuna mipango zaidi ya kumpeleka Lissu kwenye hospitali nje ya Afrika Mashariki, ingawa gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na viongozi wa Chadema walioko Nairobi ili kuthibitisha mpango huo  lakini hawakupatikana.

Kwa siku za hivi karibuni Nyalandu alijipatia sifa za kipekee baada ya kuwapeleka Marekani kwenye matibabu watoto watatu ambao walikuwa wanafunzi wa shule ya Luck Vincent ya Arusha, walionusurika kwenye ajali ya barabarani ambayo ilisababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wao wawili na dereva.

Pia Nyalandu amekuwa Mbunge pekee wa CCM aliyeenda Nairobi kumjulia hali Lissu, anayedaiwa kupigwa risasi nane kati ya 30 zilizomiminwa kwenye gari lake.

Katika andiko lake la jana, Nyalandu alisema.  “Tunawaomba wana Singida na Watanzania wote tuendelee kuchangia gharama za matibabu ya Tundu Lissu. Sote tumkumbuke katika sala na dua zetu katika majira na saa hii ya kujaribiwa kwake.

“Mungu akisema ndio, hakuna awezaye kupinga. Kwa  wote wanaohusika moja kwa moja kumtibu na kumtunza, mikono yao na fahamu zao zikahuishwe katika ubora wote wa utabibu na matunzo,” alisema.

Mbali na Nyalandu, Mbunge mwingine aliyeenda Nairobi kumjulia hali Lissu ni Zitto Kabwe, anayetoka chama cha ACT-Wazalendo.

Fulana za ‘Pray For Lissu’

Katika hatua nyingine mwandishi wetu JOHANES RESPICHIUS anaripoti kuwa, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Lazaro Mambosasa, amesema polisi haijawakamata watu wanaovaa fulana zenye maandishi ya ‘Pray For Lissu’ na kwamba watu waliokamatwa juzi ni wale waliohisiwa kutaka kuandamana isivyo halali.

Akizungumza na MTAZANIA kwa simu jana, Kamishna Mambosasa, alisema wakati askari wakifanya operesheni ya kuzuia maandamano, walipita katika ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na watu walipoiona gari la polisi, walianza kukimbia.

“Askari baada ya kuona watu wameanza kukimbia, waliamua kuwakimbiza kwani walihisi lengo lao lilikuwa ni kuandamana, hivyo waliwakamata vijana watatu na mpaka ninavyoongea leo (jana) tayari wameachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kila mara kituoni.

“Jeshi la Polisi halijamkamata mtu kwa kuvaa ‘T-shirt’ (fulana) hizo, bali lilikuwa linakamata watu ambao nia yao ilikuwa ni kuandamana siku ya Jumapili… yaani hapo hata kama ungelikutwa umevaa dera au kanzu unataka kuandamana ungelikamatwa,” alisema Kamishna Mambosasa.

Kuhusu tuhuma kwamba polisi walivamia na kuchukua  baadhi ya vifaa vya Chadema katika maduka yaliyopo karibu na ofisi za chama hicho Kinondoni, Kamishna Mambosasa alisema madai hayo hayana ukweli wowote.

Septemba 17, mwaka huu baadhi ya wafuasi wa Chadema na viongozi wa dini, walipanga kufanya maombi kumwombea Lissu.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilipiga marufuku maombi hayo likidai mkusanyiko huo unaweza kuhatarisha amani na kuwataka waandaaji kufanya maombi hayo makanisani na misikitini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles