23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MSONGO WA MAWAZO KAZINI (OCCUPATIONAL STRESS)

 

NA DK. CHRIS MAUKI,

HUU ni msongo wa mawazo kwa watu walio kazini. Kwa kawaida, humpata mtu kutokana na mazingira ya kazi, uzito wa kazi yenyewe, uwezo wa mtu kuimudu kazi yenyewe n.k.

Mambo haya kwa ujumla humtengenezea mtu aliyeajiriwa mazingira ya kupata msongo wa mawazo, mambo mengine yanayochangia msongo wa mawazo kwa watu walio makazini ni pamoja na nafasi ya mwajiriwa katika ofisi au katika ofisi aliyoko, uhusiano kati ya waajiriwa ndani ya ofisi na muundo na mwelekeo wa ofisi kiutendaji.

Kwa kawaida, msongo ukiwa juu sana au chini sana husababisha matatizo kwa mtu aliyeajiriwa, lakini hasa husababisha magonjwa na madhaifu mengine ya mwili.

Msongo  wa mawazo waweza kuwa chini sana hutokana na mwajiriwa kudhani kuwa kazi yake au nafasi yake ya kazi sio ya muhimu na kwa hiyo anaweza kuachishwa kazi na nafasi yake kujazwa na mtu mwingine wakati wowote.

Pia msongo kuwa juu sana hutokana na majukumu kuwa mengi, ya kuchosha na wakati mwingine chini ya usimamizi mkali kuhakikisha makosa hayatokei. Kwa hali zote mbili, mwajiriwa anakuwa katika mazingira ya kupata msongo wa mawazo ambao waweza kumsababishia madhaifu na hata magonjwa.

Vyanzo vya msongo wa mawazo kwa waajiriwa (stressors), huwa katika makundi mawili. Vile vinavyotokana na mtu mwenyewe, yaani ndani ya mtu (internal stressors), ambavyo hujumuishwa pamoja na mambo mengine ndani ya tabia ya mtu. Uwezo wa mtu wa kuchukuliana na majukumu mazito, kujiamini kwa mtu na pia wasiwasi mtu alio nao kwa kazi anayoifanya.

Vyanzo vingine ni vile vinavyotoka nje ya mtu (external stressors). Hivi hujumuisha mambo yanayotokea nje ya eneo la kazi na nje ya tabia au uwezo wa mtu binafsi. Mambo kama matatizo ya kifamilia, magumu ya maisha, matatizo ya kiuchumi na mazingira. Kwa pamoja, vyanzo hivi hupelekea dalili za matatizo ya kiafya kwa walio makazini, ambazo huweza kukua na kufikia  kuwa ugonjwa kamili uliokomaa.

Hata hivyo, vyanzo hivi vya msongo wa mawazo kwa walio makazini hutofautiana kutoka mtu na mtu, tofauti ya maeneo ya kazi na kazi zenyewe, pamoja na ukweli kwamba maisha ya watu pia hayafanani kati ya mtu na mtu, na hujumuisha tofauti kwa mfano katika matatizo ya kifamilia pamoja na sababu zake, nafasi za kiuchumi (financial opportunities) pamoja na matatizo ya kiuchumi yametofautiana na hivyo kufanya tofauti katika aina na madhara anayoweza kuyapata mfanyakazi kutokana na msongo wa mawazo.

 Tukiangalia kwa undani msongo wa mawazo kazini waweza kuwa katika mtiririko ufuatao.

Msongo unatokana na kazi yenyewe

Huu ni msongo wa mawazo unaosababishwa na kazi anayofanya mtu, kwa mfano, mazingira magumu ya kazi ambayo si mazuri, kazi kuwa nyingi kupita uwezo wa mtu, ufinyu wa muda wakati kazi ni nyingi pamoja na hatari zinazohusiana na kazi yenyewe.

Mfano kwa wanaofanya kazi na hasa za mikono kwenye viwanda au maeneo mengine ambapo huwa katika hatari ya kuumia au hata kufa.

Msongo unaotokana na nafasi ya mtu kazini.

Huu ni msongo wa mawazo anaopata mfanyakazi kutokana na ugumu wa nafasi ya kazi pamoja na majukumu yake, mgongano wa majukumu katika nafasi ya kazi, pamoja na ugumu wa wajibu wa mfanyakazi kwa ofisi pamoja na wateja au wapewa huduma wa ofisi.

 Wakati mwingine, hutokea mfanyakazi anapopandishwa daraja kazini (promotion), na kukuta majukumu yamezidi au mfanyakazi anapokuwa katika nafasi fulani ya kazi kwa muda mrefu, wakati wafanyakazi wengine walioajiriwa nyuma yake wakipandishwa madaraja kazini na yeye kubaki palepale.

 Hii ni kutokana na ukweli kuwa, kupandishwa daraja kazini inamaanisha kuwa kazi ya mtu imekubalika na kuridhisha, na pia hali ya mfanyakazi kiuchumi inategemewa kubadilika na kuwa nzuri zaidi. Kwahiyo, kinyume cha hayo, huleta msongo wa mawazo kwa waajiriwa na wafanyakazi wengine kwa ujumla.

Msongo unaotokana na mahusiano kazini

Huu nao ni msongo wa mawazo unaowapata walio kazini unaosababishwa na mahusiano kati ya wafanyakazi katika ofisi hasa mwajiriwa anapokuwa hana uhusiano mzuri na mkuu wake wa kazi au walio chini yake au na wafanyakazi wenzake kwa ujumla.

Mara nyingine, ugumu hutokea wakati wa kugawana majukumu ya kazi ambapo wengine huona wameonewa kwa kupewa kazi nyingi au majukumu yenyewe kutotekelezwa kikamilifu au kwa ufanisi.

 Hali hii humpa aliyepewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo wakati mgumu wa kujibu kwa walio juu yake.

Msongo unaotokana na muundo na mwelekeo wa ofisi

Hutokea wakati mfanyakazi anapokuwa hana kabisa au kuwa na ushiriki mdogo katika maamuzi ya ofisi, na hasa yanayomhusu, wakati mfanyakazi anapozuiwa kufanya kazi zake kwa uhuru, na hasa anapofuatiliwa katika kila jambo analofanya, au kunapokuwa hakuna ushauri (consultation) ya kutosha kuhusu kazi za kila siku.

Kwa ujumla, mambo hayo yote yaliyotajwa hapo juu hupelekea mfanyakazi kuwa na wasiwasi kazini, kutojiamini na kushindwa kuvumilia magumu ya kazi, ambapo kwa pamoja huwa na dalili kama mapigo ya moyo kuongezeka, kuongezeka kwa kolestro mwilini, uvutaji wa sigara uliozidi, kuwa mpweke, ulevi wa “kupunguza” mawazo, kutofurahia kazi na kupungua kwa msisimko wa kazi.

 Mfanyakazi kama huyu mara nyingi hupenda kuzungumzia hamu yake ya kuacha kazi na kujiunga na kampuni au ofisi nyingine. Dalili hizi zisiposhughulikiwa mapema husababisha magonjwa kama magonjwa ya moyo na magonjwa ya akili.

Ni kawaida mfanyakazi na hasa mwajiriwa kuwa na maswali ambayo mara nyingi hukosa majibu na kupelekea msongo wa mawazo.

Maswali hayo ni kama; ni mara ngapi huwa mwajiriwa anajisikia hana, au hajui uzito na umuhimu wa majukumu yanayoandamana na kazi yake, wakati mwingine mwajiriwa hujifikiria kama asiye na vigezo vya kutosha kwa kazi aliyo nayo, au wakati mwingine hukosa taarifa anayoihitaji ili kazi yake ifanikiwe.

Wakati mwingine hana uhakika mkuu wake wa kazi anamfikiriaje, kwamba anafurahia kazi yake au la, au kutokuwa na ujasiri katika maamuzi mazito yanayoihusu na kuigusa jamii iliyomzunguka.

Pia ni kawaida mwajiriwa kuwa na wasiwasi kwa jinsi wafanyakazi wenzake wanavyomchukulia, mathalani, wanampenda au wanamchukia? Na pia humpa wakati mgumu mwajiriwa kufikiri kuhusu yale watu waliomzunguka wanayotegemea kutoka kwake.

 

Njia pekee ya kuzuia aina hii ya msongo wa mawazo ni kwa kupunguza uzito wa vyanzo vyake katika kazi, kuwa makini na tabia za mtu ili zisijemletea msongo wa mawazo, lakini pia kuwa mwangalifu na yale yanayoweza kumsumbua mtu lakini hayahusiani na kazi moja kwa moja kama matatizo ya kifamilia au ya kiuchumi.

 Kwa wale ambao kazi zao ni nyingi kupita uwezo wao, wanapaswa ama kugawa majukumu kwa wengine au kuwa na siku fulani za kupumzika na kuwa na familia zao.

Hilo husaidia akili ya mfanyakazi kupata muda wa kupumzika na hivyo kupunguza uwezekano wa kupata msongo wa mawazo.

Imebainika kuwa, waajiriwa wengi, hasa vijana wenye umri kati ya miaka 20 na 30 na tisa wangependa kufanya kazi zinazotoa muda wa kutosha kwa wao kuwa na familia zao kuliko kazi ngumu au kazi zenye mshahara mkubwa inazowanyima muda wa kuwa na familia zao.

Maofisi mengine hutoa likizo fupifupi za mara kwa mara kwa wafanyakazi wake ili kuwapunguzia mawazo kuhusu watoto.

 Hii inamfanya mwajiriwa kuwa kazini kila anapohitajika kutokana na ukweli kuwa ana uhakika na hali za wanae na familia yake kwa ujumla kuwa wako salama.

Maofisi mengine hata yameanzisha shule kwa ajili ya watoto wa wafanyakazi wao, lengo likiwa kupunguza msongo wa mawazo kwa wafanyakazi wazazi wanaopata kutokana na kujali maslahi ya watoto na familia zao kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles