30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JOKATE AIVURUGA UVCCM

*Uteuzi wake wapingwa, viongozi wagawanyika


Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

UTEUZI wa Miss Tanzania namba mbili wa mwaka 2006, Jokate Mwegelo kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, unaonekana kutaka kuivuruga jumuiya hiyo.

Mjadala mkubwa umeibuka kuhusu uteuzi huo, ambapo baadhi ya wanachama na viongozi wa juu wa jumuiya hiyo wamedai kuwa haukufuata kanuni na taratibu za umoja huo.

Vyanzo vya kuaminika kutoka katika umoja huo vimeliambia MTANZANIA kuwa baadhi ya viongozi wa juu wa UVCCM hawakushirikishwa katika uteuzi huo uliofanywa na kigogo mmoja wa umoja huo.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa uteuzi huo haukushirikisha wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji wala Baraza Kuu la UVCCM, ambalo halikukutana kumthibitisha Jokate kama kanuni zinavyoelekeza.

Kwa mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo, wajumbe wa kamati ya utekelezaji hawazidi 10, ambapo miongoni mwao ni Mwenyekiti wa umoja huo Taifa, Makamu Mwenyekiti Taifa, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na mjumbe mmoja kutoka makao makuu ya chama.

Wajumbe wa baraza kuu ni wenyeviti na makatibu wa mikoa na mjumbe mmoja kutoka katika kila mkoa.

SHAKA ATOA NENO

Kutokana na kile kilichodaiwa kuwa ni mvurugano ndani ya umoja huo, MTANZANIA lilimtafuta Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka,  ambaye alikiri Jokate kuteuliwa kukaimu nafasi hiyo na kusema kuwa uteuzi huo ulifuata taratibu zote za chama.

“Ni kweli amekaimishwa kwa kufuata taratibu zote za chama, kikao cha Kamati ya Utekelezaji kilikutana Aprili 18, mwaka huu, Dar es Salaam na ndicho kimewakaimisha wakuu wa idara watano akiwamo Jokate.

“Hao wanaolalamika hawajui kanuni na taratibu za jumuiya yetu, huwezi kupata nafasi kama kikao cha Kamati ya Utekelezaji hakijakaa,” alisema Shaka.

Hata hivyo alikiri kutoitishwa kwa kikao cha Baraza Kuu ili kuthibitisha uteuzi huo, akisema ni gharama kubwa kuitisha kikao hicho.

“Kwa kawaida Baraza Kuu huwa linakutana kila baada ya mwaka mmoja, kuita baraza kuu ni gharama sana hivyo ikitokea kuna nafasi wazi Kamati ya Utekelezaji ina mamlaka pia ya kumthibitisha,” alisema.

JOKATE AZUNGUMZA

Akizungumza na MTANZANIA, Jokate alishukuru kwa uteuzi huo na kuahidi kuifanya jumuiya hiyo iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania.

“Nashukuru kwa imani waliyoonyesha viongozi wangu ila zaidi kuona nina uwezo wa kuongoza idara hiyo nyeti na muhimu kwenye jumuiya.

“Kikubwa ni kuifanya jumuiya iwe karibu zaidi na vijana wa Kitanzania na kurudisha tumaini na kusimamia changamoto wanazozikabili vijana katika kujiletea maendeleo,” alisema Jokate.

Jokate pia alikuwa miongozi mwa wanachama 450 wa CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Jokate alianzia kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006 ambapo aliibuka mshindi wa pili.

Hivi sasa anajishughulisha na sanaa na ujasiriamali ambapo anamiliki Lebo ya Kidoti Fashion inayojihusisha na uuzaji wa nywele na mavazi.

MADAI YA MALIMBIKIZO

Katika hatua nyingine, baadhi ya watumishi wa jumuiya hiyo wamelalamikia madai ya malimbikizo ya uhamisho na likizo.

Miongoni mwa watumishi hao wamo makatibu wa wilaya na mikoa ambao wamekuwa wakihamishwa vituo vya kazi bila kulipwa stahiki zao.

Wakizungumza kwa sharti la kutotajwa majina gazetini, watumishi hao walisema wana hali ngumu kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa muda mrefu, hali inayotishia utendaji wao.

Katibu mmoja wa wilaya ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema anadai malimbikizo ya zaidi ya Sh milioni 20 kutoka mwaka 2010 tangu alipoanza kuhamishwa vituo mbalimbali vya kazi.

Mtumishi alisema hatua hiyo ni kinyume na maazimio ya Mkutano Mkuu wa UVCCM wa nane uliofanyika Oktoba 2012 mkoani Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine uliazimia kulipa malimbikizo ya madeni ya watumishi wake wote yanayohusu gharama za uhamisho, posho ya likizo, matibabu na nyingine.

“Malimbikizo ni mengi mimi nadai zaidi ya Sh milioni 20, wapo wanadai milioni 30 na wengine hadi milioni 50, unapewa barua ya uhamisho bila kulipwa stahiki zako, huko unapoenda utaishi vipi?

“Watumishi wanajiingiza kwenye mikopo ili kupata fedha za kujikimu na wengine wanakua ombaomba, tena ukikuta mtumishi kama ni mwanamke anaambiwa nenda kule utamwona kamanda, hiyo ni sawa na kumuuza huyu mtumishi,” alisema.

Alipouliwa Kaimu Katibu Mkuu UVCCM, Shaka alisema malimbikizo hayo ya watumishi yanalipwa kadiri fedha zinavyopatikana.

“Hii ni taasisi ya chama ina taratibu zake, kuna utaratibu mzuri na malimbikizo yote yanalipwa kutokana na hali ya kifedha iliyopo…hivyo ni vitu vya kawaida hata serikalini mfumo huo upo.

“Kama sasa hivi tunakabiliana na chaguzi mbalimbali, tunapunguza malimbikizo lakini wakati huo huo tunajiandaa na uchaguzi,” alisema Shaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles