29.3 C
Dar es Salaam
Saturday, May 28, 2022

MFUNDISHE MTOTO HESHIMA AKIWA MDOGO

 

 

NA AZIZA MASOUD,

WASWAHILI husema samaki mkunje angali mbichi, huo ni msamiati wa Kiswahili wenye maana kubwa sana katika maisha yetu ya kila siku.

Maana ya msemo huo ni kwamba, kuna vitu ambavyo unapaswa kuvifanya ama kuvitengeneza mwenyewe wakati kikiwa bado hakijaonyesha ishara ya kuleta tatizo  kuelekea kutengeneza tatizo.

Hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa kwa watoto,   kikawaida kuna vitu ambavyo unapaswa kumfundishwa kabla hajakuwa mtu mzima.

Pia vipo vitu ambavyo anaweza akawa anajifunza taratibu kulingana na umri, lakini suala la kuwa na tabia nzuri linapaswa kuangaliwa kabla hajaanza kujitambua.

Wapo wazazi ambao watoto wao wanaanza kuonyesha wazi tabia ndogondogo utotoni ambazo hazina mwelekeo mzuri, lakini wanashindwa kuwarekebisha.

Kuna vitu wanafanya watoto ambavyo vinaashiria wazi kuwa hawatakuwa na tabia nzuri baadaye, lakini kwa sababu hatuwafuatilii tunajikuta mtoto anakuwa na tabia mbaya atakapokuwa mkubwa bila kujua chanzo chake ni nini.

Mfano akiwa mdogo hasa anapoanza kuongea, mara nyingi huanza kujifunza kuita wazazi, mfano baba na mama, lakini pia anapaswa kufahamu namna ya kusalimia anapoona watu wazima.

Endapo utashindwa kumtengenezea ama kumfundisha mtoto kuanza kuwasalimia hata nyinyi wazazi, ni wazi kuwa hataweza kufanya hivyo hata atakapokuwa mtu mzima.

Wapo wazazi ambao mtoto anaamka haamkii wala hamuelekezi kufanya hivyo, akidhani kwamba ni akili ya utoto, bila kujali kuwa tabia ile itakomaa mpaka anapokuwa mkubwa.

Hali hiyo wazazi huona kama masihara, bila kujali kuwa kuna vitu katika kumjenga  mtoto havihitaji kudharauliwa, mtoto unapaswa kumjengea tabia ya kusalimia watu wazima anapoamka asubuhi kama anaweza kuongea.

Siyo mtoto anaamka anawaambia wazazi ‘mambo’ ama ‘habari zenu’ mnamuangalia bila kumkemea, ipo siku atakuja kuwasalimia wageni kwa utaratibu huo muanze kuona aibu.

Mbali na hilo, wapo watoto wenye tabia ya kujibizana na kuwatolea maneno machafu wenzao, nayo si nzuri, unapomuona mtoto wako ana viashiria vya tabia hiyo unapaswa kumuonya ili asirudie na ikiwezekana umtolee ukali ili ajue kitu alichokifanya si kizuri.

Wazazi wanapaswa kutambua kuwa mtoto anaelekezwa anapokuwa mdogo na inakuwa rahisi kumbadilisha, kwa sababu ubongo wake unakuwa bado haujaanza kushika vitu vingi.

Hakuna mtoto ambaye anazaliwa akiwa na tabia nzuri, isipokuwa wote wanaelekezwa na ndiyo njia pekee ya kumjenga katika maisha ya baadaye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,631FollowersFollow
542,000SubscribersSubscribe

Latest Articles