24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Msigwa atangaza kuanza mikutano ya hadhara

Raymond Minja -Iringa

MWENYEKITI wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa, amewataka viongozi wa kanda hiyo kuanza mikutano ya hadhara kwani muda aliotoa Rais Dk. John Magufuli umefika.

Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini, alitoa kauli hiyo juzi, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, Uwanja wa Mwembetongwa mjini hapa.

Alisema kuwa Rais Magufuli alitangaza mikutano ianze kufanyika kuanzia mwaka 2020 na sasa umefika, hivyo ni lazima kiongozi afanye hivyo katika eneo lake.

“Mimi kama mwenyekiti wenu wa Kanda ya Nyasa, natangaza rasmi kuanzia leo (juzi) kuanza rasmi mikutano ya hadhara kwa kuwa muda umewadia ila mfuate taratibu, sio kwenda kufanya fujo na tumejipanga kwelikweli na lazima kieleweke, mwaka 2020 hatuendelei kulalamika, bali ni muda wa kwenda kushika dola,” alisema Msigwa.

Alisema kuwa uchaguzi uliopita wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana ulivurugwa kwa makusudi, lakini kwa sasa wamejipanga kuhakikisha uchaguzi wa mwaka huu wanakwenda kushinda na kuwa na mikakati ya kulinda kura.

“Tuliambiwa tuache siasa na tusubiri mwaka 2020 ndiyo tuanze siasa, sasa muda umewadia, ni kufanya siasa kwa kwenda mbele, hakuna kulala mpaka kieleweke au makamanda tuliamshe dude mpaka Ikulu,” alisema Msigwa.

Pamoja na hayo, alishauri Serikali ibadili mitaala ya elimu nchini ili wasomi wanapomaliza elimu yao waache kuzunguka mitaani na vyeti bali mitaala hiyo iwe na jibu kuhusu hali hiyo.

Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la wasomi ambao wanakosa ajira na kuishi mitaani jambo ambalo huwaathiri kisaikolojia.

Akizungumza sekta ya kilimo, alisema imeajiri asilimia 70 ya Watanzania, lakini amedai kwa sasa hali imekuwa mbaya kwa wakulima ambao wengi wametelekezwa kuliko awamu zilizopita.

Hata hivyo wakati akieleza hayo kuhusu sekta ya kilimo, hivi karibuni Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alisema kuwa kwa sasa Serikali imekuwa ikiweka mazingira wezeshi kwa wakulima kwa kuhakikisha wanakuwa na pembejeo za kilimo na kuwatafutia masoko ya uhakika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles