25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MSIBA WA WATOTO WETU 33 IWE CHACHU YA NDOTO YA TAIFA

NA FREDERICK FUSSI,

TAIFA limepoteza watoto 32, dereva wao na walimu wao wawili wakati wakiwa njiani kwenda kufanya mitihani kwa kujipima uwezo wa kimasomo na wanafunzi wenzao huko Karatu. Watoto wetu hawa wamepoteza uhai wakati wakiendelea na ndoto yao ya kusaka elimu bora kwa ajili ya mustakabali wa maisha yao ya baadaye. Elimu ni ndoto kubwa sana ya mabadiliko na ndio silaha itakayotumika kuzima ujinga uliolighubika Taifa letu. 

Ujinga ni hali ya kutojua mambo. Pengine unapokwenda shule si tu kujua kusoma na kuandika ndiko kunasaidia kuondoa ujinga bali hata maisha ya jumla ya shuleni husaidia kuondoa baadhi ya ujinga. Japokuwa kuna ujinga wa kiwango fulani huwezi kuondolewa kwa kwenda shule pekee, bado elimu ndio inabakia kuwa njia kuu ya kusaidia kuondoa ujinga katika Taifa.  Kukaa katika maendeleo duni nako ni ujinga wa waliosoma kushindwa kutafuta suluhu za pamoja za kuharakisha juhudi za kuondokana na umasikini wa kipato kwa Taifa letu.

Bado tuna safari ndefu kama Taifa ya kuondokana na ujinga. Ujinga mwingine ni kitendo cha kudhani kuwa itikadi na mrengo wa kisiasa unaouamini wewe ndio upo sahihi sana kuzidi ule wa wenzako wasiofanana mawazo wala mtazamo kama ule wa kwako. Wakati tunaendelea kutafakari kwa kina njia za kitaifa zitakazotusaidia kupunguza ajali za barabarani, sharti pia tuanze kuwaza njia bora zaidi za kupunguza ujinga dhidi ya majigambo na tambo za itikadi za kisiasa na kupata uelewa kuwa Taifa letu ni moja na sharti tulijenge wote kwa pamoja, upendo, furaha na amani.

Msiba huu wa watoto wetu 32 ni msiba ambao umelileta Taifa pamoja katika maombolezo. Kama ambavyo msiba huu umetuleta pamoja bila kujali tofauti za kiitikadi miongoni mwetu ndivyo ambavyo tunapaswa daima kuendelea kuwa na umoja huo katika kulijenga Taifa. Kama ambavyo msiba huu ni wa kitaifa na umetuleta Watanzania wote pamoja ndivyo ambavyo masuala mengine ya Kitaifa yanapojadiliwa ili kutafutiwa ufumbuzi wa pamoja yasizuiwe na itikadi zetu za vyama vya siasa.

Mathalani, watoto wetu hawa wanapaswa kufanyika kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya mfumo wetu wa elimu hapa nchini. Watoto wetu hawa walifariki wakiwa katika hatua za kusaka ndoto kubwa ya Taifa hili. Kama ambavyo watoto wetu walifariki dunia wakiwa wanaisaka ndoto kubwa ya Taifa hili, Je, si zaidi kwetu sisi waombolezaji kuwaenzi kwa kuisaka ndoto Kubwa ya Taifa letu?

Ndoto kubwa ya Taifa letu ndio iwe msingi imara wa kuheshimiana pasipo kujali tofauti zetu za viwango vya kufikiri na kupambanua mambo katika masuala mbalimbali ya kitaifa. Kama ambavyo tumekutanishwa pamoja katika msiba huu, ndivyo ambavyo ndoto kubwa ya kuwa na Taifa imara, Taifa bora lenye maendeleo ya watu na si vitu, Taifa bora linalojali hali za watu wake mmoja mmoja ndio ndoto kubwa ambayo kila mfanyakazi, mwanasiasa, mkulima, mfanyabiashara na watu wote nchini huitafuta!

Tunapowasindikiza watoto wetu katika nyumba zao za milele makaburini, lazima huko nyuma sisi tunaobaki tubakie wamoja kwa umoja wetu wa kitaifa, watu wenye upendo na amani tunaoisaka kwa pamoja ndoto kubwa ya Tanzania bora iliyosheheni maisha bora kwa kila mmoja wetu. Ndoto kubwa ni pamoja na kukubaliana kuwa kila mwenye mawazo na maoni katika Taifa hili anapaswa kuheshimiwa ndani ya Bunge, nje ya Bunge, ndani na nje ya Serikali.

Lazima tuamini kuwa maoni na mawazo ya kila Mtanzania kusudi lake si kuibomoa nchi yetu bali ni kuifanya kuwa nchi ya furaha, utu, upendo na amani. Ikiwapo sababu ya kulifanya Taifa letu lifurahie basi iwe ni ndoto Kubwa ya kitaifa ambayo imemwagiwa maji ya ustawi kutokana na vifo vya watoto wetu waliofariki wakiisaka ndoto kubwa ya Taifa letu. Kila Mtanzania leo, anastahili kuishi maisha mazuri kuelekea ilipo ndoto kubwa ya Taifa letu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles