23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

HIKI NDIO CHANZO CHA WATANZANIA WANAOFANYA KAZI OMAN KUPATA MATATIZO

Balozi wa Tanzania Oman, Abdallah Kilima

 

 

Na MWANDISHI WETU, OMAN

KWA siku za karibuni kumekuwapo na taarifa zenye mkanganyiko juu ya Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nchini Oman hususani kazi za majumbani na baadaye kupatwa na majanga yakiwamo kuteswa, kudhalilishwa utu wao na hatimaye baadhi yao kusababisha vifo.

Baada ya kuwapo taarifa hizi, gazeti hili liliwasilina na Balozi wa Tanzania nchini Oman, Balozi, Abdallah Kilima ambaye alituma taarifa ifuatayo kwa gazeti hili ikiwa ni hatua za utekelezaji wa ubalozi kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje katika kulinda na kuboresha maslahi ya Watanzania wanaokwenda kufanya akzi Oman na nchi zingine za Mashariki ya Kati Ubalozi wa Tanzania nchini Oman, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini Tanzania  Machi 2011, ulianza utekelezaji wa hatua kadhaa zilizokuwa na lengo la kuboresha mazingira ya kazi na kulinda haki za Watanzania wanaokuja kufanya kazi nchini Oman. 

Hatua hizi zilichukuliwa kufuatia kuwapo kwa matatizo na changamoto nyingi zinazowakabili Watanzania wanaofanya kazi Oman na hasa watumishi wa nyumbani, matatizo haya ni kulipwa mshahara mdogo, kutolipwa mshahara, kazi nyingi zisizokuwa na mpangilio,kazi za kada tofauti kuchanganywa na kuwa kazi moja ya housemaid , kufanyishwa kazi zaidi ya nyumba moja au kupikishwa vyakula vya oda za biashara, kutokuwa na mapumziko, kutowekewa bima , Kunyanyaswa kijinsia na kutokuwa na mkataba wa kazi baina ya mwajiri na mtumishi.

Hatua hizi kwa kiasi kikubwa zililenga kulinda na kutetea haki za watumishi wa majumbani  “House Maids” na hatimaye kuondoa matatizo yanayowakabili

Katika utekelezaji wa zoezi zima maslahi ya  watumishi wengine kama vile wapishi, watumishi wa saluni, madereva na wengineo pia zilizingatiwa

Hatua hizi zilizingatia matakwa ya sheria za kazi za Oman, sheria za kazi za Tanzania na zile za kimataifa. 

Hatua zinazochukuliwa kulinda haki za Watanzania walioajiriwa Oman Ubalozi unaendelea na  utaratibu wa kuratibu zoezi zima la Watanzania kwenda kufanya kazi  Oman hasa katika kada za watumishi wa nyumbani (House Maids).

Kwa utaratibu huu yeyote anayetaka kuleta mfanyakazi kutoka Tanzania anatakiwa kusoma na kuelewa mwongozo wa kuajiri Mtanzania, baada ya kusoma na kukubaliana na mwongozo anatakiwa  kujaza fomu ya kuomba kumuajiri Mtanzania na kuiwasilisha ubalozini.

Ubalozi utapitia fomu ya maombi na baada ya kuridhika nayo ubalozi utaipitisha, na kumpa mkataba, ambayo kwa ajili ya utambuzi tumeiita fomu ya ajira namba TZM/EF001 kwa watumishi wa majumbani au namba TZM/EF002 kwa ajili ya kada zingine kama madereva, wapishi, wahudumu wa saluni, migahawa na mafundi magari, mwajiri ataukamilisha na kuurudisha Ubalozini kwa ajili ya kupitishwa, katika kupitisha fomu ya maombi ubalozi unazingatia suala la umri usiwe chini ya miaka 21 na pia kima cha chini cha mshahara kiwe a Rial 80 ( kama 430,000)kwa wale wanaoanza na rial 100 ( kama shilingi 540,000 ) au zaidi kwa wale wenye uzowefu, kuwa na taarifa sahihi za mwajiri ikiwa ni anuani ya makazi, maelezo ya mwajiri kama ni mwajiriwa nk.

Mkataba huu upo katika lugha tatu, Kiswahili, Kiingereza na Kiaranu na una sehemu kuu 5, taarifa za mwajiri, taarifa za mwajiriwa, mshahara wa mwajiriwa, kazi za mwajiriwa, masharti ya mkataba, maelezo ya wakala wa ajira wa Oman na Tanzania na sehemu ya kuthibitishwa na Ubalozi  ( Kiambatanisho Na. 1) 

Baada ya fomu ya mkataba kupitishwa mwajiri atatakiwa kujaza fomu ya kiapo (affidavit) ambayo ina masharti kadhaa ambayo atapaswa atayatekeleza kwa dhati ya moyo wake ( Kiambatanisho Na. 2)

Mwajiri kupitia Wakala wa Ajira ( recruitment Agency ) baada ya kukamilisha kujaza kwa kuchapisha fomu husika anatakiwa kuirudisha Ubalozini kwa ajili ya kuthibitishwa ambapo atatakiwa kulipa rial kumi ( sawa na shilingi 54,000 ) kama ada ya uhakiki na rial 100 ( sawa na shilingi 540,000) kama dhamana.

Kiasi hiki cha dhamana kimewekwa ili kuwalazimisha waajiri kuwaleta Ubalozini kujiandikisha na kupewa ushauri nasaha  watumishi hawa mara wanapowasili Oman kuja kuanza kazi na pia kuhakikisha wame katiwa bima na kufungulia akaunti ya benki na pia taratibu zote za uhamiaji zimekamilishwa.

Baada ya kupitishwa na ubalozi, mwajiri kupitia wakala wa ajira ( recruitment Agency ) atatakiwa kuituma fomu original na si nakala kwa mwajiriwa kupitia wakala wa ajira ( recruitment Agency ) ili na yeye aweze kuisoma na kuielewa, baada ya kusoma na kuielewa, mwajiriwa atatakiwa kusaini sehemu yake na kisha kupitia wakala wa ajira ( recruitment Agency ) kuipeleka Wakala wa huduma za Ajira – TAESA (Tanzania Bara) au Kamisheni ya Kazi (Zanzibar)

TAESA na Kamisheni ya Kazi baada ya kuuhakiki na kuuthibitisha mkataba watampatia barua mfanyakazi itakayo muwezesha kuruhusiwa na Idara ya uhamiaji kusafiri nje ya nchi.

Mfanyakazi baada ya kuwasili Oman atatakiwa kuletwa Ubalozini kujiandikisha na pia kupewa ushauri nasaha namna ya kuishi na kufanya kazi Oman na pia kuhakikisha wame katiwa bima na kufungulia akaunti ya benki na pia taratibu zote za uhamiaji zimekamilishwa.


Tathmini ya utekelezaji

Tangu kuanza kwa zoezi hili machi mwaka 2011, Ubalozi umeratibu ajira za Watanzania 8,358     hadi Kufikia Disemba 31, 2015, ambapo kati ya     hawa 7,251 ni watumishi wa majumbani, 388 watumishi wa saluni, madereva 290, wapishi na wahudumu migahawani 102 , mafundi magari 244, Kada zingine (walimu, wahadhiri, wauguzi, madaktari na wahandisi) 61

Hata hivyo takwimu za Wizara ya Kazi ya Oman zinaonyesha kuwa hadi kufikia Septemba 31,  2015 kuna Watanzania 9,543 wanaofanya kazi Oman, ambapo 8,483 ni wafanyakazi wa majumbani, mafundi mechanic 45, wauguzi watano, wahadhiri watano, madaktari 10, wahandisi watano, sekta ya huduma na takrima (services and hospitality ) 202 na     madereva 152, wakulima 50, wahudumu wa saluni 330 , walezi wa wazee na wagonjwa ( care giver)100.

Ukilinganisha takwimu za Ubalozi na zile za Wizara ya     Kazi ya Oman utaona kuwa kuna wafanyakazi 1,185     hawakupitia katika utaratibu uliowekwa na Serikali, wengi wa hawa ni wafanyakazi wa majumbani , wachache ni wale walio katika sekta rasmi ambao hawana     matatizo ukilinganisha na wafanyakazi wa     majumbani

Ubalozi umefanikiwa kupandisha kiwango cha     mshahara kutoka rial 30 walizokuwa wakilipwa     Watanzania hadi kufikia Rial 80 kiwango cha chini na kuanzia rial mia kwa wale waliokuwa na uzoefu.

Baadhi ya waajiri wamekuwa wagumu katika kutekeleza masharti ya ajira yaliyomo katika mikataba hasa mapumziko ya siku moja kila wiki na muda wa kazi, malipo ya kiinua mgongo na matibabu.

Uzoefu umeonyesha kuwa waajiriwa wengi bado hawaelewi masharti katika mikataba yao ya ajira, wanasaini kitu wasichokielewa au kusainiwa mikataba na wale wanaowafanyia mipango ya kuja Oman na wengine wengi hawasaini mikataba hii kwani hukabidhiwa dakika za mwisho uwanja wa ndege wanapoingia kwenye chumba cha kuondokea ( Departure)

Wizara imebaini kuwapo kwa waajiri wasio waaminifu ambao kwa kushirikiana na makundi fulani  Zanzibar na Dar es Salaam hutumia hila kukwepa utaratibu uliowekwa na Serikali

Hila zinazotumika ni kutoa hongo kwa watendaji wa taasisi mbalimbali katika  Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na Dar es Salaam zinazohusika na mchakato wa safari za kimataifa,  kumpeleka mtumishi kwa viza ya matembezi au kuwasafirisha kupitia Kenya na hivyo kukwepa masharti ya uhamiaji yanavyohitaji kuwapo mkataba au kutumia mikataba ya kugushi, 

Ubalozi kwa mwaka 2014 ulifanikiwa kuwakamata wafanyakazi  38 walioweza kusafiri bila kuwa na mkataba na wafanyakazi 15 wakiwa na mikataba feki, Machi 2015, ubalozi ulianzisha mkakati  maalumu wa kwenda Uwanja wa Ndege wa Muscat kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanaowasili Oman kufanya kazi wamefuata utaratibu uliowekwa, katika kipindi cha siku kumi ubalozi umefanikiwa kuwanasa Watanzania 83 ambao waliweza kuondoka Tanzania kuja Oman bila kufuata utaratibu,  wanane kati ya hawa wakiwa na mikataba feki. Ubalozi ulizuia pasipoti zao na kuwataka waajiri wao kufika ubalozini kukamilisha utaratibu uliowekwa

Kumekuwa pia na matukio kadhaa ya ukiukwaji wa masharti ya mkataba kwa baadhi ya waajiri kama vile kupunguza mshahara, kutowakatia bima mpya mara bima ya awali  inapomaliza muda wake.

Kwa upande wa watumishi nao kumekuwa na wenye matatizo ya uvivu, uhuni , matumizi ya simu kupita kiasi, matumizi mabaya ya mtandao, kukutwa wajawazito au na magonjwa ya kuambukiza wanapofanyiwa uchunguzi wa afya zao wanapowasili Oman na hivyo kutia shaka usahihi wa taarifa za uchunguzi wa afya zao kwa vipimo waliofanyiwa Tanzania. 

Pia watumishi wengine kuwa si weledi wa kazi wanazokuja kuzifanya. Lakini pia kumekuwa na tatizo la Watanzania kutaka kupewa upendeleo maalumu dhidi ya waajiri wao hata pale wafanyakazi hao wanapokuwa wamekosea na pale ambapo ubalozi unatoa haki kwa mwajiri huwa hawaridhiki na hivyo kuanza kutoa tuhuma za Ubalozi kuwapendelea waajiri.

Itaendelea wiki ijayo
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles