26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

NASA YALENGA KUZOA KURA MILIONI 10

JOSEPH HIZA Na MASHIRIKA,

VYAMA vikuu katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya, Chama tawala cha Jubilee na Muungano wa upinzani wa NASA vimeshawapitisha rasmi wagombea wake wa urais tayari kwa kipute chao cha Agosti 8 mwaka huu.

Wakati Jubilee na vyama vingine vitano ndiyo vimempitisha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kutetea viti hivyo wiki iliyopita, NASA iliwapitisha Raila Odinga na mwenza wake Kalonzo Musyoka wiki mbili zilizopita.

Mikakati ya kampeni imeshaanza kuvuja huku Jubilee wakitamba kuwa watashinda kwa asilimia 70 ya kura lakini NASA wakisema kura milioni 10 kati ya zaidi ya kura milioni 19 za waliojiandikisha ni halali yao.

Rais Kenyatta ameshaunda timu tofauti sita za kimkakati kwa ajili ya kazi mbalimbali, ambazo pamoja na mambo mengine zitatumia helkopta, kuonesha miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanikishwa na utawala huo na kuvitumia vyama rafiki na watu muhimu walioasi kutoka upinzani kupenya maeneo ya upinzani.

Siri ya mkakati huo ilikuja baada ya Rais Kenyatta kuhudhuria Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa vyama vitano rafiki– Maendeleo Chap Chap, Narc Kenya, Kenya Patriotic na Economic Freedom, ambalo lilimpitisha kugombea urais kwa mara nyingine.

Uamuzi huo wa kushirikisha vyama hivyo unatokana na kile Rais Kenyatta alichoona tishio linaloletwa na ushirika wa upinzani ulioamua kuweka tofauti na masilahi pembeni kuunganisha nguvu ya vyama vitano kuhakikisha kiongozi huyo mwana wa mwasisi wa taifa hili, Mzee Jomo Kenyatta anang’oka Agosti 8.

Ijumaa iliyopita Kenyatta alikutana na vigogo kutoka kaunti 14 Ikulu mjini Nairobi kupanga mikakati ya kupata kura kutoka maeneo yao.

“Watangaza nia wa Jubilee kutoka kaunti 14 tulikutana kupanga mikakati ya uchaguzi,”Kenyatta alieleza katika akaunti yake ya Twitter baada ya mkutano huo.

“Watangaza nia hao wa Jubilee ni pamoja na magavana na wabunge waliojiunga kutoka vyama vya upinzani,”alisema Kenyatta.

Kwa upande wa upinzani, mgombea wa urais Odinga, Kalonzo Musyoka ambaye ni mwaniaji mwenza, kiongozi wa Amani National Congress (ANC), Musalia Mudavadi, Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Gavana wa Bomet Isaac Ruto (Chama Cha Mashinani) walikutana katika eneo la Pwani kupanga mikakati ya kuendesha kampeni kote nchini.

Katika mkutano huo uliofanyika mapema wiki iliyopita, vinara hao  wa NASA pamoja na kamati ya wataalamu walikubaliana kuweka mikakati ya kuhimiza wapigakura kujitokeza kwa wingi Agosti 8, hasa katika maeneo yanayodhaniwa kuwa ngome zao na kuzuia wizi wa kura.

Kamati hiyo inajumuisha msomi wa masuala ya uchumi David Ndii, Dan Ameyo, Mutakha Kangu, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na Koitamet ole Kina.

Kwa mujibu wa msemaji wa Odinga, Dennis Onyango, mkondo wa kwanza wa kampeni za NASA utaanzia maeneo yanayochukuliwa kuwa ngome za Jubilee kama vile Bonde la Ufa na Kaunti za Meru na Embu.

“Muungano wa NASA utazuru katika maeneo mbalimbali ya Bonde la Ufa kuhakikisha Chama Cha Mashinani (CCM) kinakuwa na uungwaji mkubwa,” anasema Onyango.

NASA pia unapanga kupiga kambi katika kaunti 10, ambazo kura za maoni zimeonyesha muungano huo na chama cha Jubilee vinatoshana nguvu.

Kaunti hizo ni Nairobi, Kajiado, Narok, Trans Nzoia, Mandera, Garissa, Wajir, Samburu, Marsabit na Isiolo.

Vigogo wa NASA na kamati ya wataalamu waliafikiana kuunda kamati zitakazolinda vituo vya kupigia kura kote nchini, ambazo zitatuma matokeo katika kituo kikuu cha NASA cha kujumlisha matokeo.

Kalonzo, hivi majuzi, alinukuliwa akisema kuwa kila kituo kitakuwa na mawakala watano wa kulinda kura, ikimaanisha kuwa NASA itaajiri mawakala wasiopungua 225,000 kulinda vituo vyote zaidi ya 45,000 kote nchini humo.

Wakati wa hafla ya uzinduzi wa mwaniaji wa urais wa NASA katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi, mwezi uliopita, vinara wa muungano huo walisema kibarua kilichosalia ni kuhimiza wafuasi wao kujitokeza kwa wingi kupiga kura Agosti 8 na kuzuia wizi.

Kamati za kulinda kura vituoni zimeundwa kufuatia madai yanayotolewa na Odinga kuwa alibwagwa na Rais Kenyatta katika uchaguzi wa 2013 kwa sababu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) 'ilimwongezea’ kura milioni mbili za bure.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa, Peter Ngure anakiri kuwa Rais Kenyatta na naibu wake Ruto hawapaswi kusherehekea kwani haitakuwa rahisi kuishinda NASA.

Ngure anasema Odinga ataweza kumsumbua Rais Kenyatta iwapo ilani yake ya uchaguzi itaegemea katika ahadi ambazo Jubilee haikutimiza kama vile kukabiliana na ufisadi, na njaa na hata kuboresha uchumi.

Hata hivyo, Ngure anasema kuwa NASA wana kibarua cha kuhimiza wapiga kura, haswa kutoka katika maeneo ya Magharibi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria (LSK) Okong’o O’Mogeni anasema gharama ya juu ya maisha inayopanda kila uchao huenda ikafanya Wakenya kupigia kura NASA kwa matumaini kwamba bei ya bidhaa hizo itapungua.

“Hali ya uchumi imezorota chini ya uongozi wa Jubilee. Bei ya bidhaa muhimu kama vile unga, mafuta, umeme inazidi kupanda. Hali hii huenda ikakasirisha Wakenya na kuamua kuchagua viongozi mbadala,” anasema  O’Mogeni.

Wakili O’Mogeni pia anasema hatua ya Odinga kufichua sakata mbalimbali kama vile wizi wa zaidi ya Sh1.2 bilioni katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), sakata ya Eurobond kati ya nyinginezo pia imemfanya kuaminiwa na baadhi ya wapiga kura.

Odinga ameahidi kupunguza gharama ya maisha, kushughulikia deni ambalo Kenya inadaiwa na mataifa ya kigeni na hata kufutilia mbali karo katika shule za sekondari ndani ya siku 100 za uongozi wake iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Odinga pia anasema takwimu za wapiga kura zinaonesha ngome za NASA zina idadi kubwa ya watu waliojiandikisha huku akisema kuwa upinzani unalenga kupata kura milioni 10.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa pia wanasema kuwa tofauti na 2013 ambapo Odinga alipata kura chache  zaidi katika maeneo ya Bonde la Ufa na Kati, huenda mambo yakawa tofauti.

“Odinga alipata kura chache katika maeneo ya Kati na Bonde la Ufa 2013 kutokana na wimbi la kesi zilizokuwa zikiwakabili Rais Kenyatta na Ruto.”

Lakini sasa kesi hazipo tena hivyo, kuna uwezekano Odinga atavuna kura katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa na kaunti za Jubilee kama vile Meru,  Embu na Tharaka Nithi,”  anasema Danson Omari, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Kulingana na Omari, kupokelewa kwa Odinga katika maeneo ya Eldoret na Kaunti za Meru na Tharaka Nithi kwa taadhima ni ishara kwamba NASA itavuna kura kadhaa kutoka maeneo hayo.

“Odinga atapata kura katika eneo la Meru kwa sababu anaonekana kuwa na suluhisho kuhusu changamoto inayokumba wakulima wa miraa.

Licha ya serikali ya Jubilee kuwapa kitita cha Sh1 bilioni, fedha hizo hazijawasaidia wakulima kutatua matatizo yao yanayotokana na ukosefu wa soko. Kila Odinga anapozuru maeneo hayo huwaahidi kuwatafutia soko katika mataifa ya kigeni,” akasema.

Omari anasema hatua ya Serikali ya Jubilee kushindwa kutimiza baadhi ya ahadi ilizotoa kwa wakazi wa maeneo ya Kati na Bonde la Ufa pia huenda ikawezesha NASA kuvuna kura katika sehemu hizo.

Aidha wanasema kwamba uwapo waMudavadi aliyegombea urais mwaka 2013 na kupata kura 500,000 ni mtaji mwingine kwa Odinga aliyeshindwa na Kenyatta katika uchaguzi huo kwa tofauti wa kura Zaidi ya 600,000 achilia mbali pia uwapo wa Isaac Ruto kutoka Bonde la Ufa.

Hata hivyo, Odinga ana kazi kubwa ya kufanya kutimiza ndoto yake ya kuwa Rais wa taifa hilo angalau kwa muhula mmoja kama alivyoahidi ili kumpisha kalonzo mwaka 2022.

Kwamba haitakuwa rahisi kwake kumwondoa Uhuru madarakani hasa iwapo wafuasi wake hawatajitokeza kwa wingi na iwapo Jubilee itacheza vyema karata zake. Ni muda tu utaamua!

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles