32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa kihistoria

ELIZABETH HOMBO, DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameshuhudia utiliaji saini wa ujenzi wa mradi wa kihistoria wa umeme wa Bonde la Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge kati ya Serikali ya Tanzania na Misri, ambao umesubiriwa kwa zaidi ya miaka 40 sasa.

Mradi huo uliosainiwa Ikulu jijini Dar es Salaam jana, ulishuhudiwa pia na Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Mostafa Madbouly ambaye aliongozana na Waziri wa Nishati wa nchi hiyo, Dk. Mohamed Shaqqah pamoja viongozi wengine 150.

Akizungumza baada ya utiliaji saini, Rais Magufuli alisema mradi huo utakaozalisha megawati 2,100 na kugharimu Sh trilioni 6.558, fedha zitakazo tumika ni za walipa kodi wa Tanzania.

Pamoja na mambo mengine alisema mradi huyo utakapokamilika, utasaidia pia kutunza mazingira tofauti na baadhi ya ambao watu wanaoupinga wanadai kuwa utaaribu mazingira.

Alisema kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa utekelezaji wa mradi huo, baadhi ya watu walipinga mradi huo kwa kigezo kuwa utaleta tishio la uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya Selous jambo alilosoma si la kweli.

Alisema mradi ulikuwa uanze tangu mwaka 1970 lakini leo ni zaidi ya miaka 40 ndiyo unaanza kutekelezwa.

“Mradi huu umepigwa vita sana kwa hiyo sishangai kama mawazo haya ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere tangu mwaka 1970 leo ndiyo tunakuja kuweka saini zaidi ya miaka 40, nilijua matatizo waliyokuwa wanapambanayo.

“Nafahamu wapo wanaosema mradi huu utaharibu mazingira, hiyo si kweli hata kidogo…ninavyojua mradi huu utasaidia kutunza mazingira.

“Kwanza ni kwa sababu umeme wa maji ni rafiki wa mazingira, pili eneo la kutekeleza mradi huu ni ndogo ambalo ni asilimia 1.8 hadi 2 ya eneo zima la Selous.

“Kwa hiyo utakapokamilika utazalisha umeme kwa miaka 60 na kwamba gharama za kuzalisha umeme wa maji ni ndogo kuliko zingine, gharama za kuuza pia itakuwa nafuu kwa hiyo ukikamilika umeme utashuka.

“Bei ya umeme kwa nchi yetu ni kubwa kuliko nchi zingine mfano umeme hapa kwetu kwa unit unauzwa dola za kimarekani senti 10.7 wakati Misri ni senti 4.6, Korea ya Kaskazini ni chini ya senti 8, China nayo ni hivyo hivyo chini ya senti 8.

“Afrika Kusini ni senti 7.4, India ni senti 6.8, Ethiopia senti 2.4. Hii ndiyo inatufanya gharama za uzalishaji kuwa juu kwa sababu gharama za umeme ziko juu.

“Kwa hiyo mradi huu utakapokamilika tutaunza umeme kwa bei ya chini, viwanda vyetu product (uzalishaji) yake itakuwa kwa bei ya chini na tutaweza kushindana kwenye soko la kimataifa,”alisema Rais Magufuli.

Alisema kabla ya kuamua kuanza kwa mradi huo, walikaa chini na kutafakari kwamba ni chanzo kipi kitafaa katika mazingira ya sasa ya kupata umeme ndipo wakabaini mradi huo ndiyo unafaa.

Alisema mradi huo ukikamilika pia utapunguza ukataji wa miti kwa sababu kwa utafiti uliofanyika mwaka 2015, mgawanyo wa matumizi ya aina ya nishati ya kuni na mkaa ni asilimia 92, petrol asilimia 7 na umeme asilimia 1.

“Kwa mujibu wa utafiti huo, matumizi ya mkaa yanakadiriwa kuwa ni tani milioni 2.3 kwa mwaka na inatarajiwa kuongezeka ifikapo mwaka 2030.

“Ili kuzalisha tani moja ya mkaa kwa kutumia matanuru ya kienyeji zinahitaji tani 10 mpaka 12 za miti ili upate tani moja ya mkaa, hii maana yake ni kwamba kwa ni milioni 2.3 za mkaa tunazotumia kwa mwaka zinahitaji milioni 23 hadi tani milioni 27 za miti.

“Utafiti unaonyesha kwa kila miti 18 inatoa magunia 26 ya mkaa yenye kilo 53 zitatumia miti milioni 30. Hivyo basi kukamilika kwa mradi huu utasaidia kuokoa idadi kubwa ya miti na hivyo kutunza mazingira yetu ndiyo maana nasema huu ni rafiki wa mazingira kwa sababu utaokoa miti inayokatwa kwa ajili ya mkaa na kuni,”alisema.

Kutokana na hilo, aliwataka wapenda mazingira wote kuunga mkono mradi huo mkubwa wa kihistoria nchini kwa sababu utatunza mazingira na kuinua uchumi.

Aliipongeza kampuni hiyo ya Arab Contractors ya nchini Misri kwa kushinda zabuni ya mradi huo  na kwamba wanao utaalamu wa ujenzi kuliko taifa lolote.

Alisema mkandarasi wa mradi huo, atapewa miezi sita kwa ajili ya kukusanya vifaa na miezi 36 kwa ajili kukamilisha mradi huo.

Alitoa wito kwa kampuni hiyo kukamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa na ikiwezekana kabla ya muda ili kudhirihisha kwamba waafrika wakiamua wanaweza.

“Naamini mkandarasi atakamilisha mapema kwa sababu Wamisri ni wachapakazi sana, kwa hiyo wakiukamilisha mapema itadhihirisha hiyo historia ya Wamisri.

“Nilipokuwa nazungumza na rais wa Misri amenihakikisha kwamba wameamua kujenga mradi huu na kwamba yeye anauchukua kama project yake na alitamani sana awepo kusaini nikamwambia siku ya jiwe la msingi aje.

“Kwa hiyo nitashangaa Arab Contractors  wakiuchelewesha nitasikitita sana… hela ya kulipa kwa asilimia 15 tunazo leo kwa sababu mradi huu umepigwa sana vita.

“Na leo mradi huu una baraka za pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu utiliaji saini umeshuhudiwa na viongozi wa dini haijawahi kutokea viongozi wa dini wakawa wengi kiasi hiki, nimefurahi na viongozi wa dini ninawashukuru sana.

“Haiwezekani viongozi wote hawa wa dini wote waje halafu mradi usifanyike na kule Misri ndiko Yesu alikokimbilia,”alisema.

Aliwataka wananchi wa maeneo ambayo mradi unatekelezwa waunge mkono na wasifuge mifugo karibu na mradi huu.

Rais Magufuli pia alisema kukamilika kwa utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo, kutaiwezesha Tanzania kuzalisha kiasi kikubwa cha umeme kitachokasaidia kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na mradi wa reli ya kisasa, hatua itakayoiwezesha kupiga hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wake.

Alisema baadhi ya watu waliokuwa wakiombwa mkopo wa kujenga mradi huo walikuwa wakikataa lakini wakiambia waingie ubia na Serikali katika ujenzi wake walikuwa wako tayari.

“Hii ni kwasababu walitaka kufanya iwe biashara, wafanye maamuzi wao kuhusu bei, siku nyingine wakiamua wafanye wanayotaka waseme hakuna umeme na treni yetu watu washindwe kusafiri,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Misri, Dk. Mostafa Madbouly alisema Serikali yake itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kiufundi, kitaalamu na kidiplomasia na Tanzania ili kuhakikisha kuwa ndoto za waasisi wa urafiki wa mataifa hayo zinaweza kutimizwa ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Madbouly alisema katika kipindi cha miaka michache ijayo, Serikali ya Misri kupitia kwa taasisi zake za kiuchumi zitaendelea kuwekeza kwa kasi zaidi nchini Tanzania ili kuhakikisha kuwa miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa na Tanzania inaweza kuleta tija kwa wananchi wake.

Naye Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alisema mradi huo ukikamilika utakuwa mkubwa kuliko yote Afrika Mashariki kwa kuzalisha megawati 2,115.

Alisema bwawa linalofuata kwa kuzalisha umeme mwingi ni la Bujagari nchini Uganda, likitarajiwa kuzalisha megawati 300 tu.

“Tanzania sasa kwa Afrika Mashariki ni ya kwanza tukiwa na megawati 2,115. Bwawa lililokuwa likiongoza kabla yetu ni lile la Bujagari la Uganda bado linajengwa na lina megawati 300..

“Tanzania itakuwa ya nne na kwamba nchi inayoongoza kwa kuwa na mabwawa makubwa ni Ethiopia, ambapo bwawa lake la  Renaissance linaloendelea kujengwa litazalisha megawati 6,450 na ujenzi wake utakamilika mwaka 2022.

“La pili lipo Mambira Nigeria linazalisha megawati 3,050, la tatu liko Ethiopia ambalo ni Shaika likizalisha megawati 2,160. Bwawa la nne ndiyo la kwako Rais (John) Magufuli (akimaanisha Stiegler’s Gorge).

 “Bwawa la tano liko Misri (Aswan Dam) la megawati 2,100 na la sita liko Angola la Rauka linalozalisha megawati 2,066. Hongera sana Rais Magufuli,”alisema Dk. Kalemani.

Alisema mbali na Afrika, Tanzania ni kati ya nchi 60 zenye mabwawa makubwa ya kuzalisha umeme, huku akisema jumla yapo 70.

Waziri huyo alisema bwawa kubwa kuliko yote liko China likizalisha megawati 22,500, la pili nchini Brazil (megawati 14,000) na jingine China (megawati 13,860).

“Malengo yetu ni kufikisha megawati 5,000 mwaka 2020 na megawati 10,000 mwaka 2025 kwa hiyo kukamilika kwa mradi huu ni matumaini yetu kwamba pamoja na kuwa na umeme, lakini umeme wa uchumi wa viwanda mradi huu ni injini ya uchumi wetu.

“Mradi huu unatekelezwa na makandarasi kutoka Misri wakifanya kazi kubwa nne; kujenga kuta mbili kubwa zenye urefu wa mita 1,025 na kimo cha mita 131, kujenga bwawa kubwa la kutunza maji lenye urefu wa kilomita 100 na upana kilomita 25 na uwezo wa kubeba mita za ujazo bilioni 35.2.

“Kazi ya tatu ni kujenga mtambo wa kuzalisha umeme, utakuwa na mitambo tisa na kila mmoja utazalisha megawati 235 na jumla yake zitakuwa megawati 2,115.

“Kazi ya nne ni kujenga kituo cha kufua umeme mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda,”alisema Dk. Kalemani

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles