26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Kilo tatu za Cocaine zamtupa jela maisha

KULWA MZEE , DARES SALAAM

RAIA wa Msumbiji,  Ana Chissano (36)amehukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la kukutwa na kilo 3.03 za dawa zakulevya aina ya cocaine hydrochloride.

Mshtakiwa huyo alihukumiwa jana baada ya kutiwa hatiani na Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi

Hukumu  hiyo ilisomwa mbele ya  Jaji Lilian  Mashaka baada upande wa mashtaka kuweza kuthibitisha mashtaka hayo pasipo Kuacha shaka.

Alisema mahakama imeridhishwa  na ushahidi  wa mashahidi sita wa  upande wa mashtaka waliofika mahakamani  hapo kutoa ushahidi wao.

Mahakama  imeamuru dawa hizo za kulevya kuteketezwa kwa utaratibu unaostahili.

Akitoa hukumu hiyo jana, Jaji Lilian Mashaka alisema ametoa adhabu hiyo kulingana na kifungu cha sheria namba 15 (1) (b) cha Sheria namba 5 ya 2015 ya kuzuia na  kupambana na dawa za kulevya.

“Sheria hiyo inaelekeza mtu yoyote anayejihusisha na dawa za kulevya anapopatikana na hatia anapaswa kutumikia kifungo cha maisha jela.

“Nimezingatia sababu zilizotolewa na mshtakiwa, lakini mahakama pia imezingatia sheria ambayo imeweka adhabu kwa mtu kupitia kifungu hicho inayosema mtu yeyote  atakayepatikana na hatia kwa makosa ya dawa za kulevya basi adhabu yake ni jela maisha.

 “Kwa mamlaka hayo, nakuhukumu wewe Ana Moisie Chissano kutumikia kifungo cha maisha kwa kosa ulilolitenda na iwapo haujaridhika na maamuzi una haki ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani,” alisema Jaji Lilian.

Jaji Lilian alisema dawa za kulevya ni tatizo linaloikabili jamii hivyo kwa njia yoyote yanapaswa kuzuiwa na jitihada za pamoja zinatakiwa zitekelezwe ili kupunguza tatizo ikiwemo kuwaadhibu wote wanaojihusisha na dawa za kulevya.

Wakili wa Serikali Constantine Kakula alipotakiwa kueleza kama mshtakiwa ni mkosaji wa mara ya ngapi, alidai hawana kumbukumbu ya makosa lakini  makosa hayo yamekuwa yakiongezeka na kusababisha kupotea kwa nguvu kazi kutokana na kutumia dawa za kulevya.

Kakula aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwa watu wote wanaojihusisha Mshtakiwa kupitia Wakili wake, Hassan Ruwhanya aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa sababu ni kosa lake la kwanza na kwamba anategemewa na familia kwa kuwa ana watoto wawili wadogo.

“Tunaomba mahakama izingatie kutoa adhabu nyepesi kwa sababu tangu mshtakiwa afikishwe mahakamani amekaa mahabusu miaka mitatu na ameonesha kujutia kosa lake na amejifunza,” alidai Wakili Hassan.

Awali, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi akisaidiana na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula na Batlida Mushi walidai kuwa mshtakiwa aliwasili nchini Novemba 16,2016 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na ndege ya Shirika la Ethiopia E 827 akitokea Addis Ababa Ethiopia.

Kadushi alidai kabla ya kufika maofisa wa Polisi walikuwa na taarifa kwamba mshtakiwa huyo atawasili na ndege hiyo na atakuwa amebeba dawa za kulevya.

Alidai mshtakiwa huyo alikamatwa na alivyopekuliwa kwenye begi lake alikutwa na  bahasha na ndani yake kulikuwa na unga uzaniwao kuwa ni dawa za kulevya.

Pia alidai baada ya unga huo kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali alithibitisha kuwa ni dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye uzito wa kilogramu 3.03.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,277FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles