24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 6, 2024

Contact us: [email protected]

MPANGO WA MKURABITA KWA WAKULIMA USIMAMIWE KIKAMILIFU

 

Na BENJAMIN MASESE

-MWANZA

PALE Serikali inapofanya jambo jema ambalo lilikuwa kikwazo kwa wananchi katika maisha yao ya kila siku, inapaswa kupongezwa lakini pia kuikosoa pale inapokuwa imeteleza ni moja ya hatua yenye ustawi kujirekebisha ama kujitafakari na si ugomvi tena.

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa na kaulimbiu nyingi juu ya suala la kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ambacho ni uti wa mgongo lakini mafanikio yake yameendelea kuwa hafifu na kufikia wananchi wengi  vijijini hususani vijana kukimbilia mjini na kujihusisha na biashara ya ujasiriamali yaani machinga.

Asilimia kubwa ya watu wanaojihusisha na kilimo vijijini ni wazee na kinamama ambao kwa namna moja au nyingine wamekosa njia mbadala ya kujikimu.

Hivyo basi kutokana na wakulima wengi kutowezeshwa kielimu, kitaalamu, zana za kisasa za kilimo, pembejeo na nyinginezo, ndio sababu kubwa ya asilimia 90 ya wakulima kuwa masikini.

Katika utawala wa Rais John Magufuli imefanya mambo mengi ambayo mengine yanaonekana kuwa na mafanikio kwa muda mfupi na yapo ambayo Watanzania wanayaweka katika matazamio ya baadaye. Septemba 13 na 15 mwaka huu, Serikali  chini ya Ofisi ya Rais, Idara ya Urasimishaji Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), ilianza kutoa semina  kwa wakulima wa kata mbili za Kasololo na Matale Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Semina hiyo iliwafikia wakulima 200 kati ya 900 ambao walifanikiwa kupimiwa mashamba yao na kupatiwa hati za kimila, ambapo walipata fursa ya elimu ya kutumia ardhi ndogo kwa mavuno mengi, namna ya kilimo cha kisasa, mbegu bora na wapi zinapatikana.

Kwa mujibu wa Meneja wa Mkurabita Taifa kutoka Ofisi ya Rais, Makame Juma Pandu, Serikali imejitathmini juu ya namna ya kufikia Tanzania ya viwanda na kubaini kuwa wakulima ndio chachu kubwa na ndio wenye malighafi za viwanda, hivyo wameamua kutumia fedha za ndani ili kuwakwamua wakulima kwa kuwapa elimu namna ya kuondokana na umasikini wa  kilimo cha kujikimu kwenda cha biashara.

Pia alisema asilimia 90 ya wakulima nchini ni masikini kutokana na kujikita kwenye kilimo cha kujikimu badala ya biashara, hivyo sasa Serikali imeanza kuwawezesha wakulima kupitia taasisi za fedha na kutoa elimu juu ya namna ya kutumia ardhi yao  kupata mtaji na kulima kwa kisasa.

Awali alisema mpango wa kuwawezesha wanyonge ulikuwa ukitegemea fedha za wafadhili, kitendo ambacho kilisababisha kusuasua, ambapo hivi sasa Serikali imeamua kuundeleza kwa kutumia fedha za ndani ambapo alizitaka halmashauri 54 kati ya 180 zilizoingizwa katika mpango huo kuusimamia ipasavyo.

Kama nilivyotangulia kusema, kama kuna jambo zuri linalofanywa na Serikali ni wajibu wetu tuipongeze, binafsi naipongeza Serikali kwa uamuzi huo wa kuwakumbuka wakulima ambao wengi nchini ni wanyonge kiuchumi licha ya kumiliki ardhi kubwa na kuitumia katika shughuli za kilimo.

Hatua ya Serikali kukaa na taasisi za fedha na kuwataka kutambua hati za kimila ni jambo jema, kwani litasaidia kuwakwamua kiuchumi baada ya kukopeshwa fedha ambapo walitoa elimu namna ya kuzitumia ili kupata mkopo na kulima kilimo cha biashara na kisasa.

Ni ukweli usiopingika kwamba malighafi zinazohitajika viwandani zinatoka kwa wakulima, hivyo Tanzania  ya viwanda haiwezi kufanikiwa na hata kufikia uchumi wa kati bila wakulima kubadilika.

Ni wakati mwafaka kwa maofisa maendeleo ya jamii, biashara na ushirika, kilimo na wengine, kuhakikisha  wanawasimamia wakulima hao ili kuanzisha  vikundi vya saccos vya wakulima ili kila jambo likaloanzishwa  liwe na mafanikio.

Ni imani yetu Watanzania kwamba dhamira ya Serikali ni kufikia uchumi wa kati ndio maana imeamua kuanza na wakulima kutokana na malighafi zote zinatoka kwao, lakini mafanikio hayo yatatokana na wataalamu wa halmashauri kuwa karibu na wakulima wao, vinginevyo yatajirudia yale yale ya kaulimbiu bila utekelezaji.

Imeelezwa kuwa mpango huo wa Mkurabita ndani ya Kata ya Kasololo na Matale umesaidia kumaliza mgogoro kati ya wakulima na wafugaji baada ya kutengwa  maeneo ya kilimo na malisho ya mifugo, jambo lililoondoa migogoro na mapigano yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara na kuhatarisha amani na usalama kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles