24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

MORRISON, NCHIMBI MTEGONI U/TAIFA

Asha Kigundula

YANGA leo wanashuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kusaka ponti tatu mbele ya Mbao FC, huku nyota wao, Bernard Morrison, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na wengineo wakiwa mtegoni kuelekea pambano lao dhidi ya Simba Jumapili hii.

Katika mchezo huo wa leo utakaoanza saa1:00 usiku, Yanga watatakiwa kushinda kwa idadi kubwa ya mabao ili kuwapa matumaini wapenzi wao wanaojiandaa kupepetana na Simba.

Mbali ya kusaka pointi tatu, nyota wa Yanga watasubiriwa kwa hamu kuona wajibikaji wao leo kama utawashawishi wapenzi wao kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa Jumapili.

Yanga chini ya Kocha Mkuu, Luc Eymael, wanaamini bado wana nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo licha ya kupitwa pointi 21 na Simba inayoshika usukani ikiwa na alama 65, huku wao wakijikusanyia 44.

Kikosi cha Eymael kinaingia uwanjani na kumbukumbu nzuri ya kushinda mchezo wao uliopita kwa kuifunga Alliance mabao 2-0, shujaa wao akiwa ni Nchimbi.

Ni wazi iwapo Yanga watashinda leo, hali hiyo itawatia nguvu mashabiki wao kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Taifa Jumapili, lakini kinyume chake, wengi wataingia mitini.

Hivyo basi, Morrison, Nchimbi, Niyonzima, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na wengineo walioonyesha kandanda la hali ya juu kwa siku za hivi karibuni, watatakiwa kuzidi kuwapagawisha wapenzi wa leo kama sehemu ya kusafisha njia kuelekea pambano la Jumapili.

Hata hivyo, iwapo Yanga itashinda mchezo huo, bado itabaki katika nafasi ya nne kwani waliopo juu yao, Azam na Namungo, wana alama 48 kila moja, wakati Wanajangwani hao watafikisha 47.

Kuelekea mchezo huo wa leo, Eymael amewataka mashabiki wao kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa sapoti wachezaji wakati wote wa kipute hicho.

Kwa upande wa Mbao, wanashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting kwa kufungwa mabao 2-0.

Mbao chini ya kocha wake mpya, Abdulmutik Haji ina kazi ya ziada ya kuzuia mashambulizi makali ya washambuliaji wa Yanga ambao wameonekana kuwa na uchu wa kufunga mabao.

Timu hiyo yenye makazi yake jijini Mwanza inahitaji ushindi ili kujinasua kutoka katika hatari ya kushuka daraja.

Mbao inashika nafasi ya 18 katika msimamo ikiwa na pointi 22, ilizovuna ndani ya mechi 25.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles