26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Morogoro ijumuishwe viwanja vya ndege vyakuboreshwa 

Na Shermarx Ngahemera



MOROGORO kijiografia ni karibu sana na Dar es Salaam kwani umbali wake ni kilomita 190 tu, lakini utawala wa barabara umefanya umbali huo kuwa kilomita 300 kutokana na usumbufu na muda unaotumika kusafiri kwa gari  na hivyo kukosa sifa ya kuwa na usafiri mwafaka.

Dar hadi Morogoro wasafiri wote wa magari madogo na mabasi ya umma siku hizi hutumia saa sita na kufanya umbali na muda unaotumika kuwa gumzo kwa abiria na wamiliki wa vyombo hivyo kudai kuwa wanapata hasara kwa safari kuwa chache kwa siku. Ni haraka kwenda Mtwara umbali wa kilomita 400 kuliko kwenda Morogoro.

Serikali imesema itavifanyia maboresho makubwa viwanja 11 vya ndege nchini, kikiwemo cha Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa, ili kuwa na mtandao mzuri wa huduma ya usafiri wa anga kitaifa na unaojitosheleza vilivyo.

Lakini Morogoro haimo kwa madai kuwa ni karibu ya Dar es Salaam na Dodoma na hivyo kuchukuliwa  kuwa  ni hali hasi ya kupata uwanja badala ya kuwa fursa kubwa ya kufanikisha usafiri wa haraka na salama kwa sehemu hizo tatu.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa, alipotembelea na kukagua Kiwanja cha Ndege cha Sumbawanga, ambako ujenzi wake kiwango cha lami na upanuzi unatarajiwa kutumia zaidi ya Sh bilioni 55.9, alivitaja viwanja vingine vya ndege ambavyo vinatarajiwa kufanyiwa maboresho makubwa kuwa ni Kiwanja cha Nduli mkoani Iringa, Songea, Manyara, Geita, Kigoma, Tabora, Bariadi, Shinyanga, Tabora na Musoma.

Kimkakati wa ulinzi na usalama itakuwa bora zaidi na Morogoro ingejumuishwa ili tuwe  na uhakika kufikisha watalii kwa muda mfupi zaidi kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Udzungwa, Selous  na Ruaha.

Itakua murua kama Morogoro itaingizwa kwenye hiyo programu hasa kwenye zoezi mahususi la kuchechemua utalii wa Kongani ya Kusini. Morogoro ina hifadhi tatu za Selous, Mikumi na Udzungwa na hivyo inastahili kwa sifa zake na si kwa unazi tu.

Kwa kuzingatia usalama wa eneo na maumbo halisi kiwanja kitapendeza  kama kitajengwa Dakawa na hivyo kufikika kirahisi kwa wanaokwenda pande zote ikiwamo Dodoma, Tanga, Iringa na Dar es Salaam. Itapendeza sana kwani Morogoro ni mji wenye viwanda, vyuo vikuu na vivutio tosha vya utalii na vile vile mji uko kati ya Dar na Dodoma, majiji shindani na vinara nchini. Hivyo basi ima faima Morogoro ipate uwanja wa ndege kwani treni SGR si hoja kwani ina jicho moja na barabara ya jongoo.

Wazo hili ni sahihi ukizingatia kuwa barabara zetu si salama na hivyo ni vizuri kuwalinda wasomi wetu na wengine ambao ni rasilimali kubwa katika mkakati wetu wa kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati kutoka madereva viruu barabarani.

Inawezekana kabisa kuipatia Morogoro huduma hiyo adhimu kupitia mpango wa PPP ili kufanikisha azma hiyo kama vigezo vitazingatiwa.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles